TANGAZO


Wednesday, April 25, 2012

Di Matteo apigiwa debe aendelee Chelsea

Meneja wa muda Roberto di Matteo anastahili kuendelea kukinoa kikosi cha Chelsea kilichoingia hatua ya fainali ya Ubingwa wa Kandanda wa Ulaya, kwa mujibu wa aliyekuwa meneja wa klabu hiyo Avram Grant.
Meneja wa muda wa Chelsea Roberto Di Matteo
Meneja wa muda wa Chelsea Roberto Di Matteo
Chelsea ikicheza na wachezaji 10 ilifanikiwa kuwatoa Barcelona katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali ambapo timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 kwenye uwanja wa Nou Camp na kufanikiwa kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2.
Grant, ambaye alitimuliwa licha ya kuiongoza Chelsea hadi fainali ya mwaka 2008, alisema mmiliki wa timu hiyo Roman Abramovich hatabiriki.
"Nadhani Roberto anastahili takriban mwaka mmoja zaidi lakini Abramovich kuna baadhi ya wakati anafikiria tofauti," aliifahamisha BBC.
Di Matteo ambaye aliwahi kuichezea Chelsea katika nafasi ya kiungo, aliteuliwa kushika umeneja wa muda hadi msimu huu utakapomalizika baada ya Abramovich kumtimua Andre Villas-Boas mwanzoni mwa mwezi wa Machi.
Grant alisema Abramovich atakuwa amefurahishwa kwa Di Matteo kuibadili Chelsea, kwa kuiongoza hadi fainali ya Ubingwa wa Ulaya na Kombe la FA.
"Ameshawatimua mameneja wengi lakini hadi sasa kiwango cha kandanda kimekuwa kikiporomoka na timu nayo ilikuwa inaporomoka, Grant ambaye kwa sasa ni meneja wa klabu ya Partizan Belgrade alizidi kuifahamisha BBC.
"Nadhani katika macho yake timu inakwenda juu na Di Matteo anayo nafasi ya kukabidhiwa mikoba na kuendelea."
Di Matteo alipongeza mafanikio makubwa ya kikosi chake baada ya kucheza mechi ya marudiano dhidi ya mabingwa watetezi kwa muda wa saa moja wakiwa 10 baada ya John Terry kutolewa kwa kadi nyekundu.
Msaidizi wa Di Matteo Eddie Newton amesema matokeo hayo yanatokana na kazi kubwa ya kujituma katika klabu hiyo.
Avram Grant ambaye ni rafiki wa Abramovich, awali alijiunga na Chelsea akiwa na wadhifa wa mkurugenzi wa kandanda lakini aliteuliwa kuwa meneja mwezi wa Septemba mwaka 2007 baada ya kuondolewa kwa Jose Mourinho.
Grant naye baada ya kutimuliwa anafasi yake ilichukuliwa na Mbrazili Luiz Felipe Scolari, aliyedumu kwa miezi saba kabla ya Carlo Ancelotti kushika hatamu.
Ancelotti alifanikiwa kushinda Ligi ya England na Kombe la FA mwaka 2010 lakini alifurushwa mwaka mmoja baadae hali iliyomkuta pia Villas-Boas aliyeshika hatamu chini ya miezi tisa.

No comments:

Post a Comment