Ashley Young alifunga mabao mawili wakati Manchester United ilipofanikiwa kupunguza wigo wa pointi na kuwa mbili dhidi ya wanaoongoza ligi ya kandanda ya England Manchester City.

Ashley Young akishangilia moja ya mabao yake na Rooney
Ashley Young akishangilia moja ya mabao yake na Rooney

Spurs walianza vyema mchezo huo, huku mlinda mlango wa Manchester United David de Gea alikaa imara na kumnyima bao Jake Livermore.
Lakini Manchester United walimaliza mchezo kwa aina yake, Wayne Rooney akianza kufungua lango la Tottenham alipounganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Ashley Young kipindi cha kwanza.
Young aliweza kufunga mabao mawili kipindi cha pili kabla ya Jermain Defoe aliyeingizwa dakika za mwisho kuifungia Tottenham bao la kufutia machozi.
Katika mchezo mwengine Pavel Pogrebnyak alifunga mabao matatu peke yake wakati Fulham ilipoivurumishia Wolves mabao 5-0 na kumuweka katika wakati mgumu meneja mpya wa Wolves Terry Connor .
Mshambuliaji huyo kutoka Urusi alianza kupachika bao katika dakika ya 36 alipounganisha mkwaju wa kona wa Damien Duff kabla ya kuunganisha mpira wa chini uliopigwa na Andy Johnson na kuandika bao la pili kabla ya mapumziko.
Clint Dempsey alifanikiwa kumpiga chenga mlinda mlango wa Wolves Wayne Hennessey na kufunga bao la tatu, kabla ya Pogrebnyak kwa mara nyingine kupachika bao la tatu kwa kuunganisha mkwaju uliopigwa na Johnson.
Na alikuwa Dempsey aliyefunga bao lake la pili na la tano kwa Fulham lililozidi kuichosha Wolves.
Naye Shola Ameobi aliifungia Newcastle bao muhimu la kusawazisha wakati walipokuwa wamebanwa na majirani wao Sunderland, ambao wachezaji wao wawili walitolewa nje kwa kadi nyekundu.
Nicklas Bendtner alifunga mkwaju wa penalti baada ya Mike Williamson kucheza rafu isiyolazima kwa Michael Turner, na kuipatia Sunderland bao la kuongoza.
Demba Ba alikosa kufunga mkwaju wa penalti kabla ya Ameobi kurejesha matumaini ya Newcastle kwa kufunga bao la kusawazisha dakika za nyongeza.
Stephane Sessegnon alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumpiga kiwiko Cheick Tiote, wakati Lee Cattermole alikumbana na kadi nyekundu baada ya mpira kumalizika alipooneshwa kadi ya pili ya manjano kwa kumtolea maneo ya kuudhi mwamuzi.