Kagame
Washirika wake Kagame wakimbilia uhamishoni
Rwanda imewasimamisha na kuwaweka katika kizuizi cha nyumbani maafisa wanne wa kijeshi wa ngazi za juu, kwa mujibu wa msemaji wa jeshi.
Maafisa hao wanachunguzwa kwa "matendo ya utovu wa nidhamu", kuhusiana na tuhuma za biashara ya madini kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Mmoja wa waliokamatwa ni mkuu wa ujasusi, ambaye alikuwa mshauri wa Rais Paul Kagame wa masuala ya usalama.
Rwanda imekuwa ikikanusha tuhuma kuwa inachukua madini ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Mwandishi wa BBC mjini Kigali, Prudent Nsengiyumva anasema hatua ya kukamatwa kwa maafisa hao imewashtua wengi nchini Rwanda hasa kutokana na vyeo vyao vikubwa.
Mwandishi wetu anasema kitendo cha maafisa hao kuwekwa katika kizuizi cha nyumbani kunaonesha kuwa hakuna aliye juu ya mkono wa sheria.
Waliokamatwa ni Luteni Jenerali Fred Ibingira, Mkuu wa itifaki wa jeshi la akiba; Jenerali Richard Rutatina, mkuu wa ujasusi wa jeshi; kamanda wa kikosi Jenerali Wilson Gumisiriza na Kanali Dan Munyuza, mkuu wa ujasusi wa nje ya nchi.
Rwanda imeivamia mara mbili Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ikisema inapambana na makundi ya waasi, lakini jeshi la nchi hiyo limekuwa likituhumiwa kwa kupora madini wakati wa mapigano, ambayo yalisababisha vifo vya watu milioni tano.
Katika miaka miwili iliyopita, washirika wa kijeshi ambao wapo karibu na Bw Kagame wamekimbilia uhamishoni, na wamekuwa wakishutumu mtindo wake wa utawala.