Senegal itapambana na Oman tarehe 23 Aprili katika kujaribu kujipenyeza katika nafasi ya mwisho iliyosalia kwa upande wa michuano ya soka ya wanaume katika mashindano ya mwaka 2012 ya Olimpiki mjini London.
Oman, ambaye kwa hivi sasa iko chini ya mkufunzi wa zamani wa timu ya Cameroon, Paul Le Guen, iliweza kuishinda Uzbekistan 2-0 siku ya Alhamisi, na kuibuka kama mshindi katika mashindano ya kufuzu yaliyoyashirikisha mataifa matatu nchini Vietnam. Senegal ilifika hatua ya kushiriki katika mashindano hayo ya kufuzu mwezi Desemba, ilipomaliza katika nafasi ya nne, katika mashindano ya kwanza ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 23, yaliyofanyika nchini Morocco.
Mchezo kati ya Senegal na Omen utafanyika nchini Uingereza.
Droo ya michuano ya soka ya Olimpiki itafanyika mara tu baada ya mechi hiyo, tarehe 24 Aprili.
Naibu mwenyekiti wa chama cha soka cha Senegal, Louis Lamotte, ameielezea BBC kwamba ujumbe kutoka nchi yake uliweza kufuatia mechi za Vietnam.
"Sio jambo la kushangaza kwa kuwa Oman ni timu kubwa, tunafahamu wanacheza soka vizuri, lakini Senegal wanaweza kupata ushindi pia", alieleza.
Alisema pia watajitahidi kukandaa mechi nyingine moja ya kirafiki ya vijana chini ya umri wa miaka 23, kabla ya kupambana na Oman.
Mchezaji wa Oman, ambaye vile vile ni kipa wa Wigan, Ali Al Habsi, amefurahishwa sana na wazo la timu yao ya Olimpki kuweza kucheza nchini England.
"Ninafurahi sana kwa sababu mchezo kati ya Oman dhidi ya Senegal utafanyika Coventry," aliandika Al Habsi katika mtandao wa jamii wa Twitter.
Gabon, ambayo ndio nchi bingwa Afrika katika mashindano ya vijana wa umri wa miaka 23, Morocco iliyo katika nafasi ya pili, na Misri ikishikilia ya tatu, ni mataifa mengine ambayo yatawakilishwa katika soka mjini London katika mashindano ya mwaka 2012.
Korea ya Kusini, Japan na Imarati ni mataifa ya Asia ambayo tayari yamefuzu kushirikishwa katika mashindano ya London.
No comments:
Post a Comment