TANGAZO


Sunday, August 6, 2017

UFAFANUZI ULIOTOLEWA JANA NA CUF KUHUSU KILICHOTOKEA JUZI MAHAKAMANI WAKATI WA KUSIKILIZWA KWA SHAURI LA WABUNGE 8 WALIOFUKUZWA UANACHAMA NA PROF. LIPUMBA , MWENYEKITI ANAYETAMBULIWA NA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA, JAJI MUTUNGI


Naibu Mkurugenzi wa Habari wa Chama cha Wananchi (CUF), Mbarala Maharagande, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, wakati akifafanua kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mashauri ya chama hicho, yaliyoko mahakamani kwa uamuzi ikiwemo maombi ya zuio la hatua za bunge na tume ya uchaguzi kuwatangaza wabunge wapya wanane wa Viti Maalum waliochaguliwa na Profesa Lipumba, Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi. Kulia ni Mwenyekiti wa Matawi ya CUF jijini Dar es Salaam, Rashid Abdullah. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Joran Bashange akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, wakati akifafanua kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mashauri ya chama hicho, yaliyoko mahakamani kwa uamuzi, ikiwemo maombi ya zuio la hatua za Bunge na Tume ya Uchaguzi kuwatangaza wabunge wapya wanane wa Viti Maalum waliochaguliwa na Profesa Lipumba, Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi. Kulia ni  Naibu Mkurugenzi wa Habari wa Chama cha Wananchi (CUF), Mbarala Maharagande.
**************************************
MAELEZO YA UFAFANUZI WA MASUALA MBALIMBALI YANAYOENDELEA NDANI YA CUF
KWA WAANDISHI WA HABARI YALIYOTOLEWA LEO TAREHE 5 AGOSTI, 2017 KATIKA
UKUMBI WA OFISI YA WABUNGE WA CUF-MAGOMENI, DAR ES SALAAM:

1.      UTANGULIZI:

Ndugu Waandishi wa Habari,

Awali hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na afya njema kuweza kukutana. Tuwashukuru kwa kazi kubwa mnayoendelea
nayo ya kuuhabarisha umma wa watanzania ndani na nje ya mipaka ya Tanzania juu ya masuala mbalimbali yanayoendelea nchini hususani ndani ya Chama chetu cha CUF.


Kama tunavyofahamu kuwa Jana yamefanyika mazishi ya aliyekuwa Rais (Mwenyekiti wa Taifa) wa Chama TADEA ndugu John Lifa CHIPAKA. Kwa niaba ya Chama Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Taifa Mheshimiwa Julius MTATIRO ambaye yupo nchini Marekani kwa masomo ya Utawala
katika Chuo kikuu nchini humo ametuma salaamu za Rambirambi kwa  Chama cha TADEA, ndugu, jamaa na marafiki na wote walioguswa na msiba huu kwa namna moja au nyingine. “CUF imepokea kwa masikitiko makubwa
taarifa ya kifo cha John Chipaka  ambaye amekuwa ni mpambanaji wa kudai demokrasia na ni  muasisi wa mageuzi nchini kabla na baada ya Uhuru wa Tanganyika. Aliamini ktk utawala wa kidemokrasia kwa mfumo wa uwepo wa vyama vingi nchini, jambo lilompelekea kuonekana ni mtu mbaya
kwa watawala na kuwekwa kizuizini kwa kosa la uhaini kwa miaka zaidi ya kumi na mbili chini ya utawala wa awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere. 


Pamoja na misukosuko aliyopitia kipindi chote hicho hakuwahi kurudi nyuma na kubadilisha msimamo wake wa kudai uhuru wa fikra na hoja mbadala kwa maslahi ya Taifa. Mwaka 1992 John Chipaka pamoja na umri wake kuwa mkubwa naye alishiriki kuasisi tena mageuzi nchini kwa
kuanzisha moja ya chama cha siasa kinachojulikana kwa jina la TADEA na yeye kuwa Rais wa chama hicho mpaka alipofariki. Hakika marehemu Chipaka katika msimamo huo ameacha funzo kubwa kwa vijana na wazee wenzake kuwa na moyo wa mageuzi, na ujasiri wa kupambana kudai haki na uhuru”. Ameeleza Mheshimiwa Mtatiro.   


