Imetolewa leo Tarehe 9/8/2017
Na. Kurugenzi ya Habari, Uenezi Na Mahusiano Na Umma-CUF Taifa
WENYEVITI WA SERIKALI ZA MTAA DAR ES SALAAM WAPINGA TAMKO FEKI LILILOTOLEWA BUGURUNI, WASEMA WAPO NGANGARI:
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mtaa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Bakari Kasubi (Ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mtambani kata ya Mzimuni, Magomeni-DSM) amekanusha vikali linaloitwa ‘TAMKO LA VIONGOZI WA SERIKALI ZA MITAA JIJINI DAR ES SALAAM…’ lililotolewa na Shilingi H. Shilingi Mwenyekiti S.Mtaa Keko Mwanga (B) jana Buguruni mbele ya waandishi wa habari.
Mhe Kasubi amesema Dar es Salaam ina jumla ya Wenyeviti wa Serikali za Mitaa 78, kati ya hao Wenyeviti 64 hawaungi mkono hujuma zinazofanywa na Lipumba na Genge lake ndani ya CUF.
Kama ilivyo kwa madiwani wote 21 wa Mkoa wa Dar es Salaam, Madiwani 19 wanampinga Lipumba na genge lake. Kama Shilingi anapingana na Tamko letu kwa kusema hatukukutana swali ni dogo tu yeye alikutana na nani kupanga kutoa Tamko hilo? Sisi tulikuwa “very clear” na tulisema wapo baadhi yetu hatuko nao tukijua kuwa hata Ibilisi/Shetani ana wafuasi. Jana pale tumemuona Wenyeviti watano tu waliohudhuria hapo Rajab Haruna-huyu Mnyamwezi wa Tabora kutoka kata ya Kurasini, Mkandu-Mwananyamala, kutoka Mbagala Kiburugwa, kutoka Kinondoni, na wengine ni wajumbe wa Serikali za mitaa. Hatujawaona hao Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wanaodai kukutana na kutoa tamko hilo.
Sisi kama wawakilishi wa wananchi hatuwezi kuwa makuadi wa CCM ndani ya upinzani. Kikao chetu kilihudhuriwa na Wenyeviti zaidi ya 50. Sisi hatuwezi kuyumba wala kuyumbishwa tunaunga mkono Chama chetu na kupinga Usaliti na Ukibaraka wa Lipumba na genge lake.
Lipumba hana Baraza Kuu kwa kuwa wajumbe wa Baraza Kuu wanapatikana kwa kuchaguliwa na Mkutano Mkuu wa Taifa kwa mujibu wa Ibara ya 79(i) (j)(k)(l)(m)(n) na (o) ya Katiba ya CUF.
Maalim Seif Sharif Hamad ndiye Katibu Mkuu na wala haitaji kutambuliwa na Wasaliti na anatekeleza vyema majukumu yake akiwa Makao Makuu ya Chama ambayo yapo Mtendeni, Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ya CUF ibara ya 1(2) inaeleza kuwa “ Makao Makuu ya Chama yatakuwa katika Mji Mkuu wa Zanzibar na anuani yake itakuwa kama itakavyoamuliwa na Baraza Kuu la uongozi la Taifa”
Mhe. Kasubi amehoji kama wanadai Maalim Seif Hafiki ofisini Buguruni, kwanini Lipumba hajawahi kufika Makao Makuu ya Chama Mtendeni Zanzibar kwa kipindi cha Mwaka wa pili sasa toka 2015?
Mhe kasubi amesema wao wenyeviti wanaunga mkono juhudi na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Chama kutokana na maamuzi halali ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lililokutana hivi karibuni Unguja, Zanzibar na kuhudhuriwa na wajumbe Halali 45 kati ya wajumbe Halali 52 kwa sasa kutokana na Wajumbe wengine 11 ambao wangefanya jumla ya wajumbe wote wa Baraza Kuu kuwa 63 wapo waliokwisha fukuzwa, kusimamishwa uanachama, kufa, na wengine kuhama Chama kama ilivyofafanuliwa katika tamko la Maazimio ya kikao hicho.
Amesema kamwe hawawezi kushiriki na kuwa sehemu ya uharibifu wa historia iliyotukuka ya Chama Cha CUF katika kudai Haki Sawa Kwa Wote nchini.
Mheshimiwa Kasubi ametoa wito kwa wanaCUF na Watanzania kwa ujumla kulipuuza Tamko hilo FEKI la wahuni, madalali wa CCM na kuendelea kubaki na msimamo wa kukitumikia Chama.
Dar es Salaam ni jiji la watu waelewa hakuna wanaCUF wala Wenyeviti wa Serikali za Mitaa walio makini wanaoweza kukubaliana njama za Lipumba na genge lake. – Bakari Kasubu- 0712833318
CUF NI TAASISI IMARA, YENYE VIONGOZI MAKINI.
HAKI SAWA KWA WOTE
MBARALA MAHARAGANDE
NAIBU MKURUGENZI

No comments:
Post a Comment