Rais wa shirikisho la soka barani Ulaya, Uefa Michel Platini anasema njia bora ya kukabiliana na ubaguzi wa rangi katika mchezo wa soka ni kwa waamuzi kusimamisha mechi wakati inabainika kuna ubaguzi huo.
Wiki iliopita kipindi cha BBC cha Panorama kilionyesha matukio ya ubaguzi wa rangi katika viwanja vya Poland na Ukraine, wenyeji wa mashindano ya mataifa bingwa barani Ulaya mwaka 2012, yanayoanza siku ya Ijumaa.
" Muamuzi anaweza akamaliza mechi. Sasa wana uwezo huo wakati suala la ubaguzi wa rangi linapojitokeza," alimwambia mhariri wa michezo wa BBC David Bond.
" Nafkiri, hiyo ndiyo njia nzuri ya kukabiliana na ubaguzi wa rangi katika mchezo huu."
Platini alikanusha taarifa kuwa hadhi yake itashuka kama kutatokea matukio ya ubaguzi wa rangi katika mashindano ya mwaka huu 2012.
" Hadhi yangu, kwa kuwa kuna wabaguzi wa rangi nchini Poland na Ukraine - unafanya mzaha? Unafkiri ni jukumu langu kwa wabaguzi wote wa rangi barani Ulaya au England au Ufaransa?" alisema.
" Jukumu langu ni kukabiliana na tatizo hilo - na nimejitahidi kubadilisha sheria, kubadilisha kanuni, kusaidia kwa kauli mbiu ' Watu wote ni sawa' na ' Isifanyike Tena'. Tunawasaidia sana, tunafanya mengi kukabiliana na ubaguzi wa rangi - lakini si jukumu langu kwa jamii nzima.
No comments:
Post a Comment