TANGAZO


Friday, June 1, 2012

Rais Dk. Shein apongezwa na Ofisi yake

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein
Na Rajab Mkasaba


Ikulu, Zanzibar  
1.6.2012                                                                                            

OFISI ya Rais  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi imezipongeza juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein za kukutana na viongozi na watendaji wa kila Wizara na kueleza kuwa changamoto anazowapa zimeweza kuwasaidia katika upangaji na utekelezaji wa kazi zao pamoja na kusimamia maadili ya matumizi ya fedha.

Uongozi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi chini ya Waziri wake Mhe. Dk. Mwinyihaji Makame ulieleza hayo katika mkutano wa kuangalia utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo kwa kuangalia robo tatu za utekelezaji wa Bajeti  ya mwaka wa fedha 2011-2012 na kulinganisha na robo  ya kwanza na ya pili pamoja na vipaumbele na malengo kwa mwaka wa fedha 2012-2013.
 Mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ulikuwa chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein pia, ulihudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Uongozi wa Ofisi hiyo ulieleza kuwa  juhudi anazozichukua Dk Shein katika uongozi wake ni za kupigiwa mfano katika kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wote ikiwa ni pamoja na kuangalia maslahi ya wafanyakazi wote wa sekta ya umma, wakulima na wananchi wote kwa jumla.
Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa Wazanzibari kadhaa wanaoishi nchi za nje wameitikia wito wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wa kuwataka kuchangia na kuekeza katika sekta za kijamii, elimu na afya, na kutolea mfano ujenzi wa madarasa matano katika skuli ya Unguja Ukuu.
Pia, uongozi huo ulieleza kuwa kazi ya ujenzi wa Chuo Kipya cha Mafunzo Hanyegwa Mchana inaendelea kwa kukamilisha michoro itakayotumika kujenga chuo hicho na kununua baadhi ya vifaa vya ujenzi
Ofisi ya Rais kwa kupitia Ofisi ya Usajili na Kadi za Utambulisho imeendelea kuwasajili wananchi waliotimiza masharti ya kupewa vitambulisho vile vile vipindi kadhaa vimetayarishwa na kurushwa katika Shirika la ZBC redio kwa lengo la kuwaelimisha wananchi.
Akisoma utangulizi juu ya taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi hiyo  Mhe. Waziri Mwinyihaji  alisema kuwa mkazo zaidi umewekwa na ofisi hiyo katika utekelezaji wa shughuli ambazo zinalenga kuinua hali za wananchi kiuchumi na kupunguza kero zao za kijamii.
Aidha, alisema kuwa Ofisi imeweza kuratibu na kusimamia utekelezaji wa malengo ya MKUZA II, Dira 2020 na malengo ya Melenia pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015 ambapo utekelezaji wake umezingatia vipaumbele vilivyowekwa.
Waziri huyo pia, alieleza kuwa vipaumbele vimewekwa katika kuendeleza Umoja wa Kitaifa na mshikamano, kuimarisha uwezo, utoaji wa huduma ikiwemo usafishaji wa miji na uendeshaji wa Serikali za Mitaa, Mikoa na Wilaya sanjari na utekelezaji wa miradi kumi ya maendeleo.
Nae Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad aliipongeza Ofisi hiyo na kusisisitiza kuimarisha mashirikiano zaidi katika utendaji wa kazi ambayo ndiyo yaliyoipa mafanikio makubwa afisi hiyo.
Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa Wafanyakazi, viongozi na watedaji wote wa afisi hiyo kwa kushirikiana pamoja na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendeleza mashirikiano zaidi katika utendaji wa kazi katika ofisi hiyo huku akitoa pongezi kwa jinsi inavyo inavyoshirikiana nae katika juhudi za kuwaletea maendeleo wananchi. Aidha, alieleza kuwa afisi hiyo inapaswa iendeleze juhudi zake ili iwe mfano wa kuigwa na wengine.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na Uongozi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ulio chini ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia Waziri wake Mhe. Dk. Mwinyihaji Makame ambaye akisoma utangulizi wa taarifa juu ya utekelezaji  wa malengo ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa alaieleza vipaumbele ilivyoviweka ni pamoja na kutatua migogoro ya ardhi kwa kutoa elimu na kufanya ziara pamoja na vikao mbali mbali.
Kwa upande wa Baraza la Manispaa, uongozi huo ulieleza mikakati yake iliyojiwekea katika uzoaji taka na uondoaji mifugo ndani ya eneo la Manispaa ya Zanzibar na kudhibiti uchimbaji wa mchanga usiofuata taratibu na ujenzi holela katika maeneo yasiofaa.
Aidha, uongozi huo ulieleza vipaumbele vyake  katika kuimarisha majengo ya Ofisi kwa kuyafanyia marekebisho na kuanza ujenzi wa ofisi mpya, kuimarisha mfumo wa ukusanyaji na udhibiti wa mapato.
Dk. Shein kwa upande wake, alitoa pongezi kwa juhudi za uongozi huo kwa utendaji wao wa kazi na kueleza haja ya kuiimarisha miji  ili iweze kuvutia ikiwemo manispaa ya mji wa Zanzibar pamoja na kuendeleza kuzitafutia ufumbuzi kwa mashirikiano ya pamoja changamoto mbali mbali zilizopo katika Mikoa, Wilaya na Halmashauri zake.

No comments:

Post a Comment