Naibu Katibu Mkuu CUF Zanzibar, Nassor Mazrui
TAARIFA YA CHAMA CHA WANANCHI (CUF) ILIYOTOLEWA NA NAIBU KATIBU MKUU (ZANZIBAR), MHE. NASSOR AHMED MAZRUI, KUHUSIANA NA KADHIA YA ZANZIBAR KUONDOLEWA UANACHAMA WA SHIRIKISHO LA SOKA AFRIKA (CAF) MIEZI MINNE TU BAADA YA KUKUBALIWA KUJIUNGA
Waheshimiwa Wanahabari,
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima na asubuhi ya leo tukaweza kukutana hapa.
Pili, napenda kukukaribisheni nyote katika mkutano huu makhsusi kwa ajili yenu. Sisi katika CUF tunathamini sana nafasi yenu katika wajibu wa kutuunganisha na umma. Taifa imara ni lile ambalo wananchi wake wanaarifiwa juu ya kila kinachowahusu kadiri inavyowezekana na hiyo ina maana kuwepo uhuru wa kutoa na kupokea habari.
Ni furaha yetu kuwa kila mara mko nasi CUF na kwa pamoja tunashirikiana katika wajibu wetu wa kujenga nchi yetu ambayo imekuwa ikipitita katika kipindi kigumu.
Waandishi wa habari mna dhima kubwa ya kuisadia nchi hii kwa njia ya kuongoza, kushauri, kukosoa na kuwezesha umma kupata habari ili uweze kufanya maamuzi sahihi. Kazi mnayoifanya ni adhimu na muhimu na huwa haikosi misukosuko katika kuitekeleza. Nawahakikishieni kwamba CUF inakuungeni mkono na iko pamoja nanyi.
Waheshimiwa Wanahabari,
Madhumuni ya mkutano wetu huu ni kuzungumzia suala la Zanzibar kutolewa katika Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) ikiwa ni miezi mine tu baada ya kupata uanachama huo tukiwa wanachama nambari 55, jambo ambalo lilikonga nyoyo za Wazanzibari wote, hususan vijana.
Kupatikana kwa uanachama huo, ambapo baadhi yetu tuliuona wa jasho na damu, ilikuwa ni alama kubwa ya kutambua kilio cha Zanzibar cha muda mrefu cha kutaka siyo tu kutambuliwa kimataifa bali angalau kuweza kushiriki katika harakati mbali mbali za kikanda katika sekta ya michezo.
Wengi tuliamini kuwa baada ya uanachama kamili wa CAF, kutokana na kuwa Mwanachama Shirikishi kwa miaka 7, tuliona kuwa hiyo ndiyo njia sasa ya kuelekea uanachama wa Shirikisho la Kimataifa la Soka Duniani (FIFA).
Kuingia FIFA maana yake ni kutambuliwa kidunia na kwa hivyo kuweza kushiriki katika michuano mikubwa ya Kombe la Dunia, mbali ya fursa mbali mbali zinazotolewa na FIFA, sawa ni zile ambazo tungezipata ndani ya Bara la Afrika kwa kubakia kuwa mwanachama wa CAF.
Hii ina maana kuingia kwa Zanzibar katika CAF au FIFA ni suala muhimu, la lazima na la msingi kabisa kwa sababu za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Zanzibar ina haki kabisa ya kujipigania, narudia tena, Zanzibar ina haki kabisa kujipigania, kuingia katika vyombo hivyo vikuu vya michezo Afrika na Ulimwenguni.
Ila pia kupatikana kwa uanachama huo kulikuwa na maana ya kuamini kuwa haki ya Zanzibar kujisimamia wenyewe imepatiwa suluhu na uanachama huo ungerudi katika muundo wa Muungano ambapo ilikuwa ndio chachu na mlango wa kuelekea kwenye Mamlaka Kamili ya Zanzibar.
