TANGAZO


Wednesday, March 28, 2012

Wanaovaa mavazi yasiyo ya heshima kuchuliwa hatua CBE

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) Athuman Ally Ahmed akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu kuanza kutumika kwa sera ya mavazi chuoni hapo. 

Na Aron Msigwa – MAELEZO, Dar es salaam.
Uongozi wa Chuo cha elimu ya biashara (CBE) kampasi ya Dar es salaam umesema kuwa hautasita kumchukulia hatua mwanafunzi au mfanyakazi  yeyote atakayefika chuoni hapo akiwa amevaa mavazi yasiyo ya heshima huku ukitoa wito kwa wananchi kuunga mkono kampeni hiyo yenye manufaa katika kujenga taifa lenye maadili mazuri.
Akizugumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Kaimu mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Bw. Athman Ally Ahmed amesema chuo hicho kimefikia uamuzi huo kufuatia kukithiri kwa vitendo vya uvaaji wa mavazi yasiyokuwa na staha vinavyofanywa na wanafunzi  wa kike na wale wa kiume wawapo chuoni hapo hali inayosababisha udhalilishaji wa utu wa wanafunzi ndani na nje ya chuo.
Amesema wanafunzi ambao wengi wao ni vijana chuoni hapo wamekuwa mstari wa mbele katika kuiga kila aina ya vazi kutoka tamaduni za watu wa magharibi hali ambayo ameielezea kuwa ni ukiukaji wa mila , desturi na tamaduni za mtanzania .
“Mtindo huu wa kuiga tamaduni za magharibi pasipokuangalia wapi tunakwenda haukubaliki hata kidogo,ukiangalia katika vyuo vingi vya elimu hapa nchini wanafunzi wamekuwa wakivaa mavazi ya ajabu na yasiyofaa kabisa katika maeneo ya chuo” amesema.
Amesema kuwa Chuo hicho  kimekaa na kubuni sera  ili kuyaondoa mavazi ambayo hayaruhusiwi kuvaliwa katika maeneo ya chuo  na kubuni sera ya mavazi kwa ajili ya wanafunzi  hali itakayowajengea  nidhamu wasomi  hao  wa fani mbalimbali pindi watakapomaliza masomo yao chuoni hapo.
Amefafanua kuwa  adhabu mbalimbali zitatolewa kwa wanafunzi watakaokiuka agizo la uvaaji wa mavazi yenye heshima amabazo ni pamoja na kuzuiliwa kupita getini kwa mwanafunzi husika kuingia katika eneo la chuo kwa wale wanaotoka nje ya hosteli na wale wanaoishi ndani ya eneo la chuo hawatapewa huduma yoyote kama vile kuingia darasani,kantini , maktaba au ofisi yoyote ya chuo.
Aidha amefafanua kuwa wanafunzi  ambao  hawatakua  tayari kufuata utaratibu huo watafikishwa mbele ya kamati ya nidhamu huku akibainisha kuwa adhabu itakayotolewa ni mwanafunzi kusimamishwa  chuo kwa  muda wa miezi mitatu.
Kwa upande wake makamu mkuu wa chuo hicho ambaye pia ni mkurugenzi wa mafunzo Bi. Bertha Kipillimba amesisitiza kuwa zoezi hilo litawahusu wafanyakazi wote wa kampasi ya Dar es salaam na wanafunzi  zaidi ya 6000 wa chuo hicho.
Amesema hivi sasa taratibu hizo za uvaaji wa mavazi yenye staha zimeingizwa kwenye kanuni za chuo  na kuongezwa kwenye masharti ya fomu za kujiunga na chuo hicho huku akifafanua kuwa tayari wametoa kipindi cha wiki mbili kwa utekelezwaji wa kanuni hizo na watakaokiuka kuadhibiwa kwa mujibu wa kanuni hizo.
Naye mlezi wa wanafunzi wa hicho (Dean of Students) Bw. Faustin China amefafanua kuwa umefika wakati wa wanafunzi hao kujitambua huku akisisitiza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakinyoshewa vidole na jamii kuhusu suala la uvaaji na mienendo ya wanafunzi chuoni hapo.
“Tumesemwa vibaya kwa muda mrefu hatuwezi kuachia suala hili likaendelea, tunataka wanafunzi wetu wavae vizuri kwa mujibu wa kanuni tulizojiwekea ili kujenga heshima ya chuo” amesema.
Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi wamekuwa na maoni tofauti kuhusiana na uanzishawaji wa sera ya mavazi chuoni hapo wakieleza kuwa inaingilia uhuru wao wa kuamua huku wengine wakiupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuliona suala hilo na kulichukulia hatua ili kuleta na kulinda heshima ya chuo hicho.
 Eneo la mbele la jengo la Utawala la Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Kampasi ya Dar es salaam. 




 Baadhi ya wanafunzi wa CBE, kampasi ya Dar es salaam wakiwa darasani. (Picha na Aron Msigwa -MAELEZO)

No comments:

Post a Comment