TANGAZO


Monday, October 12, 2015

Balozi Seif Iddi awaonya wananchi wanaotiliana saini mikataba kienyeji

Kaimu Sheha wa Shehia ya Uroa Bwana  Bwana  Abass Sheha  akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Iddi, athari za Maji ya Bahari yaliyoathiri mwambao wa eneo la Kijiji cha Uroa, kutokana na ukuta uliojengwa na Hoteli ya Palumbo Kambakocho ambao waliulalamikia tokea mwanzoni mwa ujenzi wake. 
Baadhi ya sehemu za ukuta uliojengwa na Hoteli ya Palumba Kambakopcho ukionekana kubomoka kutokana na kasi kubwa ya mawimbi ya maji ya Bahari katika Kijiji cha Uroa. 
Sehemu ya Makaburi ya wanakijiji cha Uroa  ikukumbwa na mmong’onyoko wa ardhi unaosababishwa na kasi ya mawimbi la Bahari pembezoni mwa Hoteli ya Kitalii ya Palumbo Kambakocho. 
Mkurugenzi wa Hoteli ya Kitalii ya Palumbo Kambakocho Bwana Pablo Palumbo  wa kwanza kutoka Kulia akitoa ufafanuzi wa ujenzi wa ukuta wa kuzuia mawimbi ya Bahari pembezoni mwa Hoteli hiyo mbele ya Balozi Seif aliyepo mwazo kutoka kushoto ambao kwa sasa unaonekana kuleta athari ya Mmong’onyoko wa ardhi. Kulia ya Bwana Pablo ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Nd. Mustafa Aboud Jumbe. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
12/10/2015.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameonya kwamba tabia ya baadhi ya Wanavijiji wanaoishi katika ukanda wa maeneo ya uwekezaji wa sekta ya Utalii wa kutiliana saini mikataba katika mfumo wa kienyeji usiozingatia taratibu wa Kisheria umekuwa ukiibebesha mzigo mkubwa Serikali Kuu.

Amesema tabia hiyo hivi sasa imekuwa donda ndugu linaloonekana kuleta migogoro kati ya Wanavijiji na wawekezaji wa Hoteli na Nyumba za Wageni na hatimae  kuitia dosari Sekta ya Utalii iliyolengwa na Serikali kusaidia uchumi na kuongeza mapato ya Taifa.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo wakati alipofanya ziara ya ghafla ya kukagua athari ya ukuta uliojengwa pembezoni mwa Bahari ya Hindi katika fukwe ya Hoteli ya Kitalii ya Palumbo Kambakocho iliyopo katika Kjiji cha Uroa Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Ukuta huo uliojengwa kwa nia ya kuzuia kasi ya mawimbi ya Bahari hivi sasa umeanza kuleta athari kubwa ya Mmong’onyoko wa ardhi unaoelekea katika  Makaazi ya Wana Vijiji pamoja na  makaburi yaliyopo pembezoni mwa eneo hilo.

Balozi Seif alisema katika  hatua za kukabiliana na athari hiyo ameuagiza Uongozi wa Idara ya Mazingira Zanzibar kwa kushirikiana na Taasisi ya Uchunguzi wa Sayansi Baharini ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi pamoja na Serikali ya Mkoa wa Kusini Unguja kufanya utafiti wa kina kujua athari ya tatizo hilo.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa maamuzi mara baada ya kupokea Ripoti ya uchunguzi huo kama itaelekeza kubomolewa kwa ukuta huo au kupatikana suluhisho jengine la kuhami hali hiyo.

Aliiishauri Kamati hiyo aliyoiunda kuangalia upya mikataba  iliyotiwa saini Kati ya Muwekezaji na Wana Vijiji hao  itakayoainisha kwamba imezingatia taratibu zote zilizowekwa na Taasisi za uwekezaji miradi ya Utalii hapa Nchini.

“ Tumeanza kubaini matatizo yanayoibuliwa na baadhi ya Wanavijiji wa maeneo ya uwekezaji Utalii kutiliana saini Mikataba ya kienyeji isiyozingatia sheria na matokeo yake ni kuibebesha mzigo mkubwa Serikali Kuu “. Alisema Balozi Seif.

Mapema Kaimu Sheha wa Shehia ya Uroa Bwana  Abass Sheha  alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  kwamba Kamati ya Mazingira ya Kijiji cha Uroa ililalamikia ujenzi wa Ukuta huo tokea mwaka 2009 ambao walielewa kuwa utaleta athari ya Mmong’onyoko wa Ardhi.

Bwana Abass alisema  kasi ya maji ya Bahari katika eneo hilo iliyozuiwa na Ukuta huo kwa  hivi sasa imekuwa ya kutisha na kuleta hofu kwa wanakijiji hao umaliziaji wake unaelekea katika makaazi ya watu na eneo na makaburi.

Akitoa ufafanuzi wa mradi huo wa ujenzi wa ukuta wa kuzuia kasi ya mawimbi ya Bahari Mkurugenzi wa Hoteli ya Palumbo Kambakocho Bwana Pablo Palumbo alimueleza Balozi Seif kwamba ujenzi huo umefanywa baada ya makubaliano baina  ya Uongozi wa Hoteli hiyo pamoja na Wanavijiji wenyewe.

Bwana Pablo alisema  Uongozi wa Hoteli yake ulikuwa na nia safi ya kujenga Ukuta huo kutokana na ongezeko la kasi ya maji katika Bahari ya Hindi ndani ya kipindi cha miaka sita tokea  kuanza kwa Mradi wao.

No comments:

Post a Comment