Mwenyezi Mungu amsamehe
mapungufu yake na amuweke mahala pema peponi. Amiin!!


2.      KUHUSU KESI/MASHAURI YA CUF YALIYOPO MAHAKAMANI:
Kama tunavyofahamu mwaka jana mwezi wa Septemba 24, 2016 baada ya Lipumba kufanya uvamizi wa ofisi za chama pale Buguruni kinyume na sheria na taratibu baada ya Kujiuzulu kwa hiari yake na kuiacha ofisi hiyo takribani kwa kipindi cha mwaka mzima. Chama cha CUF kupitia
maamuzi ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa iliagiza Kamati ya Utendaji ya Taifa kusimamia suala hilo kwa kulifikisha mbele ya vyombo vya sheria-Mahakama ili kulipatia ufumbuzi. 


Ni kwa msingi huo kuliendelea kujitokeza kwa ukiukwaji wa mambo mbalimbali na athari za uvamizi huo na mpaka sasa kuna Mashauri 6 ya Msingi yaliyopo Mahakamani Pamoja na mashauri madogo mengine ambayo sijayataja katika
orodha hii kama ifuatavyo;

a)      Kuna shauri la msingi (Civil Application/Cause) namba 23/2016 hili linahusu kuhoji uhalali wa maamuzi ya Msajiri wa Vyama vya siasa nchini Jaji Franscis Mutungi kumrejesha Lipumba katika Uenyekiti kinyume na Katiba ya CUF na maamuzi ya Mkutano Mkuu wa Taifa. Lipo mbele ya Jaji Kihiyo na limepangwa kutajwa Tarehe 7/9/2017.


b)      Kuna shauri la msingi la madai (Civil Application no. 21/2017) kuhusu wizi wa Ruzuku na shauri dogo (Miscellaneous Civil Application No.28/2017) hili linahusu kuhusu kuweka Zuio [Injuction] kutolewa Ruzuku ya Chama kutokana na wizi wa shilingi 369 zilizoibwa na Lipumba
na kundi lake wakishirikiana na Msajili Jaji FRANCIS Mutungi. 
Limepangwa kutolewa maamuzi ya Pingamizi Tarehe 11 Agosti, 2017 Lipo Mbele ya Mheshimiwa Jaji Wilfred Ndyansobera.

c)       Kuna Shauri La Madai Namba 13/2017 Lililofunguliwa Na Ally Salehe dhidi ya RITA, Lipumba na wenzake kuhusu uhalali wa Bodi FEKI ya Wadhamini ya CUF iliyosajiliwa na RITA. Na shauri dogo namba 51/2017 linaloomba kuwepo kwa zuio (Injuction) ya kuizuia bodi hiyo kufanya kazi mpaka shauri la msingi  litakaposikilizwa na kufanyiwa maamuzi.
Limepangwa kutajwa na au kusikilizwa tarehe 11 Agosti, 2017. Nalo lipo mbele ya Mheshimiwa Jaji Ndyansobera.


d)      Kuna shauri la Jinai namba 50/2017 kuhusu Lipumba na wenzake, Emmy Hudson -RITA, Jaji FRANCIS Mutungi kughushi nyaraka na kutaka kuingilia mwenendo wa mashauri yaliyopo Mahakama (CONTEMPT OF COURT
PROCEEDINGS)


e)      Kuna shauri la msingi (Election Petition) namba 1/2017
linalohusiana na uchaguzi wa wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki katika Mahakama kuu ya Dodoma kati ya Twaha Taslima, Abdallah Mtolea, Katani Ahmed katani dhidi ya Bunge kwa kukiuka utaratibu na kanuni za uchaguzi huo uliompa Mohamed Habibu Mnyaa uwakilishi wa CUF hali si
mwanachama.


f)      SHAURI LA MSINGI (CIVIL CASE NO.143/2017) Juu ya Wabunge 8 wa CUF na Madiwani 2 kupinga kuvuliwa uanachama na Lipumba lakini pia kuna maombi madogo (Miscelleneous Civil Application No. 447/2017) ambayo
inahusiana na kuomba Zuio la muda (Temporary Injuction Order and To maintain Status Quo)

