UNITED
REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
Fax: 255-22-2113425
|
![]() |
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O.
BOX 9120,
DAR
ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Katika
mahojiano yake leo, Alhamisi, Aprili 5, 2012, na Redio One, ikiwa ni kauli yake
ya kwanza baada ya Mahakama Kuu ya Arusha kutangaza kumvua ubunge, aliyekuwa
Mbunge wa Arusha Mjini, Bwana Godbless Lema, amedai kwa jazba sana kuwa hukumu
ya Mheshimiwa Jaji Gabriel Rwakibalira imetokana na maelekezo ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Ikulu.
Kauli hii
ya Bwana Lema ni upuuzi. Siyo Mheshimiwa Rais Kikwete wala Ikulu imeingilia kati
kesi yake kwa namna yoyote ile, iwe ni kwa kupiga simu ama kuzungumza na
Mheshimiwa Jaji Rwakibalira.
Kwa hakika,
haijapata kutokea Mheshimiwa Kikwete, tokea alipoingia madarakani, Desemba 21,
2005, akaingilia, kwa namna yoyote ile, mwenendo wa kesi yoyote ile katika
Mahakama yoyote na ya ngazi yoyote katika Tanzania. Na wala hakusudii kufanya
hivyo wakati wote wa muda wake uliobakia wa uongozi. Siyo kazi ya Rais kutoa
hukumu ama kuelekeza namna ya kutoa hukumu katika kesi zilizoko Mahakamani.
Rais hana madaraka wala mamlaka hayo.
Aidha,
kauli ya Bwana Lema ni ukosefu mkubwa wa adabu na heshima kwa Mahakama ambao ni
Muhimili Huru usioingiliwa na Serikali ama na Muhimili mwingine katika maamuzi
yake. Bwana Lema amekuwa kiongozi kwa muda sasa, hivyo ni lazima atambue jambo
hili kubwa na muhimu katika mfumo mzima wa utawala wa nchi yetu.
Ni jambo
lisilokuwa na mshiko wala tija, na kwa kweli ni bahati mbaya, kwamba Bwana Lema
anajaribu kuingiza mambo yasiyohusika katika jambo la dhahiri kabisa kuwa ni la
kisheria ambalo msingi ni hoja na maelezo mahakamani.
Bwana Lema
asitafute visingizio kwa yaliyomfika kwa sababu hakuna mtu mwingine wa kumbebea
msalaba huu. Badala ya kutafuta
mchawi asiyekuwepo, ni vyema Bwana Lema angekaa chini na kuangalia ni sababu
zipi za kisheria zilizomfanya ashindwe na kama ameridhika kuwa hakutendewa haki
akate rufani kwa mujibu wa sheria na taratibu. Tunaomba wananchi wampuuze. Ameshindwa kesi kwa makosa yake aliyofanya hana mtu wa
kumlaumu bali ajilaumu mwenyewe
Mwisho.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
05 Aprili, 2012


No comments:
Post a Comment