TANGAZO


Thursday, April 5, 2018

UTAFITI WA MAPATO NA MATUMIZI YA KAYA BINAFSI TANZANIA BARA WA MWAKA 2017/18

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa

*Dkt. Chuwa awataka Wadadisi kutekeleza Majukumu yao kwa weledi na kuzingatia Kanuni na Taratibu za Utafiti

Na Mwandishi Wetu
WADADISI wa Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18 unaoendelea hivi sasa wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia mafunzo waliyopewa ili kuhakikisha ubora na usahihi wa taarifa wanazokusanya.

Wito huo umetolewa kwa nyakati tofauti na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa wakati wa ziara yake ya siku tatu katika Wilaya ya Karagwe mkoa Kagera kukagua maendeleo ya utafiti huo wilayani humo.

“Tumewapa mafunzo ya kutosha ya kuwawezesha kutekeleza kazi hii hivyo ni wajibu wenu kuifanya kwa umakini na weledi kwa kuwa mnao uwezo huo” amesema Dkt. Chuwa.

Dkt. Chuwa aliwahimiza wadadisi kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia kanuni na taratibu za utafiti mojawapo ni kwa mdadadisi kukusanya taarifa katika kaya kwa siku 14 bila kukosa.

“Kama zilivyo kazi nyingine, kazi ya kufanya utafiti ina changamoto zake hivo hatuna budi kukabiliana nazo… hakuna kurudi nyuma” alisema Dkt. Chuwa na kutolea mfano kuwa endapo kaya imechaguliwa mdadisi lazima kwa namna yeyote ile aifikie kaya hiyo hata kama ni kwa kutembea kwa masaa ili kupata taarifa zake.

Katika ziara hiyo ambayo aliambatana na Meneja wa Takwimu Mkoa wa Kagera Mr. Fabian Fundi, Mkurugenzi Mkuu huyo alitembelea maeneo ya utafiti ya Kigando katika kijiji cha Nyaishozi, Katwe katika kijiji cha Katwe na Nyakagoyagoye katika kijiji cha Rwemigogo.

Alimpongeza mdadisi Liliani Silvester aliyemkuta katika kijiji cha Nyaishozi akiendelea na kazi ya utafiti siku ya sikuu ya Pasaka na kumuelezea kuwa ni “mfano wa vijana wanaoipenda kazi yao.”

Akiwa katika ziara hiyo, Dkt. Chuwa aliwakumbusha wanakaya wa kaya zilizochaguliwa kushiriki katika ufatifi huo kwa kuwapa ushirikiano unaostahiki wadadasi kwa kutoa taarifa zilizo sahihi ambazo zitasaidia Serikali kupata takwimu bora ambazo zitatumika katika kupanga na kutathmini mipango ya maendeleo ya nchi. 

Hata hivyo, Mkurugenzo Mkuu huyo alibainisha kuwa kazi hiyo ya utafiti itafanikiwa zaidi ikiwa kutakuwa na ushirikiano wa karibu kati ya wadadisi, wanakaya na viongozi wa maeneo husika ya utafiti hivyo alitoa rai kwa wahusika wote kushirikiana ili wadadasi waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo na kufikia malengo ya utafiti huo.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa wadadisi kwa kutoa taarifa zilizo sahihi na za kweli wakati wote wa utafiti”alisisitiza Dkt. Chuwa na kuongeza kuwa yeyote anayekataa kushirikiana nao iwe kwa kukataa kabisa au kutoa taarifa zisizo sahihi anakuwa amefanya kosa la jinai.   

Alibanisha kuwa wapo baadhi ya wanakaya waliotakiwa kushirika katika utafiti huo walioomba kupewa ‘chochote’ kitendo ambacho si sahihi kwa kuwa utafiti huo una manufaa kwa wananchi wote hivyo kuwataka washirikiane na wadadisi.

No comments:

Post a Comment