UFAFANUZI WA KILICHOTOKEA NA MAAMUZI YA MAHAKAMA KUU:


Shauri la msingi (CIVIL CASE NO. 143/2017) Limepangwa
kusikilizwa/kutajwa Tarehe 31/8/2017 shauri hili lililofunguliwa na wabunge wetu 8 na Maadiwani wawili wa manispaa za ubungo na Temeke ambao ni

1.      MIZA BAKARI HAJI
2.      SAVERINA SILVANUS MWIJAGE [MBUNGE]
3.      SALMA MOHAMED MWASA [MBUNGE]
4.      RAISA ABDALLAH MUSSA [MBUNGE]
5.      RIZIKI SHAHRI NG’WARI [MBUNGE]
6.      HADIJA SALUM ALLY AL QASSIM [MBUNGE]
7.      HALIMA ALI MOHAMED [MBUNGE]
8.      SAUMU HERI SAKALA [MBUNGE]
9.      ELIZABETH ALATANGA MAGWAJA- DIWANI VITI MAALUMU MANISPAA YA TEMEKE.
10.     LAYLA HUSSEIN MADIBI- DIWANI VITI MAALUM-MANISPAA YA
UBUNGO.

DHIDI YA

1)      BODI YA WADHAMINI -CUF,
2)      MWENYEKITI WA CHAMA TAIFA,
3)      KAIMU KATIBU MKUU-CUF,
4)      MKURUGENZI TUME-NEC,
5)      KATIBU WA BUNGE,
6)      MKURUGENZI MANISPAA- TEMEKE
7)      MKURUGENZI MANISPAA -UBUNGO
8)      RUKIA AHMED KASSIM,
9)      SHAMALA AZIZ MTAMBA,
10)     KIZA HUSSEIN MAYEYE,
11)     ZAINAB MNDOLWA AMIR,
12)     HINDU HAMIS MWENDA,
13)     SONIA JUMAA MAGOGO,
14)     ALFREDINA APOLINARY KAHIGI,
15)     NURU AWADH BAFADHILI

Wabunge na Madiwani Wetu wanadai haki ya uanachama wao kwa kuhoji mchakato uliotumika kufikia maamuzi hayo ambao haukufuata katiba ya CUF na huku kukiwa na mashauri ya msingi yanayoendelea mahakamani
yanayohoji uhalali wa Uongozi juu ya ‘Mgogoro uliopandikizwa na Vyombo vya dola kwa kumtumia Msajili wa Vyama vya siasa unaoendelea. Wanahoji juu ya uhalali wa vyombo vilivyochukua hatua hizo za nidhamu dhidi yao
kama zimefuata taratibu ikiwa ni pamoja na kuwapatia taarifa za tuhuma zao kwa maandishi ili waweze kujiandaa kwa utetezi, siku na tarehe ya kikao hicho ukizingatia kuwa si wote wanaoishi hapa Dar es Salaam, uharaka wa Bunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuchukua hatua bila kujiridhisha na alau kiubinaadamu Bunge ikiwa ni wajumbe wake
kuwauliza na kujua kutoka kwako hicho kilichojitokeza, kwa ujumla hawakupewa nafasi ya kusikilizwa na kujitetea, maamuzi hayakuzingatia haki za kikatiba ikiwemo kukata Rufaa ndani ya siku 14 Ibara ya 108(5) ya katiba ya CUF, Wabunge wamekatia Rufaa maamuzi hayo na kumuandikia
barua na kukiomba Chama kupitia Katibu Mkuu kiweze kuitisha Mkutano Mkuu wa Taifa ili kufikisha rufaa yao.


Mkutano Mkuu ndio wenye mamlaka na maamuzi ya mwisho juu ya masuala yote ndani ya Chama. Hilo lilifanywa na Lipumba na wenzake pale Baraza Kuu la uongozi taifa
lilipowachukulia hatua za kinidhamu kwa kuwasimamisha uanachama Tarehe 28 Agosti, 2017.


