Hali ya hatari ambayo imekuwa ikitumika nchini Misri kwa miongo mitatu na kuyapa majeshi ya usalama ya Misri madaraka ya kupindukia kwa kuwakamata washukiwa na kuwafikisha katika mahakama maalum, imeondolewa.
Sheria ya hali ya hatari ilianzishwa mwaka 1981 na Rais Mubarak, kufuatia mauaji ya mtangulizi wake, Anwar al-Sadat.
Watawala wa kijeshi wa Misri ambao walitwaa madaraka baada ya Rais Hosni Mubarak kung'olewa madarakani mwaka jana walionyesha kuwa wasingeirejesha tena sheria hiyo baada ya kumalizika muda wake usiku wa kuamkia leo.
Kuondolewa kwa sheria hiyo, lilikuwa dai kubwa la waandamanaji wapenda demokrasia ambao walichochea uasi dhidi ya Bwana Mubarak.
hofu ya raia
Baadhi ya raia wa Misri walihofia nchi hiyo kungekuwa na ombwe la madaraka iwapo sheria hiyo ingeondolewa. Hata hivyo, baraza kuu la majeshi lilitoa taarifa kuwahakikishia raia wa Misri kuwa '' litaendelea na majukumu yake ya kitaifa ya kulinda nchi hadi pale serikali mpya itakapochukua madaraka''.
''Hii ni hatua kubwa'' Hossan Bahgat, mwanaharakati wa haki za binadamu ambaye amekuwa akikampeni sheria hiyo itolewe, alisema.
Sheria ya hali ya hatari ilikuwa kiungo muhimu kwa utawala wa Rais Mubarak, ambaye mara kadhaa alivunja ahadi za kuiondoa.
No comments:
Post a Comment