Dk. Mtasiwa asimamishwa uanachama kwa mwaka mmoja
JK atakiwa kuwatafutia kazi nyingine Nyoni, Dk. Mtasiwa.
|
CHAMA cha Madaktari Tanzania (MAT), kimeipa Serikali
masaa 72, iwe imekwisha kuwarejesha Hospitali ya Taifa Muhimbili, Madaktari wanafunzi ililiowafukuza na kuwaondolea udaktari
kutokana na kugoma wakati walipokuwa wakidai malipo yao. Tamko hilo,
limetolewa na Rais wa Chama hicho, Dk. Namala Mkopi, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari, Dar es Salaam leo. Aidha, Chama hicho kimtaka Rais Jakaya
Kikwete, kuwatafutia kazi nyingine, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, Blandina Nyoni pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Deo Mtasiwa kwa kosa la
kumshauri vibaya Waziri wa wizara hiyo, Dk. Hadji Mponda. Alisema Dk. Mponda
anasamehewa, kwani hajui alitendalo, ila wanamtaka kuwaomba radhi kwa kuwaita
madaktari wenzao kuwa si madaktari bali bado wangali wanafunzi. Rais huyo, alitangaza pia kuwa kimemfutia uanachama kwa muda wa mwaka mmoja, Mganga
Mkuu wa Serikali, Dk. Mtasiwa kwa kosa lake la kuusaliti udaktari kutokana na
kukiuka kiapo
cha chake kinachosema kuwa Madaktari wote ni ndugu na
nitawatendea haki, kama dada na kaka.
Alisema endapo Dk. Mtasiwa
ataendelea na tabia hiyo, ya kudharau taaluma ya udakatari, basi chama hicho, kitaamua
kumfukuza kabisa na kumuweka kwenye mtandao wa madaktari duniani, ili iwe
fundisho kwa madaktari wengine wenye tabia kama hiyo. Dk. Mkopi alisema kuwa
chama kimesikitishwa sana na kwamba hawaoni ni kwa nini Serikali imeamua
kuwaadhibu madaktari wenzao waliokuwa wakidai haki yao ya msingi na kuwaacha
kuwaadhibu watu waliosababisha ucheleweshwaji wa makusudi wa kutowalipa malipo
yao. Aliwataka viongozi kuacha tabia ya kutumia siasa kuingilia
masuala ya kitaaluma na kwamba wanavyofanya hivyo, wajue kwamba wanaowakomoa si
madaktari bali ni wagonjwa ambao ni ndugu na jamaa zetu sote.
Alisema kitendo cha kuwaondoa madakari zaidi ya 200,
tayari kimeanza kuleta athari kwa madakatari mabingwa waliokuwa wakisaidia kazi
na kwamba kibaya zaidi kusababisha wagonjwa wengi kufariki hospitalini
hapo. "Kitendo cha Serikali kuwaondoa madaktari wenzetu katika
Hospitali ya Muhimbili na kuamua kuwapangia Hospitali zingine si kizuri, kwani
baadhi ya hospitali walizohamishiwa hakuna nafasi wala mambo wanayotakiwa
kujifunza, hivyo mpaka sasa hakuna wanalolifanya," alisema. Chama hicho, kimeitisha
mkutano mkubwa wa madakari wote nchini, Jumatano ijayo utakaofanyika, Dar es
Salaam, ambao utazungumzia mambo kadhaa, likiwemo la madakatari hao.
Alitaja baadhi ya ajenda watakazozungumzia kwenye mkutano huo,
kuwa ni pamoja na hatima ya heshima ya Udaktari, Ulipaji posho kwa Madaktari, Mshahara
uendane na elimu, Majukumu na hadhi ya Udaktari, Madaktari kupewa nyumba, posho
ya mazingira magumu, posho ya mazingira hatarishi pamoja na uhamishaji ovyo wa
madaktari. |
No comments:
Post a Comment