Hayana mengine ndiyo yanayohojiwa Mahakamani katika shauri hili la msingi.

3.      KUHUSU SHAURI DOGO LA MADAI [MISCELLENEOUS CIVIL CASE NO. 447/2017]
WABUNGE [8] NA MADIWANI [2] WA CUF DHIDI YA walalamikiwa walewale 15 tajwa hapo juu.

Maombi hayo yanahusu kuiomba Mahakama Kuu itoe zuio la muda [Temporary Injuction Order and to maintain Status Quo- HII MAANA YAKE NI KUSIMAMISHA MAAMUZI YA BUNGE NA TUME NA KUWAREJESHA WABUNGE WALIODAIWA KUVULIWA UANACHAMA WAENDELEE NA SHUGHULI ZA BUNGE NA KUWA WAKILISHI
HALALI] katika kipindi hiki mpaka hapo shauri la msingi
litakapoamuriwa. Kabla maombi hayo hayajasikilizwa Walalamikiwa (Respondent's No.1,2,3,4,5,8-15) waliweka Pingamizi la Awali (Preliminary Objections) juu ya shauri hilo kwa madai ya kukosa sifa za kisheria (incompetence enacted provisions of law) na hoja hizo 4 za pingamizi zilizosikilizwa takribani kwa masaa 4 Tarehe hiyo 2/8/2017 pale shauri hilo lilipoitwa kwa kusikilizwa na baadae kupangwa kutolewa maamuzi ya Pingamizi hilo jana Tarehe 4/8/2017.

4.      MAAMUZI JUU YA PINAMIZI LA AWALI YALIYOTOLEWA NA MAHAKAMA KUU;

Katika kupitia hoja zilizowasiilishwa Mahakamani hapo katika pingamizi hilo la awali (Preliminary Objection) lililowekwa na walalamikiwa Mahakama Kuu imekubaliana na hoja za waweka pingamizi kuwa kifungu cha sheria kilichotumika kufungulia shauri hilo mahakamani sio sahihi na hivyo kuliondoa shauri hilo kwa maana ya ‘STRUCK OUT”

Unapozungumzia pingamizi unazungumzia hoja za kisheria pekee (pure points of law) kati ya hoja 4 zilizowasilishwa hoja 3 zimekataliwa na moja kukubaliwa iliyohusiana na matumizi ya sheria za uingereza (Common Law)  section 2(3) ya JALA kifungu ambacho kwa mtazamo/maoni ya Jaji hakiipi mamlaka ya kisheria Mahakama kusikiliza maombi hayo.
Nini maana ya maamuzi hayo na tafsiri ya kisheria juu ya neno “Struck out na Dismissal”

LEGAL DEFINITION :

"Difference between DISMISSAL and STRIKE OUT. When a case is dismissed, there is no right to reinstate it in the future. This is the legal way to say the case is closed and it cannot be re-opened. When a case is struck out, it may be re-opened.

TAFSIRI YA KISHERIA:

“Tofauti kati ya kufuta na kuondoa (shauri) ni kwamba kesi ikifutwa, hakutakuwa na haki ya kuirejesha tena (kurudisha/kuifungua upya) hapo baadae. Hii ni njia ya kisheria kusema kuwa kesi imefikia mwisho na huwezi kuifungua upya. Pale kesi inapoondoshwa, inaweza kufunguliwa upya.”

Pingamizi juu ya maombi ya Shauri namba 447/2017 yameondolewa mbele ya Mahakama na wala hakuna hiko kitu kinachoitwa ‘kesi imefutwa, au kutupiliwa mbali au mahakama imeruhusu Wabunge wapya kuapishwa, KWA
HAKIKA HAKUNA USHINDI WA MAAMUZI YALIYOTOLEWA’ kama inavyoripotiwa. Shauri limeondolewa kwa kumaanisha kama vile hakukuwa na kitu kilichopaswa kujadiliwa na Mahakama juu ya maombi hayo. Pingamizi la
awali [Preliminary Objection] na Maombi ya Zuio [injuction/Stop Order] ni vitu viwili tofauti kisheria. Wabunge wa CUF wameomba Zuio. Lipumba na wenzake wameweka Pingamizi. Huo ndio usahihi wa maelezo ya nini
kilichojitokeza katika maamuzi ya Mahakama Kuu jana.

