Arsene Wenger amepongeza "ujasiri" uliooneshwa na kikosi chake na hatimaye kufanikiwa kupata ushindi dakika ya mwisho ya mchezo dhidi ya Newcastle.
Wenger amesema: "Kilichofanya tuwafunge ni ujasiri wetu."
"Sikutarajia kama tutashinda. Nilikuwa nlimwambia msaidizi wangu tunahitaji kushambulia mara moja zaidi na tutafunga."
Arsenal walikuwa nyuma ya Tottenham kwa pointi 10 katika mbio za kuwania nafasi ya tatu, kabla ya pambano lao mwezi uliopita, lakini Gunners kwa sasa wapo nyuma ya majirani wao hao kwa pointi moja tu baada ya kuendeleza ushindi katika mechi zao zilizopita.
Kikosi hicho cha Wenger kilianza kufungwa katika uwanja wa Emirates Stadium katika mechi ya nne mfululizo wakati Hatem Ben Arfa alipoachia mkwaju pembeni mwa nguzo ya lango, lakini Robin van Persie alijibu kwa kishindo ndani ya dakika moja tu na kuandika bao lake la 44 katika mechi 45 za Ligi Kuu ya England, kabla Vermaelen kuipatia Arsenal bao la ushindi dakika ya mwisho ya mchezo.
"Hii ilikuwa ni mechi muhimu kwa timu zote," alisema Wenger.
"Newcastle ni timu nzuri na unahitaji kitu maalum kuweza kuwalaza."
Newcastle walijaribu kutupunguza kasi lakini tulifanikiwa kuwapenya mara nyingi. Tulipata dakika tano za nyongeza na hizo zilitusaidia kushinda.
"Tulishinda katika dakika ya mwisho dhidi ya Sunderland, Liverpool na sasa Newcastle. Hii inaonesha tunadhamira ya ushindi.
Walcott - ambaye alicheza kwa kiwango cha juu katika muda wote wa mchezo - anaamini timu yao inaweza kuwaengua Tottenham katika nafasi ya tatu.
"Tottenham hawana budi kujitazama upya sasa," alisema Walcott.
"Kutokana na kikosi tulichonacho na tukiwa na wachezaji wengi ambao wanarejea baada ya kuumia, tunaamini tutaweza kufika mbali zaidi.
"Umekuwa ni msimu wa kukurukakara nyingi za kufanya vizuri na kuporomoka, lakini namna unavyomaliza ndio jambo la muhimu zaidi."
Kwa upande wake meneja wa Newcastle Alan Pardew anahisi kikosi chake kilistahili kupata angalao pointi moja, lakini aliwataka wachezaji wake wasihuzunike sana kwa kupoteza mchezo hali itakayopunguza matumaini yao ya kucheza soka ya Ulaya.
Newcastle wapo nyuma kwa pointi tano dhidi ya Chelsea wanaoshikilia nafasi ya tano zikiwa zimesalia mechi 10 kabla msimu haujamalizika.
"Kilikuwa ni kibarua kigumu," Pardew aliongeza.
"Tumecheza na kikosi ambacho kiwango chake kimeimarika na ari yao iko juu. Tulijaribu kuwazuia wasicheze mchezo wao kwa muda mrefu na walituweka katika wakati mgumu.
"Kusema ukweli imetuumiza sana. Timu kubwa huwa zinafunga mabao dakika za mwisho. Kwa ujumla usiku huu tulistahili pointi moja.
"Tunakabiliwa na mchezo mgumu siku ya Jumamosi dhidi ya Norwich na tunahitaji kushinda, kwa hiyo tunahitajika kuhakikisha tunajitengeneza upya."
No comments:
Post a Comment