TANGAZO


Thursday, April 12, 2012

Viwanja vya Ndege watakiwa kuweka maslahi ya Zanzibar mbele

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar, Hamd Masoud


Na Nafisa Madai-Maelezo Zanzibar.
WAZIRI wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar, Hamad Masoud Hamad ameitaka Bodi ya Mamlaka ya Viwanja vya ndege kutoweka mbele maslahi binafsi, badala yake wajikite zaidi na kazi kwa ajili ya maslahi na maendeleo ya Zanzibar.
Waziri Hamad ameeleza hayo alipokua akizindua rasmi Bodi ya mamlaka hiyo katika ukumbi wa Mamlaka ya viwanja hivyo Kisauni nje kidogo ya mji wa Zanzibar ambapo aliieleza bodi hiyo kazi yoyote ikiongozwa na tamaa  maendeleo yake kupatikana inakuwa kwa shida sana.
Amesema ili Nchi iweze kupata maendeleo ya haraka ni lazima watu wanaopewa dhamana ya kuongoza wawe na mashirikiano makubwa na kukaa pamoja  katika kufuatilia matatizo yaliyopo katika sehemu wanazoziongoza.
Alisema hapo awali Mamlaka hiyo ilikuwa katika hali mbaya sana kiasi ambacho ilikuwa ikiitia aibu mamlaka hiyo kwa wageni ambao waliokuwa wakiingia na kutoka katika kiwanja cha ndenge  kwa kukuosa bodi ambayo ilikua ikiangalia matatizo yanayokabili viwanja hivyo.
Waziri Masoud pia alitaka bodi hiyo mara tu itakapoanza kufanya kazi zake iangalie kwa umakini suala la wafanyakazi wake ili waweze kujua idadi ya watakaoendelea kwa lengo la kufanyakazi kwa ufanisi.
Sambamba na hilo Waziri huyo amesema  bila ya kuwepo kwa wafanyakazi wenye taaluma katika mamlaka hiyo haitoweza kuwa na sifa za kimataifa  za kuwahudumia  wageni wanaoingia na kutoka  katika uwanja wa ndege wa Zanzibar.
Aidha waziri huyo aliwaasa wafanyakazi hao kujenga uaminifu katika utendaji wa kazi zao kwani vitendo vya udokozi vinaweza kupoteza haiba ya uwanja huo.
Aliongeza kuwa kumfanyia kitendo kibaya mgeni mmoja kunaweza kupoteza wageni wengi jambo ambalo linaweza kurudisha nyuma malengo yaliyokusudiwa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Captain Saidi Ndubugani amesema hivi sasa Mamlaka yake itakuwa na uwezo mkubwa katika kufanya kazi kwani hapo awali walikuwa wanapata matatizo katika kufanya maamuzi yanayohusu mamlaka hiyo.
Aidha alisema Mamlaka hivi sasa ipo katika hali ya ushindani wa kibiashara  kati ya Tanzania Bara na Kenya hivyo kuundwa kwa bodi hiyo itaweza kuwasaidia katika kuimarisha huduma mbalimbali za Mamlaka hiyo.
Hata hivyo alisema mamlaka yake inakabiliwa na changamoto kubwa ya uvamizi wa kiwanja, ulipaji wa fidia kwa wananchi waliohamishwa katika maeneo karibu ya kiwanja hicho pamoja na kukatisha wanyama katika njia inayopita ndege ambapo amesema imekua ikirudisha nyuma hatua zinazochukuliwa na mamlaka.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo Abdulghan Himid Msoma amesema yeye binafsi na wajumbe wa bodi yake wameahidi kuwa watafanya kazi kwa uzalendo kwa ajili ya maendeleo ya mamlaka hiyo.
Hakuna maendeleo bila ya changamoto na nipo tayari kukabiliana na changamoto hizo kwa hali na mali bila ya kujali maslahi yoyote” alisema Msoma.

No comments:

Post a Comment