Ni lazima tuelewe kwamba kulinda, kuhifadhi na kudumisha mamlaka ya Zanzibar ni wajibu wa kikatiba wa kila Mzanzibari. Ibara ya 23 (4) ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inafafanua wajibu huo kama ifuatavyo:
“23.(4) Kila Mzanzibari ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi, na kudumisha uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa Zanzibar.”
Hivyo basi, tunapolizingumzia suala hili, tunatekeleza wajibu wetu wa kikatiba wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha mamlaka ya Zanzibar na tunatoa wito kwa Wazanzibari wote kuungana katika kuutekeleza wajibu wao huu wa kikatiba.
Lakini ifahamike kwamba tunafanya hivi tukiwa na wajibu wa ziada pia kwani CUF ndiyo tuliyopewa ridhaa na Wazanzibari tarehe 25 Oktoba, 2015 kuwa wasimamizi wa uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa Zanzibar.
Wananchi wa Zanzibar walimchagua kwa kumpa ushindi mkubwa mgombea Urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye walimpa jumla ya kura 207,847 dhidi ya mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyeambulia kura 182,011 ikiwa ni tofauti ya kura 25,836. Ridhaa ya Wazanzibari kwa CUF pia ilielekezwa kwenye ushindi mkubwa wa nafasi za Uwakilishi ambapo iliongeza majimbo yake kisiwani Unguja kutoka manne (4) hadi tisa (9) mbali ya kuendelea kubakisha majimbo yake yote 18 kisiwani Pemba, tena hayo yakifanyika baada ya uvurugaji mkubwa wa mipaka ya majimbo ya uchaguzi ambayo CCM, kwa ujuaji wa mtu anayeitwa Haji Omar Kheri, walidhani ingewasaidia.
Kwa hivyo, kulisemea hili ni wajibu wetu wa kikatiba lakini pia unatokana na kuwa sisi ndiyo tuliochaguliwa na Wazanzibari kuwasimamia mamlaka yao. Hata kama watawala waliamua kufuta matokeo hayo, hilo halifuti ukweli ambao unajulikana dunia nzima.
Waheshimiwa Wanahabari,
Baada ya utangulizi huo, ni vyema tuelewe kuwa soka au michezo kwa ujumla si bururdani na uchumi tu bali ni siasa, mahusiano ya kimataifa na alama ya utaifa kwa nchi yoyote ile, Zanzibar ikiwemo. Kuwemo katika CAF, FIFA au Shirikisho la Kimataifa la Olimpiki (IOC) ni sehemu ya alama ya fakhari na utambulisho wa nchi yoyote ile.
Zanzibar ilikoseshwa fakhari na utambulisho huo kwa muda mrefu sana kupitia muundo wa kikandamizaji wa Muungano uliopo. Fakhari na utambulisho huo katika michezo tulianza kuupata miezi minne iliopita, kabla ya kukatishwa na Kikao cha Mkutano Mkuu (General Assembly) cha CAF kilichotuvua uanachama huo, ambapo kusema kweli imekuwa ni sawa na kuvuliwa nguo.
Kwa sababu hiyo basi, hicho si kitendo kinachostahamilika hata kidogo. Mbali ya kukilaani, bali pia ni haki yetu kukipinga. Na zaidi ya kukilaani na kukipinga, CUF inaona tuna wajibu wa kudai kupata maelezo ya kutosha, kutoa taarifa/taaluma ya kutosha kwa CAF na kukikatia rufani kadiri ya Kanuni zinazohusika zilivyo ili tukisemee, tukisimamie na tukitafutie suluhu.
Tulitegemea wale waliopora mamlaka ya kuongoza za Zanzibar na walinzi wao walioko upande wa pili wa Muungano wangelilisemea jambo hili kwa nguvu inayopaswa kusemewa, lakini tumeshindwa kuona hatua thabiti za kuukabili msiba huo kwa Zanzibar na pia tumeshindwa kusikia sauti ya kunguruma kuzungumzia tukio hilo, ambalo limeturudisha nyuma mno baada ya kuonekana tumepiga hatua moja kubwa na ya maana kwa nchi yetu. Vibaraka wanaogopa! WAMEUFYATA!
