Pages

Tuesday, August 15, 2017

MKUTANO MKUU WA SKAUTI WA DUNIA 2017 UNAOFANYIKA NCHINI AZERBAIJAN

Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa katika Mkutano Mkuu wa Dunia wa Skauti 2017.
Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa katika Mkutano Mkuu wa Dunia wa Skauti 2017. 
Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa katika maadhimisho ya miaka 100 ya Skauti Tanzania.

15/08/2017
MKUTANO Mkuu wa Skauti wa Dunia unafanyika nchini Azerbaijan katika mji wa Baku kuanzia tarehe 14 hadi 18 Agosti 2017. 

Mkutano huu utajumuisha nchi zote wanachama ambao zinafikia nchi 167. 

Kila nchi inapaswa kutuma wajumbe 6 kuhudhuria mkutano huu, lakini pia waangalizi (Observers) wanakaribishwa. 

Ni mkutano mkuu ambao unazungumzia masuala mbalimbali yanayohusu mafunzo kwa vijana skauti, miradi mbalimbali, mafanikio na changamoto mbalimbali zinazokabili nchi wanachama. 

Tanzania inawakilishwa na wajumbe 6 muhimu kama Katiba ya Shirikisho la Vyama vya Skauti Duniani (World Scout Bureau) inavyosema, lakini pia ujumbe huo unaongozwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya 4 Mheshimiwa DK. Jakaya Mrisho Kikwete, kama Mlezi Mstaafu wa Chama cha Skauti Tanzania. 

Kwa kawaida Mlezi wa Chama cha Skauti Tanzania ni Rais wa Nchi kwa mujibu wa Katiba ya Chama cha Skauti Tanzania. 

Mheshimiwa DK. Jakaya Kikwete amepewa Heshima ya kuwa Msemaji Mkuu (Keynote Speaker) wa ujumbe wa Chama cha Skauti Tanzania. 

Ujumbe wa Chama cha Skauti Tanzania tayari umeshaondoka nchini kuhudhuria Mkutano huo, ambapo Mheshimiwa DK. Jakaya Kikwete ameomba kukutana na Viongozi wa Vyama vya Skauti nchi za Afrika kuzungumza na kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu uskauti barani Afrika wakati wa Mkutano Mkuu huo. 

Ujumbe wa Chama cha Skauti Tanzania ni pamoja na Skauti Mkuu Mheshimiwa Mwantumu Bakari Mahiza. Kamishna Mkuu Mheshimiwa Abdulkarim Esmail Shah. Naibu Kamishna Mkuu ndugu Rashid Kassim Mchatta. Kamishna Mtendaji Bi. Eline Kitaly. Na Kiongozi wa skauti kutoka mkoa wa D’salaam ndugu. Dinesh Rajah. 

Chama cha Skauti Tanzania kimetimiza Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake hapa nchini, na sherehe za maadhimisho hayo zilifanyika mkoani Dodoma kuanzia tarehe 21 hadi 28 Julai 2017 ambapo Viongozi mbalimbali wa Kitaifa walialikwa wakiwemo Marais Wastaafu, Mawaziri Wakuu, pamoja na Skauti wenyewe kutoka ndani na nje ya Nchi. 

Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa  Maadhimisho hayo alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ambaye alimuwakilisha Rais wa Nchi Mheshimiwa DK. John Pombe Magufuli. 

Tuzo na Nishani kadhaa zilitolewa kwa Viongozi mbalimbali wa Nchi, Viongozi wa Skauti, na skauti wenyewe ambao wameshiriki katika matukio ya ujasiri, michezo na mashindano za stadi za kiskauti. 
Maadhimisho ya Miaka 100 ya Skauti Tanzania yalifungwa na  Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi. 

Ujumbe wa Viongozi wa Chama cha Skauti Tanzania ambao wanahudhuria Mkutano Mkuu wa Skauti wa Dunia  pia utapokea Tuzo na Cheti maalum cha kutimiza Miaka 100 ya uskauti Tanzania, ujumbe huo  unatarajia kurejea nchini tarehe 21 Agosti 2017. 

HIDAN .O. RICCO.
KAMISHNA MKUU MSAIDIZI
MAWASILIANO NA HABARI

No comments:

Post a Comment