Pages

Thursday, September 28, 2017

MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA WAZEE OKTOBA MOSI 2017 YATAKAYOFANYIKA DODOMA, TANZANIA.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na watoto Bw. Patrick Golwike (kushoto) akizungumza na waandishi wa Habari mbalimbali leo hii kuhusu Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee yanayofanyika Kitaifa katika Manispaa ya Dodoma, mkoani Dodoma.(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW)
Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii Bw. Rabikira Mushi (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee yanayofanyika Kitaifa katika Manispaa ya Dodoma, mkoani Dodoma.
Meneja wa Miradi kutoka Shirika la Kimataifa la kuhudumia Wazee Bw. Joseph Mbasha (Katikati) akitoa maelezo kuhusu mikakati inayofanywa na Serikali kwa ushirikiano na wadau katika kuboresha upatikanaji wa haki na huduma za afya kwa wazee nchini. 

MKUTANO KATI YA KATIBU MKUU WA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, BIBI SIHABA NKINGA NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA WAZEE ITAKAYOADHIMISHWA TAREHE 1 OKTOBA, 2017 KATIKA UWANJA WA NYERERE SQUARE MKOANI DODOMA.

Ndugu Wanahabari,
Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha sote kukutana mahali hapa. Pili, napenda kuwashukuru wote mliohudhuria kikao hiki, kwani kupitia kwenu kwa pamoja tutapata fursa ya kuongea wazee, jamii na watanzania wote kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee kwa mwaka 2017.

Tarehe 1 Oktoba ya kila mwaka Tanzania huungana na Nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Afrika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wazee.  Kwa mwaka huu, Serikali itaadhimisha Siku hii adhimu katika Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Mkoa wa Dodoma na Halmashauri zake zote pamoja na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali hapa nchini. 

Ndugu Wanahabari, 
Katika siku hii, Tanzania inaungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa kuwaenzi wazee kwa mujibu wa Azimio la Umoja wa Mataifa Na. 45/106 la mwaka 1990. Maadhimisho haya ya Siku ya Wazee Duniani ni moja kati ya jitihada za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) katika kutambua na  kuhamasisha jamii kuweza kulinda na kutetea haki za wazee duniani kote.  Umoja wa Mataifa umetenga siku hii kwa lengo la kutafakari hali ya maisha ya wazee na changamoto zinazowakabili wazee; na hivyo kuweka mipango thabiti ya kuboresha maisha yao na kuwafanya waishi maisha ya heshima, hadhi, na kuthaminiwa utu wao.  

Kila mwaka, Maadhimisho haya huwa yanabeba Kauli Mbiu yenye ujumbe mahususi. Kwa mwaka  2017  Kaulimbiu inasema  “Kuelekeza Uchumi wa Viwanda: Tuthamini Mchango, Uzoefu na Ushiriki wa Wazee kwa Maendeleo ya Taifa”. Kaulimbiu hii inahimiza Serikali, jamii, na wadau wote wa Maendeleo kuona umuhimu wa kuwashirikisha wazee ili kutumia uzoefu walio nao kwa  lengo la kufikia maelengo ya Taifa ya kujenga uchumi wa viwanda  utakaowezesha makundi yote ya jamii kuwa na maisha bora na yenye Staha; na hivyo kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.

Ndugu Wanahabari,
Maadhimisho haya kwa mwaka  2017 yanafanyika Kitaifa katika Manispaa ya Dodoma, mkoani Dodoma. Mgeni Rasmi anatarajiwa  kuwa  Mzee Ally Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili. 

Maadhimisho haya yatatanguliwa na shughuli mbalimbali kabla ya siku ya  kilele chake tarehe 01/10/2017. Tarehe 29/09/2017 (kesho) kutafanyika uzinduzi  wa Maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Wazee Kitaifa, yatakayofanyika katika Viwanja vya Nyerere Square. Katika  maonesho hayo wazee watapata huduma ya kupimwa afya zao, kupatiwa ushauri wa kitabibu; pamoja ufunguzi wa  maonesho ya kazi na huduma mbalimbali za Wazee. 

Wizara inaamini kuwa Wazee watajitokeza kwa wingi kupima afya zao na kupata ushauri wa kitaalam ili waishi maisha yenye afya na furaha. 

Tarehe 30/09/2017 kutakuwa na Kongamano la wazee litalofanyika katika  Shule ya Sekondari Dodoma kuanzia saa 4.00 asubuhi hadi saa  10.00 Alasiri. Kongamano litajadili masuala mbalimbali yanayogusa wazee  na mamna ya kukabiliana na changamoto hizo ikiwemo mwitikio wa Sera ya matibabu bure kwa wazee; tatizo la mauaji kwa wazee kwa imani za kishirikina; umuhimu wa mpango wa pesheni jamii kwa wazee wote na pendekezo la Sera ya Taifa ya Wazee kutungiwa sheria. 

Ndugu Wanahabari,
Siku ya kilele itatanguliwa na Maandamano  ya Wazee yatakayoanza katika viwanja  vya mashujaa wakipita Ofisi za Benki ya Posta  na barabara ya CDA hadi Uwanja wa Nyerere Square. Maandamano yatapokelewa na Mgeni Rasmi Mheshimiwa Mzee wetu Ally Hassan Mwinyi, Rais mtaafu wa awamu ya Pili. 

Hivyo, nitoa wito kwa wana Dodoma na Watanzania kwa ujumla  kufika Viwanja vya Nyerere Square kuanzia siku ya ufunguzi tarehe 29/9/2017 hadi siku ya kilele tarehe 1/10/2017 ili kupata huduma na nasaha mbalimbali kuhusu haki na ushauri nasaha kwa afya na ustawi wa wazee. 

Sanjari na huduma hizo kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mabalibali amabo watatumia fani yao kuelimisha na kuhamasisha jamii kuzingatia utekelezaji wa kaulimbiu ya siku ya wazee kwa mwaka 2017. 
Ndugu Wanahabari,

Napenda nitoe wito kwa jamii kuwa  hatuna budi kuenzi na kudumisha mila na desturi nzuri za kuwaenzi wazee kwa kutambua kuwa wazee ndiyo chanzo cha urithi wa historia ya nchi, washauri wa familia na jamii, ni watu wenye hekima, na walezi katika jamii. Hivyo jamii inaowajibu wa kuwaondolea vikwazo wazee katika kupata huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kuboresha afya, matunzo na ulinzi katika kipindi chote cha maisha yao. 
Mwisho.

Nawashukuru sana wanahabari wote kwa kushirikiana nasi katika maadhimisho haya na napenda kuwasihi muendelee kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza ufahamu wa wananchi na wadau kuhusu uimarishaji wa huduma ya matunzo, afya na matibabu kwa wazee wetu ikiwa ni pamoja na kuzuia unyanyapaa kwa kutumia uzoefu, stadi na maarifa yao katika kuendeleza Tanzania ya uchumi wa viwanda. 
Asanteni sana.


ANGALIA VIDEO HAPA

No comments:

Post a Comment