Waheshimiwa Wanahabari,
Tunajua suala la kukubaliwa na kukataliwa uanachama wa Zanzibar katika CAF ni la kisheria zaidi lakini tunaamini kuwa tuna nafasi kubwa ya kuielezea CAF kuwa haiko sahihi katika uamuzi wake kwa hoja ambazo imezitoa. Tunaamini kikubwa CAF ilichokifanyia maamuzi ni kukosekana kipengele cha kuchukua hatua ndani ya mipaka ya sheria kwa kesi kama ya Zanzibar ambayo haifanani na nyengine yoyote hapa Afrika kwa waliokubaliwa wanachama wa CAF.
Hapa kwetu Afrika hakujatokea mambo ambayo huko kwa wenzetu yametokea na bado nchi zimeweza kuwa wanachama wa mashirika kama UEFA na CONCAF na mengineyo, kwa nchi ambazo katika hali zake huku Afrika zingeonekana hazifai kuwa mwanachama kama nchi au taifa.
Mfano wa nchi za England, Scotland, Wales na Ireland ya Kaskazini tukiuwacha mbali kuna mifano mingi ya nchi ambazo hazina utawala kamilifu, hazina ligi zake wenyewe, hazina mfumo kamili wa soka na wala si wanachama wa Umoja wa Mataifa, na bado ni wanachama wa FIFA. Tunaambiwa England, Scotland, Wales na Ireland ya Kaskazini wamepata bahati hiyo kwa sababu kuingizwa kwao kulitokana na sababu maalum ya kuwa walikuwa ni sehemu ya nchi zilokuwa katika Bodi ilotunga sheria za FIFA.
Ila nchi hizo kwa pamoja katika michuano kama Olimpiki huingia kama nchi moja chini ya bendera kubwa ya United Kingdom na sio nchi hizo moja moja na peke yao au peke yake kila moja.
Na hiyo ingekuwa kwa Tanzania kwamba tunaingia katika CAF kila upande peke yake, katika FIFA kila upande peke yake lakini tunaingia katika Olimpiki kama taifa moja. Wanasheria wanasema angalau kuna hukumu elekezi katika hilo (precedent).
Waheshimiwa Wanahabari,
CAF imetoa hoja kuu mbili zilizopelekea kuinyang’anya Zanzibar kiti chake katika chombo hicho. Moja, ni kwamba haiwezi kutoa nafasi mbili kwa nchi moja kuwakilishwa na pili, ni kuwa kigezo cha uanachama ni kuwa nchi hiyo ni mwanachama wa UN. Hoja zote ni dhaifu.
Inavyoelekea CAF hawakutaka kujitaabisha kutizama hali ya ulimwengu ilivyo katika suala hili, au sisi hatukutumia nafasi yetu vya kutosha kuwaelewesha kuwa katika hili wamejipotosha, tena wamepotoka sana. Zinaweza kuwepo hoja zifuatazo kupingana na mtizamo wa CAF:
1. Kama tulivyosema hapo juu kuwa England, Scoland, Wales na Ireland ya Kaskazini ni wanachama wa FIFA kwa sababu ya historia, lakini nchi hizo katika katika Umoja wa Mataifa zinaingia kama United Kingdom.
2. Kuwa mwanachama wa UN hakumaanishi nchi inaingia FIFA moja kwa moja na ipo mifano kama vile nchi ya Nauru mwanachama nambari 187 wa UN si mwanachama wa FIFA, halikadhalika Tuvalu mwanachama nambari 189 wa UN lakini si mwanachama wa FIFA.
