BW. JUMA SHABANI MGOO |
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA
KWA UMMA
BW. JUMA SHABANI
MGOO ATEULIWA KUWA AFISA MTENDAJI MKUU WA WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA
(TFS)
Waziri wa Maliasili
na Utalii Mhe Ezekiel Maige amemteua Bw. Juma Shabani Mgoo (51) kuwa Afisa
Mtendaji Mkuu (Chief Executive Officer) wa Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania (Tanzania Forest Services Agency - TFS).
Mhe. Waziri amefanya
uteuzi huo kwa mamlaka aliyo nayo chini ya Kifungu cha 9 (1) cha Sheria ya
Wakala wa Serikali Sura Na. 245, kama kilivyorekebishwa na Sheria ya Wakala wa
Serikali mwaka 2009.
Kabla ya uteuzi huo
Bw. Juma Mgoo alikuwa akitumikia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kama Kaimu
Mkurugenzi wa Usimamizi Rasilimali Misitu na Ufugaji Nyuki (Ag. Director of Resources
Management). Aidha, kabla ya Wakala wa Huduma za Misitu kuanza Bw.
Juma Mgoo alikuwa akifanya kazi Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii
kama Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji Misitu.
Bw. Juma Mgoo ambaye
ni mtaalam wa Misitu alihitimu Shahada ya Kwanza ya Misitu (BSc Forestry) katika Chuo
Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mwaka 1986. Baadaye alihitimu Shahada ya Uzamili
ya Uendelezaji wa Maliasili (MSc Natural Resources Management) katika
Chuo Kikuu cha Norway mwaka 1992. Pia alihitimu masomo ya juu ya Ujasiriamali (Post Gradute Diploma in
Entreprenuership and Enterprise Development) katika Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam mwaka 2006.
Bw. Juma Mgoo
ameitumikia Serikali katika vituo mbalimbali, pamoja na Songea kama Afisa
Misitu na Kigoma kama Afisa Misitu Mkoa wa Miradi ya Misitu. Pia alifanya kazi Makao
Mkuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kama Meneja Mradi wa Misitu ya Hifadhi na
Mikoko, Mratibu wa Programu Taifa ya Misitu na Ufugaji Nyuki Tanzania (NFBKP),
Mratibu wa Programu ya Kuendeleza Maliasili (Management of Natural Resources
Programme - MNRP) na Kiongozi wa Kamati ya Kuandaa Uanzishwaji wa Wakala
wa Huduma za Misitu Tanzania.
Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania ulianzishwa kisheria tarehe 1 Julai 2010, na kuanza kazi rasmi
tarehe 1 Julai 2011. Wakala huo umechukua shughuli za kiutendaji ambazo
zilikuwa zinatekelezwa na Idara ya Misitu na Nyuki chini ya Wizara ya Maliasili
na Utalii.
Uteuzi wa Bw. Juma
Mgoo kama Afisa Mtendaji Mkuu ni kuanzia tarehe 1 Desemba 2011 na utadumu kwa
kipindi cha miaka mitano hadi tarehe 30 Novemba 2016.
[MWISHO]
George
Matiko
MSEMAJI
WIZARA
YA MALIASILI NA UTALII
5
Machi 2012
Simu
0784 468047
No comments:
Post a Comment