Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage akisisitiza jambo mbele ya wadau na Wafanyabiashara katika kikao cha kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda uliofanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akiteta jambo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage katika kikao cha Wadau wa Sekta ya Dawa katika kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya Dawa na vifaa Tiba hapa nchini.
Wadau na Wafanyabiashara wa Sekta ya Dawa wakifuatilia kwa umakini taarifa kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu katika kikao cha kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya Dawa, tukio limefanyika mapema leo jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Mwijage wakiwa na Wadau wa Sekta ya Dawa katika kikao cha kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya Dawa na vifaa Tiba hapa nchini.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage (kushoto), akiteta jambo na Katibu wake Mkuu, Profesa Elisante Ole Gabriel, wakati wa mkutano huo.
SERIKALI yawataka Wadau wa Uwekezaji nchini kujitokeza kwa wingi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya dawa ili kusaidia kupunguza gharama kubwa za matumizi zinazotokana na kununua, kusafirisha na kuhifadhi dawa zinazotoka nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. UMMY MWALIMU katika kikao cha kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa nchini, kilichokutanisha wadau mbalimbali wa Uwekezaji katika Sekta ya Dawa, Vifaa na Vifaa tiba
Waziri Ummy alisema kuwa Serikali imekuwa ikitumia zaidi ya tirion moja kunuua dawa kutoka nje, hivyo kupitia uwekezaji wa viwanda vya dawa nchini itasaidia kupunguza adha hiyo nchini kwa kiwango kikubwa.
Nae Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji nchini Mhe. Charles Mwijage amewataka wote wenye nia ya kuwekeza katika Ujenzi wa viwanda vya dawa, vifaa na vifaa tiba lazima wahakikishe wanashirikiana na taasisi za Utafiti zilizopo nchini ili kuangalia mahitaji na aina dawa zinazohitajika.
Aidha, Mhe. Charles Mwijage amesema kuwa Uwekezaji na ujenzi wa Viwanda nchini utasaidia kupunguza tatizo la ajira na kuchochea Maendeleo ya ukuaji wa Uchumi katika ngazi ya watu na taifa kwa ujumla.
Chini ni hotuba kamili ya Waziri Ummy Mwalimu
................................................................................................
HOTUBA YA MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, KATIKA KIKAO CHA WADAU WA SEKTA YA DAWA KATIKA KUHAMASISHA UANZISHWAJI WA VIWANDA VYA DAWA NA VIFAA TIBA HAPA NCHINI TAREHE 04 APRILI, 2018 UKUMBI WA MIKUTANO WA MWALIMU JULIUS NYERERE DAR ES SALAAM
Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji
Wawakilishi wa Mashirika ya Serikali, Yasiyo ya Serikali na Sekta Binafsi,
Wakurugenzi,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii, kuwashukuru kwa kukubali mwaliko wetu katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa nchini.
Kama mtakumbuka Mhe. Rais John Pombe Joseph Magufuli amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuanzishwa kwa viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa nchini. Mara ya mwisho ilikuwa ni tarehe 26/03/2018 katika hotuba yake wakati akizindua magari 181 ya Bohari ya Dawa (MSD) alisikitishwa kwa jinsi nchi inavyotumia fedha nyingi kuagiza dawa na vifaa tiba kutoka nje ya nchi. Ambapo ni asilimia 6 tu ya mahitaji ya dawa yanapatikana nchini na asilimia 94 zinaagizwa kutoka nje.
Ndugu Wageni Waalikwa,
Katika kumuunga mkono Mhe. Rais nimewaiteni leo ili tuweze kujadili nini kifanyike il tuharakishe uzalishaji wa ndani wa dawa, vifaa na vifaa tiba wote tukafahamu fursa na taratibu zilizowekwa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mh. Rais John Pombe Joseph Magufuli katika kuanzisha viwanda nchini. Aidha, tungependa kusikia maoni na mapendekezo yenu kuhusu uwekezaji katika Sekta hii Muhimu.
Ndugu Wageni Waalikwa,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (WAMJW) imepewa jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa dawa zenye kukidhi ubora, ufanisi na usalama kwa Watanzania. Hata hivyo, uwezo wa kuzalisha dawa nchini ni mdogo. Tanzania ina jumla ya viwanda vya kutengeneza dawa kumi na tatu (13) ambapo uwezo wake wa kuzalisha ni chini ya asilimia 12 ya dawa zote zinazotumika nchini.
Ndugu Wageni Waalikwa
Zipo faida nyingi za kuwekeza katika Sekta ya Viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba hapa nchini ambapo MSD imepewa maelekezo ya kununua dawa moja kwa moja toka viwandani, hiyo ni fursa kubwa kwa uwekezaji wa viwanda vya dawa vya ndani. Aidha, Wizara yangu imeandaa orodha ya dawa (negative list) ambapo MSD itanunua dawa zilizopo katika orodha hiyo kutoka viwanda vya ndani tu. Orodha hiyo imeandaliwa kulingana na uwezo wa uzalishaji wa dawa nchini ambapo timu yangu ilifanya ufuatiliaji. Idadi ya dawa katika ‘negative list’ itaongezeka kadri viwanda vitakavyoimarisha uzalishaji.
Ndugu Wageni Waalikwa
Mawaziri wa Afya wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Africa (SADC) kwa kauli moja wamepitisha uteuzi wa nchi ya Tanzania kupitia Bohari ya Dawa (MSD) kuwa Mnunuzi Mkuu wa Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi vya Maabara kwa ajili ya nchi hizo kupitia mfumo wa Ununuzi Shirikishi (Pooled Procurement Services (SPPS).
Hatua ya uteuzi wa Tanzania kuwa mnunuzi mkuu wa Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi vya Maabara umetokana na juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa MSD ambapo sasa inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
Hivyo, Viwanda vyetu vya ndani vina fursa ya soko la uhakika la kuuza dawa kwa nchi za SADC. Nisisitize, kama nchi tutumie fursa hii vizuri kwa kuanzisha na kuimarisha viwanda vya dawa vilivyopo.
Mhe. Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wawakilishi wa Wizara mbalimbali na Taasisi za Serikali,
Kwa kutambua kwamba suala la viwanda vya dawa ni mtambuka tutaendelea kushirikiana na wadau wengine zikiwemo wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji; Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Wizara ya Nishati; Wizara ya Fedha na Mipango; Wizara ya Maji na Umwagiliaji; Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano; Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na Taasisi mbalimbali ili kuleta mabadiliko katika sekta hii ya uzalishaji wa Dawa na Vifaa Tiba.
Ndugu Wageni Waalikwa,
Mwisho naomba nitumie nafasi hii kumshukuru Mhe. Rais, Makamu wa Rais na Mhe. Waziri Mkuu kwa kuhimiza maendeleo katika Sekta ya Afya ikiwamo kuhimiza uwekezaji katika viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa nchini.
Ninaamini katika mkutano huu tutapata maoni na mapendekezo yatakayoleta mafanikio katika kukuza viwanda vya dawa nchini.
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA
No comments:
Post a Comment