3. Halidhalika kuna Monaco ambayo imo ndani ya Ufaransa na inatambuliwa na UN lakini si mwanachama wa FIFA.
4. Kama kipimo ni nchi moja, chama kimoja ndani ya FIFA na hicho ni kigezo cha CAF basi Macau, Hong Kong, Taiwan zote ziko chini ya Mamlaka Kuu moja ya China kwenye UN lakini kila mmoja wao ana kiti katika FIFA
5. Visiwa vya Neue na Cook viko chini ya New Zealand na si wanachama wa UN lakini vyote vinapeperusha bendera zao katika uanachama wa FIFA.
6. Pia kuna Visiwa vya British Virgin na US Virgin, ambavyo viko chini ya Uingereza na Marekani mtawalia na hata hawana pasi zao wenyewe za kusafiria na bado wamekubaliwa kuwa ni wanachama wa FIFA.
Waheshimiwa Wanahabari,
Hoja ya uanachama wa UN ni dhaifu kiasi ambacho orodha ya UN ya nchi wanachama ni fupi lakini ile ya FIFA ni refu zaidi na ushahidi kama tulivyoonyesha. Wanachama wengine wa FIFA ambao si wanachama wa UN ni kama ifuatavyo:
Samoa, Anguilla, Aruba, Bermuda, British Virgin Islands, Cayman Islands, Chinese Taipei, Cook Islands, Curacao, Faroe Islands, Gibraltar, Guam, Hong Kong, Macau, Montserrat, New Caledonia, Puerto Rico, Tahiti, Turks and Caicos Islands, na U.S. Virgin Islands.
Ukweli ni kuwa baadhi ya nchi hizo wanachama wa FIFA bila ya kuwa wanachama wa UN hazina uwezo wa hata kuwa na ligi za soka zao wenyewe na kwa hivyo wapo wapo tu, au wengine hucheza katika ligi za nchi nyengine.
Kuna nchi kubwa kama ya Canada, basi wamekubali tu kuwa ndio mfumo wao, na wao hucheza ligi yao ndani ya Marekani katika soka na pia katika hoki ya barafu, kwa maana kuwa hata kuwa mwanachama wa FIFA unaweza kuwa pia na utaratibu wako mwenyewe wa kisoka, alimradi tu Sheria na Kanuni za FIFA zinahusika.
Waheshimiwa Wanahabari,
Hoja kubwa ya pili ya CAF kuikatalia Zanzibar uanachama ni kuwa na vyama viwili au wawakilishi wawili kutoka nchi moja kuingia kwenye taasisi hiyo, ambayo pia si jambo lenye mashiko.
Tumeonyesha hapo juu mbali ya United Kingdom ambayo ni kesi maalum, lakini New Zealand ina matawi yake ndani ya FIFA; China ina matawi yake; Marekani na Uingereza pia kwa maana ya British Virgin, US Virgin, Puerto Rico na Gibraltar.
Haikuwa sahihi kabisa kwa CAF kuamua tu, kwa kutizama hali ya juu juu kuwa kuingia kwa Zanzibar Football Association (ZFA) kutaifanya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (Tanzania) iwakilishwe na vyama viwili na kwa hivyo si stahiki, ilhali CAF ilikuwa iende ndani zaidi ya kujua kuwa kila moja kinawakilisha maslahi tofauti kabisa.
ZFA ni kwa maslahi ya Zanzibar na TFF ni kwa maslahi ya Tanganyika.
Kwa hivyo, CAF ingepaswa kujua kuwa mbali ya kuwa tuna nchi mbili ndani ya Jamhuri ya Muungano, lakini pia tuna muundo ambao Afrika nzima haupo ambapo ndani ya Muungano huu, kila nchi kati ya nchi mbili zinazouunda, ina mamlaka yake, nje ya yale mambo ya Muungano na kila mmoja akijua kuwa michezo si suala la Muungano na wala halijawahi kuwa.
Pia kwa muundo huo kila nchi yaani Zanzibar na Tanganyika tuna Mawaziri wa Michezo, Wizara za Michezo, Mabaraza ya Michezo na Vyama vya Michezo na kuwa sisi kama ilivyo kwa Muungano wa Falme za Kiingereza (United Kingdom) tunakutana katika kuunda timu ya pamoja ya Olimpiki tu, basi!
