Mshindi wa tuzo ya Nobel ya amani kutoka Yemen, Tawakul Karman, amesema Urusi na Uchina zinabeba jukumu la mauaji yanayotokea Syria, baada ya mataifa hayo kupinga kwa kura ya turufu azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana.
Chama kikuu cha upinzani cha Syria, SNC, kimelaani kura za turufu za Urusi na Uchina katika Baraza la Usalama kwamba zimeipa serikali ya Syria idhini ya kuuwa.
Shirika la habari la taifa la Syria limeunga mkono msimamo wa nchi mbili hizo na kusema utayapa shime mabadiliko ya kisiasa yaliyoahidiwa na serikali.
Na wapiganaji katika mji wa Homs wanasema vifaru vya jeshi vimekuwa vikiwekwa karibu na mitaa inayodhibitiwa na upinzani.
Mwandishi wa BBC mjini Homs anasema ameelezewa kuwa maiti zimefukuliwa kutoka vifusi vya majengo yaliyoangamizwa kwa mizinga Ijumaa usiku.
Serikali ya Syria imesema taarifa kuwa ilifanya uvamizi mkubwa mjini humo ni uzushi.
No comments:
Post a Comment