TANGAZO


Wednesday, August 13, 2014

Serikali yatoa shilingi Bilioni 2.3 ya fidia kwa wakazi wa eneo la Mloganzila

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli

Na Rose Masaka, MAELEZO
Dar Es Salaam, 13.08.2014
SERIKALI imetoa kiasi cha Tsh. Bilioni 2.3 ya fidia kwa wakazi wa eneo la Mloganzila lililopo katika Kijiji cha Kwembe Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam, ambao waliathiriwa kutokana na ujenzi wa barabara kutoka Kibamba-Kisokwa hadi Barabara ya Morogoro.
Akizungumza jana wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya Barabara katika Manispaa hiyo, Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli alisema kwa mujibu wa vifungu vya sheria ya ardhi na barabara inasema iwapo barabara ikimfuata mtu eneo alipo lazima mtu huyo apewe fidia, na mtu atakayeifuata barabara hataweza kupewa fidia yoyote.
Kwa mujibu wa Dkt. Magufuli aliongeza kuwa  baadhi ya wananchi waliokuwa wakiidai serikali tayari wamelipwa kulingana na madai yao, na kuwa Serikali haipo kwa ajili ya kuonea watu na watu wasiionee serikali.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania Mhandisi Patrick Mfugale amesema kuwa katika awamu ya kwanza ya mradi huo Serikali imekusudia kujenga barabara hiyo kwa urefu wa kilometa  4, meta 7 za upana pamoja na kutenga eneo lenye ukubwa wa meta 4 kwa ajili ya waenda kwa miguu.
”Ujenzi ulianza mwaka 2013 mwezi wa 8, na kiasi cha Tsh. bilioni 6.4 zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha mradi huu na mradi huu wenye awamu mbili unatarajia kukamilika mwaka 2016 na pia kiasi cha Tsh bilioni 1.6 zinatumika katika ajili ya utanuzi wa barabara ya Kibamba yenye km 1.4” alisema Mfugale.
Katika hatua nyingine Waziri Magufuli pia alifanya ziara ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa mzani eneo la Vigwaza uliopo Wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu, ambapo mpaka kukamilika kwake unatarajia kuigharimu Serikali kiasi cha Tsh. bil 10.11.
Dkt. Magufuli aliwatahadhalisha madereva wa magari makubwa kuzingatia sheria za ujao wa mizigo usiozidi uzito wa tani 56, kwani kitendo hicho cha kinaifanya Serikali kutenga kiasi kikubwa cha fedha katika bajeti yake.
Katika Tanzania asilimia 25 ya magari yanachangia kuharibika kwa barabara hizi tunazojijenga, hivyo suala la kuzingatia sheria ya vipimo ni jambo muhimu kuzingatiwa na madereva wote” alisema Waziri Magufuli.

Dkt. Magufuli alisema mzani huo ni wa kisasa na Tanroad wanatakiwa kujifunza matumizi ya mtambo huo kwa umakini na pia wanatakiwa kutoa mikataba maalumu kwa watumishi wa mzani huo itakayoanisha hatua ya kinidhamu zitakazomkabili mfanyakazi huyo iwapo kutatokea uharibifu wa makusudi wa mitambo katika mzani huo.

No comments:

Post a Comment