Kama FIFA ni kigezo na kama United Kingdom ni kigezo basi pia muundo wa Tanzania ulipaswa kuwa ule wa vyama kuwakilisha maslahi ya kila upande ambayo vyovyote vile hata ikilazimishwa na CAF hayataweza kuendana na hali halisi ya ndani.
Kwa maana hiyo CAF ilipaswa pia kujua yafuatayo kuhusu muundo wa TFF, chama ambacho CAF inasema kiwakilishe maslahi ya Zanzibar:
a) Kwamba TFF ni ya Tanganyika pekee, na Zanzibar ipo ZFA.
b) Kwamba TFF iko chini ya Wizara yake na ZFA chini ya Wizara yake.
c) Kwamba Waziri wa Michezo anayesimamia TFF si wa Muungano na hana mamlaka ya Kimuungano.
d) Kwamba TFF ina Katiba yake yenye mamlaka ya eneo la Tanganyika bila kuigusa Zanzibar.
e) Kwamba muundo wa TFF una wanachama usioihusisha Zanzibar kivilabu au kimikoa.
f) Kwamba TFF haina na haijawahi kuwa na mamlaka ya kusimamia soka Zanzibar.
g) Kwamba TFF haina na haijawahi kuwa na program ya kuendeleza mchezo wa soka Zanzibar, na hata ikitaka haina mamlaka hayo.
h) Kwamba hakujawahi kuwa na kiongozi wa kuchaguliwa wa TFF kutoka Zanzibar, na hata akiwepo kikatiba hawezi kuiwakilisha Zanzibar kwa sababu michezo si suala la Muuungano.
i) Kwamba TFF haina mamlaka ya kuisemea wala kuiwakilisha Zanzibar kisheria na kikatiba.
j) Kwamba TFF haijawahi kuchukua ridhaa ya kuisemea ZFA na haijawahi kupewa ridhaa hiyo.
Waheshimiwa Wanahabari,
Mtaona basi kwa sababu ya mahusiano hayo tuloyataja hapo juu ya TFF na ZFA sisi CUF tunaiona CAF kuwa inataka kutulazimishia TFF juu ya Zanzibar na kwa lugha rahisi na ya moja kwa moja ni kuendeleza kile ambacho tumekipinga kwa muda mrefu – kulaliwa na Tanganyika kwa kuvaa koti la Muungano.
CAF wameshindwa kabisa kuelewa hilo na suala linakuja: Je, tumeshindwa sisi wenyewe kuwaelewesha? Kwa sababu ukweli ni kuwa hata CAF wakilazimisha kuwa TFF iwe ndio chama pekee cha kuwakilisha ndani ya taasisi hiyo, hali ndani ya Tanzania haitabadilika yaani TFF itakuwa ya Tanganyika na ZFA ya Zanzibar.
Ni kama vile tunavyolazimishwa sasa kuwa mambo yasiyo ya Muungano kusemewa na Wizara za Muungano na Wizara zisizo za Muungano kuisemea Zanzibar bila ya ridhaa yetu. Na hata zile za Muungano kutokuwa na wajibu wa kisheria wa kuhakikisha zinasikiliza sauti za Zanzibar. Hizi ndiyo sababu zinazowafanya Wazanzibari kuuona Muungano huu kukosa sura ya kuwa ushirika wa nchi mbili huru, na badala yake kuchukua sura ya Ukoloni wa Tanganyika dhidi ya Zanzibar.
Tuna masikitiko makubwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haikulipa kabisa uzito jambo hili kama ambavyo tulitaraji wakati wa kuomba uanachama kuwepo na ujumbe mzito wa Kiserikali wa Jamhuri ya Muungano akiwemo Waziri wa Habari na Waziri wa Mambo ya Nje.
