TANGAZO


Tuesday, April 17, 2012

Balotelli asema hataondoka Man City

Mario Balotelli amesema "hana nia ya kuondoka" Manchester City msimu huu.
Mario Balotelli akioneshwa kadi nyekundu
Mario Balotelli akioneshwa kadi nyekundu
Meneja Roberto Mancini alikiri angekuwa tayari kumuuza mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Italia baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu walipopambana na Arsenal.
Mancini baadae alijirudi kwa kauli hiyo na akamuonya Balotelli hana budi kubadilika iwapo anapendelea kubakia katika klabu hiyo.
"Mustakabali wangu? Bado nina mkataba na City na sina nia ya kubadilisha fulana," alisema mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 21.
Wakati Manchester City ikiwa haina nia thabiti ya kumuuza mchezaji huyo, Kitengo cha michezo cha BBC kimefahamu kuwa klabu hiyo inajiandaa kusikiliza maombi yoyote ya maana iwapo kuna klabu itataka kumnunua Balotelli msimu ujao.
Mshambuliaji huyo wa Italia amekuwa akihusishwa kurejea kwao na kujiunga na klabu mbili kubwa za huko, Inter na AC Milan ambao imefahamika zinamfuatilia kwa karibu mshambuliaji huyo.
Hata hivyo, Balotelli anaamini uzoefu anaoupata England unamsaidia kukua. Ameshafunga mabao 17 katika mechi 31 msimu huu, lakini ameshatolewa nje mara mbili.
"Ninachofikiria kwa sasa ni kushinda ubingwa," aliliambia gazeti la michezo la Italia liitwalo La Gazzetta dello Sport. "Kwa nini kila mara mnanihusisha na Inter na Milan?"
"Sina hamu na Italia. Ligi Kuu ya England ni sehemu bora na imenifunza mengi. Nilipokuwa Inter Milan nilikuwa nikimuita mama yangu kunisaidia hata kwa matatizo madogo madogo. Sasa nawajibika kuyakabili peke yangu. "
Uhusiano wa Mancini na Balotelli amekuwa chanzo cha matatizo msimu huu.
Mancini alitania kuwa angemchapa makonde mshambuliaji huyo kila siku ingekuwa wanacheza timu mmoja, lakini Balotelli amesisitiza ana bahati kufanya kazi na meneja wake huyo wanaotoka nchi mmoja, aliyemsajili kutoka Inter Milan kwa kitita cha paundi milioni 24 mwezi wa Agosti mwaka 2010.
"Bado nahitajika kubadilika, hasa kama mcheza kandanda," aliliambia gazeti hilo. "Nina bahati kufanya kazi na Mancini, mmoja wa mameneja bora duniani.

No comments:

Post a Comment