5.      MATOKEO YA MAAMUZI YA MAHAKAMA KUU;

Maamuzi hayo yametupa fursa ya kuandaa vizuri zaidi nyaraka hizo na tayari tumepata faida ya kujua hoja wanazosimamia walalamikiwa (Respondents). Wabunge wetu wameweza ndani ya masaa 2 baada ya maamuzi
tayari nyaraka zilitayarishwa, kusainiwa pamoja na marekebisho yote ya msingi na ya lazima yaliyopaswa kuingizwa ikiwemo kuwajumuisha katika shauri hilo Wakurugenzi wa Manispaa za Ubungo na Temeke ambao
wanahusika kutokana na Madiwani waliopo katika halmashauri zao kuathiriwa na maamuzi ya Lipumba na genge lake. Ni matarajio yetu kuwa Jumatatu ya tarehe 7/8/2017 tutapata mrejesho wa kujua Mahakama Kuu
imelipanga lini kulisikiza shauri hilo kutokana na kuingizwa kwa hati ya dharura/haraka (Under Certificate of Urgency).

6.      WITO KWA WAAANDISHI WA HABARI, WANACHAMA NA WATANZANIA KWA UJUMLA:
KESI ni MCHAKATO siyo TUKIO. Utaratibu wa kisheria una njia na namna kadhaa za kupitia ili kuifikia haki inayopiganiwa. Tunawaomba waandishi wa habari kuripoti habari za kimahakama kwa usahihi na kutumia weledi ili kuepusha taharuki na kuwachanganya wananchi na
wadau mbalimbali wa habari. 


Tusitoe taarifa kwa kutumia ‘mizuka’ mkanganyiko uliojitokeza jana na leo katika vyombo vya habari
haukujenga weledi na afya njema kwa kuwahabarisha wananchi ndivyo sivyo.

Tunatoa wito kwa wanachama wa CUF, Wapenzi na Watanzania kwa ujumla kupuuza habari za upotoshaji na propaganda zinazoendelea kufanyika kupitia mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari. Si shauri
la msingi wala maombi ya zuio lililosikilizwa na Mahakama Kuu na kuyatolea maamuzi. Kilichotolewa maamuzi ni Pingamizi juu ya hoja za za kisheria pekee ambazo zimesharekebishwa na kurejesha upya shauri hilo mahakamani.

Tuendelee kuwa watulivu na kwamba viongozi wenu ngazi ya Taifa wapo makini kulisimamia suala hili na kuhakikisha kuwa haki inapatikana. Tuna imani kubwa na Mahakama kuwa ni chombo cha kusimamia haki si Chombo cha kuchezewa. Maamuzi ya Mahakama Kuu juu ya pingamizi tumeyapokea, ni sahihi kwa mujibu maoni ya Jaji kwa mujibu wa sheria
na wala SI HUJUMA DHIDI YA HAKI kama inavyotaka kuaminishwa na baadhi ya wasiojua taratibu na misingi ya kisheria. Hakuna maamuzi yoyote mpaka sasa yaliyotolewa na Mahakama Kuu katika kadhia hii inayoendelea zaidi ya Kuzuia Ruzuku isitolewe kwa Lipumba na genge lake na hili la kuondoa maombi madogo yaliyowasilishwa.

Tutaendelea kukilinda na kukitetea Chama chetu cha CUF kwa nguvu zetu zote na kukiimarisha zaidi ilii kiendelee kutekeleza wajibu wake katika uendeshaji wa siasa za kistaarabu, na kwa njia za amani na zinazofuata Katiba ya CUF, Katiba ya JAMHURI  ya Muungano wa Tanzania
na Sheria nyingine za nchi yetu.

CUF NI TAASISI IMARA, YENYE VIONGOZI MAKINI.

HAKI SAWA KWA WOTE

MBARALA MAHARAGANDE
K/ NAIBU MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI, NA MAHUSIANO NA UMMA-CUF TAIFA.

No comments:

Post a Comment