Na sasa baada ya Zanzibar kutolewa kwa idhara kubwa, tunashuhudia kimya kikubwa kilichopo ambacho kinatisha bila kauli ya Waziri anayesimamia michezo na pia bila ya kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje na ndio maana tunaamini ndani ya Muungano, Zanzibar imebaki ni yatima, haina wa kumsemea na kwa hiyo ndio sababu kubwa ya CUF kudai Mamlaka Kamili ili isimamie kidete haki za Zanzibar. Na hiyo pia ndiyo sababu Wazanzibari wakaichagua CUF kwa ushindi mkubwa ili kusimamia mamlaka yao.
Waheshimiwa Wanahabari,
CUF inaamini kuwa ni vyema hili likasimamiwa kwa makini zaidi katika kuelekea kukata rufaa au kupinga uamuzi wa CAF wa kuitoa Zanzibar baada ya kupitishwa na Mkutano Mkuu na tuna hoja zifuatazo:
1. Wahusika kutoka Zanzibar wasilifanyie ajizi jambo hili na lifuatiliwe kwa utaalamu na umakini wote.
2. Wahusika waiarifu CAF kuwa kutwambia tuwakilishwe na TFF katika mazingira yaliopo sasa kunakaribisha ukoloni mamboleo, kwa sababu kikatiba na kisheria haiwezekani.
3. Tunaamini njia ya kutoka katika hili ni kuishawishi CAF iunde Tume Maalum kulifuatilia suala hili kwa kina na undani unaostahiki.
4. Iwapo jambo hili ni kwa maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, CUF inataka kuona unakuwepo mkazo wa hali ya juu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kuhusishwa kikamilifu Wizara ya Mambo ya Nje ambayo inapaswa kusimamia maslahi ya Tanganyika na Zanzibar kwa usawa. Wizara ya Mambo ya Nje si ya Tanganyika, ni ya ushirika wa Zanzibar na Tanganyika ndani ya Muungano.
5. Kwa kipindi hiki, Zanzibar isishiriki katika inayoitwa Timu ya Taifa ya Tanzania yaani Taifa Stars ili kusimamia hoja yake ambapo ni kichekesho cha kiulimwengu kuwa unaunda timu ya taifa kutoka Ligi Kuu mbili ndani ya nchi moja.
6. Zanzibar ijizuie kushiriki katika chochote kitakachoitwa ligi ya pamoja ili kusisitiza haki yake hiyo.
7. Zanzibar itoe kauli kwa CAF itayosema wazi kuwa haiwakilishwi kwa njia yoyote ile na TFF katika ngazi ya Afrika na FIFA kwa sababu sio tu kimuundo haina uwakilishi ndani ya TFF lakini pia kimuungano haiwezi kuwa hivyo.
8. Kampeni kubwa ya kimataifa iendeshwe kuieleza Afrika juu ya makosa na dhulma hii kubwa iliyofanywa na CAF dhidi ya Zanzibar ambapo ujumbe maalum utumwe kutembelea Balozi za nchi za Kiafrika ziliopo Dar es Salaam na pia kufika makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa.
9. Kutumia mitandao ya kijamii kupazia sauti kilio cha Zanzibar.
10. ZFA na Zanzibar iiambie CAF kuwa inapaswa ifikiri nje ya boksi kwamba kwa sababu za kimpira Zanzibar inayo haki ya kuwa mwanachama maana ina mfumo kamili wa soka katika ngazi zote zinazohitajika na FIFA kinyume na nchi nyingi ambazo ni wanachama wa FIFA bila kuwa wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Mwisho kabisa, CUF inawataka Wazanzibari kukaza kamba na kushtadi katika harakati zao za kudai muundo mpya wa Muungano utakaoheshimu Mamlaka Kamili ya kila nchi kati ya Tanganyika na Zanzibar kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kujinasua na kadhia kama hii ya kutolewa kwa idhara kutoka CAF.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
NASSOR AHMED MAZRUI
NAIBU KATIBU MKUU-ZANZIBAR


No comments:
Post a Comment