Serikali ya Libya inasisitiza kuwa ina uwezo wa kumfanyia kesi mkuu wa zamani wa usalama, Abdullah Sanussi, na imeomba arejeshwe nyumbani.
Kumetolewa wito kuwa Bwana Sanussi apelekwe Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, ICC, mjini Hague au Ufaransa, ambako ameshtakiwa kwa ugaidi.
Ingawa hakuna picha zilotolewa za Abdullah Sanussi tangu kuarifiwa kuwa amekamatwa nchini Mauritania, wakuu wa Libya wanasema wana hakika kuwa ametekwa, na wameomba kuwa arejeshwe nyumbani.
Mkuu huyo wa ujasusi wa Kanali Gaddafi, anakabili mashtaka kadha, pamoja na yale yanayohusu mauaji.
Serikali ya mpito ya Libya ina hamu kuwa arejeshwe nyumbani kufikishwa mahakamani haraka.
Lakini kuna wasiwasi, kwa sababu serikali kuu ya Libya bado haina nguvu, na bado hakuna mfumo wa sheria unaoweza kufanya kesi ya al-Sanussi au viongozi wengine wa zamani wa utawala wa Gaddafi.
Ufaransa imeshasema kuwa itapenda kumpata al Sanussi kwa sababu ya kuhusika kwake na shambulio la bomu kwenye ndege ya Ufaransa mwaka wa 1989.
Piya kuna wito mwengine kuwa mwanasiasa huyo apelekwe ICC, ambako anakabili mashtaka ya kushiriki kwenye shughuli za kufyeka upinzani wa Libya mwaka jana.
Wakuu wa Mauritania bado hawakusema vipi watajibu maombi hayo, na inaweza kuchukua muda kabla ya afisa huyo kurejeshwa nyumbani - afisa aliyechukiwa na kuogopwa kabisa nchini mwake.
No comments:
Post a Comment