TANGAZO


Thursday, March 15, 2012

Di Matteo asifia wachezaji wa Chelsea


Meneja wa muda wa Chelsea Roberto di Matteo amewapongeza wachezaji wake akiwaita "wasio na mfano" baada ya kuwalaza Napoli 4-1 na kufika hatua ya timu nane bora zitakazowania ubingwa wa vilabu vya Ulaya ama Champions League.
Roberto di Matteo akimkumbatia kwa furaha Drogba baada ya ushindi
Di Matteo akimkumbatia kwa furaha Drogba baada ya ushindi

Branislav Ivanovic alipachika bao la ushindi katika dakika za nyongeza na Chelsea kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 5-4 baada ya mabao ya awali ya Didier Drogba, John Terry na Frank Lampard.
"Baadhi ya wachezaji walikuwa wanashindwa kukimbia dakika za mwisho kwa sababu walichoka lakini hawakukata tamaa na kupigana kiume," alisema Di Matteo.
"Tulikuwa tunafahamu ingetuchukua muda mrefu kuibuka washindi lakini kila mtu alicheza vizuri sana."
Wakiwa na deni la kufungwa mabao 3-1 katika mchezo wa awali walipocheza Naples, Chelsea walifungua lango la wapinzani wao kwa bao la kichwa lililofungwa na Drogba.
Terry alipachika bao la pili kwa kichwa pia kutokana na mpira wa kona kabla Lampard kulipa deni kwa mkwaju wa penalti lakini mambo yaligeuka pale Gokhan Inler kipindi cha pili alipofumua mkwaju mkali na kuiandikia Napoli bao la pekee ambalo liliipatia nafasi nzuri kama mambo yangekwenda hivyo hivyo.
Lampard alilazimisha mchezo uende dakika thelathini za nyongeza kwa bao hilo la mkwaju wa penalti baada ya Andrea Dossena kuunawa mpira ndani ya sanduku la hatari na Ivanovic akamalizia kazi kwa kufunga bao la ushindi katika dakika ya 104 minutes.
Upangaji wa timu zitakazomenyana katika hatua ya robo fainali utafanyika siku ya Ijumaa na Chelsea imeungana na timu hatari za Apoel Nicosia, Barcelona, Bayern Munich, Benfica, Marseille, AC Milan na Real Madrid ambazo zimefanikiwa kucheza hatua hiyo.

No comments:

Post a Comment