Marehemu Willy Edward |
Na Ahmed Makongo, Mugumu
Juni 23, 2012
MWILI wa aliyekuwa mhariri mkuu wa Gazeti la Jambo Leo, Willy Edward Obunde, umezikwa leo nyumbani kwao katika kijiji Morotonga, nje kidogo ya mji wa Mugumu mkoani Mara.
Mazishi ya mhariri huyo, yalihudhuriwa na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, waandishi wa habari, viongozi wa Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti kapteni mstaafu James Ryamungu, viongozi wa vyama vya siasa, madhebu ya dini, pamoja na wananchi mbalimbali.
Aidha, mazishi ya mhariri huyo, pia yalihudhuriwa na mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mngeja pamoja Mkuu mpya wa Wilaya ya Magu, ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari, Jacqline Liana.
Ibada ya mazishi hayo, iliongozwa na Askofu wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mara, Hilkiah Omindo, ambaye aliwataka wananchi kujiandaa kwa kufanya matendo mema na kumtumikia Mwenyezi Mungu.
Akitoa salamu kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, Mwenyekiti wa CCM, mkoani Shinyanga, Khamisi Mngeja, amesema kuwa waandishi wa habari wamepata pigo kubwa kwa kuondokewa na mwenzao ambaye alikuwa ni mchapakazi, mwadilifu na anayefuata maadili na weledi wa uandishi wa habari.
Willy Edwar (38), alifariki dunia ghafula akiwa mkoani Morogoro, usiku wa kuamkia juni 17, mwaka huu, wakati akiwa kwenye semina ya uandishi wa habari za Sensa ya watu na makazi.
Marehemu Willy Edward, alikuwa mhariri mkuu wa gazeti la Jambo Leo na ameacha watoto watatu na mjane mmoja, Mungu alitoa na Mungu ametwaa, jina la Mungu iliimidiwe, na hivyo tunaomba aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi, Amina.
No comments:
Post a Comment