Majeruhi wa milipuko ya Congo wakihudumiwa

Bado ni hatari kuingia eneo ambapo milipuko ilitokea siku ya Jumapili katika mji mkuu wa Congo, Brazzaville. Waokoaji wanasema kufikia sasa bado kunamilipuko midogo midogo ambayo ingali inashuhudiwa.
Na mwandishi wa BBC amesema inahofiwa kuwa kuna mamia ya maiti ambazo huenda zingali katika vifusi vya majengo yalioporomoka kutokana na milipuko hiyo ya Jumapili.
Serikali inasema idadi ya waliofariki ni 146 . Hata hivyo takwimu kutoka vyumba vya kuhifadhia maiti na madaktari wanasema kuwa idadi ya waliofariki imefikia zaidi ya 200 na wale waliojeruhiwa ni 1,500
Na maafisa wa kijeshi wamenukuliwa wakisema kuwa hatari nyegine inayokabili watu ni kutapakaa kwa vilipuzi . Hii inaleta hofu kuwa moto huenda ukatokea katika ghala la pili la silaha
Hospitali zilizoko Brazzaville zinawakati mgumu kukabiliana na idadi kubwa ya majeruhi.
Watu waliokuwa wakiishi karibu na kambi ya kijeshi nchini Congo, bado wanaendelea na shughuli ya kujaribu kuokoa mabaki ya mali yao iliyoteketea kufuatia mlipuko uliotokea katika kambi hyo na kusababisha vifo vya zaidi ya watu miaka moja hamsini.
Nyingi ya nyumba zilizokuwa karibu na kambi hiyo ya kijeshi ilikuwa imejengwa kwa mabati. Watu hao wanasema walipoteza mali yao yote wakati wa mlipuko huo uliosababisha na hitilafu za nguvu za umeme katika ghala moja ya silaha.
Ukuta unaozunguka kambi hiyo ya kijeshi ilianguka licha ya kuwa imejengwa na saruji.
Mmoja wa manusura wa mlipuko huo ameiambia BBC kuwa atajaribu kutafuta makaazi kutoka kwa jamaa wake na ikiwa atakosa atalazimika kuishi katika kambi za muda zilizojengwa na serikali.
Amesema miili ya watu ilikuwa imetapakaa katika bara bara za mji huo baada ya mlipuko huo siku ya jumapili.
Misaada ya kibinadamu inaendelea kutolewa kwa manusura wa mkasa huo. Hospitali kuu ya mjini humo bado inapokea watu waliojeruhiwa.
Baadhi yao wanaendelea kupkea matibabu katika hema zilizojengwa nje ya hospitali hiyo ya chuko kikuu na shirika na madaktari wasio na mipaka Médecins sans Frontières
Waziri wa huduma za jamii nchini humo na kamishna mkuu wa muungano wa ulaya kuhusu misaada ya kibinadm wamesema kuwa suala kuu kwa sasa ni kuhakikisha kuwepo kwa madaktari zaidi hasa madaktari wa upasuaji ili kutibu wale waliojeruhiwa.
Tatizo lingine linalokabili serikali ya nchi hiyo ni suala la silaha zilizotawanyika wakati wa mlipuko huo.
Mwakilishi wa shirika moja linalojihusiha na harakati za kupinga utumizi mabomu za kuzikwa ardhini, amesema raia kadhaa walionekana wakikusanya mabomu ya aina hiyo ambao haikulipuka bila kuwa na vifaa vya kujilinda.
Vile vile usalama wa kambai hiyo sio dhabiti kufuatia mkasa huo. Amesema kundi lake lilikuwa limetambua athari za ghala hilo la silaha wakati wa ziara yao katika kambi hiyo na kuwa walifahamisha utawala wa nchi hiyo na hawakuchukua hatua zozote.