Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Joyce Ndalichako |
Na Dotto Mwaibale
Juni 8, 2012.
LICHA ya Jeshi la Polisi kuzuia maandamano ya Waislamu ya kwenda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kushinikiza kujiuzulu kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Joyce Ndalichako, walifanikiwa kukusanyika kwa staili yake kwenye viwanja vya Kidongo Chekunduku jijini Dar es Salaam leo na kuipa Serikali siku saba kutoa majibu ya madai yao.
Waislamu hao, walifika katika viwanja hivyo kwa staili ya kuingia na mabasi madogo aina ya Coaster na magari madogo na mara baada ya kuteremka walitoa mabango yenye ujumbe tofauti pia wakiwepo wanafunzi na akina mama kwenye maandamano hayo.
Baadhi ya mabango hayo yalikuwa na ujumbe uliosomeka NECTA ivunjwe huku mengine yakishinikiza viongozi wa Baraza la Mitihani la Taifa, kujiuzulu kutokana na kashifa ya kudidimiza elimu kwa wanafunzi wa Kiislamu.
Katika hatua nyingine, walimtaka Katibu Mkuu wa NECTA na Wiraza ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wajiuzulu kutokana na kashifa hiyo.
Waislamu hao, wakiwa wamekusanyika katika viwanja hivyo, Polisi walifika na kuwachukua viongozi wao, akiwemo Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Kiislamu, Shabani Mapeyo, Selemani Daud na Kondo Bungo, ambapo waliwapeleka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa ajili ya kupeleka madai yao ambapo walipokelewa na Ofisa mmoja kwa niaba ya Naibu Waziri Shukuru Kawambwa.
Akizungumza baada ya kutoka katika ofisi ya Naibu Waziri, Mapeyo alisema walipokelewa na kukabidhi madai yao na kuahidiwa kufanyiwa kazi katika kipindi kifupi kijacho.
Hata hivyo, Waislamu hao, walitoa wiki moja kwa Serikali kutoa majibu ya madai yao kinyume na hapo, wapo tayari kumwaga damu ili kufanikisha jambo hilo walilodai ni haki yao na wanafunzi wa Kiislamu kwa ujumla.
Waislamu hao, walitoa mapendekezo matano ambayo waliitaka Serikali iyafanyie kazi.
Katika mapendekezo hayo la kwa nza wamemtaka Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Joyce Ndalichako kujiuzulu mara moja ili kulinda heshima ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Pendekezo letu la pili tunataka Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Mitihani na Mfumo wa Kompyuta kufukuzwa kazi " alisema Selemani Daud.
Alilitaja pendekezo la tatu kuwa ni kuundwa kwa tume huru ya kulichunguza Baraza hilo, utendaji wake wa kazi kwa muda wa miaka 10 iliyopita ili kubaini madai yao.
Pendekezo la nne likiw ni kuchukuliwa kwa sheria za kinidhamu dhidi ya wahusika wote waliohusika kwa njia moja ama nyingine katika kuhujumu matokeo ya wanafunzi wa Kiislamu.
Na la mwisho alisema kuwa muundo mzima wa Baraza hilo uzingatie uwiano wa dini zote kuliko ilivyo sasa ambapo wamejaa Wakristo, jambo ambalo linawanyima haki Waislamu.
Alisema tangu mwaka 1973, Baraza hilo, halijawahi kuongozwa na Muislamu hali inayoonesha katika nchi hii hakuna Muislamu msomi anaye weza kushika nafasi hiyo.
"Watoto wengi wa Kiislamu wanahangaika mitaani kwa kusukuma mikokoteni wakati walikuwa wakijiweza kimasomo na hiyo yote imetokana na kudhulumiwa haki yao ya masomo kwa nafasi zao kupewa Wakristo" alimaliza Daud.
No comments:
Post a Comment