TANGAZO


Sunday, July 16, 2017

WAZIRI PROFESA MBARAWA ATOA MIEZI 10 KWA MKANDARASI CICO

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Tabora Eng. Damian Ndibalinze, akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, maendeleo yaliyofikiwa katika ujenzi wa barabara ya Tabora –Nyahua KM 85, wakati alipokagua ujenzi wake, Mkoani humo jana. 
Muonekano wa sehemu ya KM 6 ya barabara ya Tabora–Nyahua yenye jumla ya urefu wa KM 85, inayojengwa kwa kiwango cha lami, Mkoani humo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akitazama mchoro wa ujenzi wa kalvati itakayojengwa katika barabara ya Tabora-Sikonge yenye urefu wa KM 30, Mkoani humo jana.  
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mkazi anayesimamia ujenzi wa barabara ya Tabora-Sikonge yenye urefu wa KM 30 Eng. Golam Shahid, kumaliza mradi huo kwa viwango na ubora unaostahili, Mkoani humo jana. 
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Bw. Abeli Busalama, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wakati alipokuwa akikagua barabara ya Kaliua-Kazilambwa yenye urefu wa KM 56 iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami, Mkoani humo jana.

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amempa muda wa miezi kumi Mkandarasi wa Kampuni ya CICO anayejenga barabara ya Tabora-Sikonge yenye urefu wa KM 30 kwa kiwango cha lami kukamilisha kazi hiyo.

Prof. Mbarawa ameyasema hayo mkoani Tabora mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo na kuelezea kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wake. 

“Nakupa miezi kumi tangu sasa hadi mwezi Mei mwakani uwe umeikabidhi Serikali barabara hii”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa ukamilishaji wa barabara hiyo uendane na viwango na ubora vinavyoendana na thamani ya fedha waliyopewa ili barabara hiyo iweze kudumu kwa muda uliopangwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mwalimu Queen Mlozi, amemshukuru Waziri Prof. Mbarawa kwa kuufuatilia kwa karibu mradi huo ambao utachochea kasi ya maendeleo mkoani humo.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Tabora Eng. Damian Ndabalinze, amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa atamsimamia mkandarasi huyo kikamilifu ili barabara hiyo ikamilike katika kipindi cha miezi kumi.

Pia, Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Tabora-Nyahua yenye urefu wa KM 85 na kumtaka mkandarasi CICO anayejenga barabara hiyo kukamilisha KM 6 zilizobaki ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa amempongeza Mkandarasi CHICO anayejenga barabara ya Kaliua-Kazilambwa yenye urefu wa KM 56 iliyokamilika kwa kiwango cha lami na kusisitiza wananchi kuilinda na kuitunza barabara hiyo kwa kutoiharibu miundombinu yake.

Ametoa nafasi nyingine kwa mkandarasi huyo kuomba kazi nyingine za ujenzi wa barabara katika maeneo mengine mbalimbali ya nchi kwani utendaji wao ni wa viwango na wanamaliza kwa wakati.

Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Bw. Abel Busalama, ameipongeza Serikali kwa jitahada zake za kufungua Mikoa na Wilaya nchini kwa kujenga barabara za lami kwani barabara hiyo imefungua shughuli za kiuchumi na kimaendeleo wilayani kwake.

Waziri Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kikazi ya siku mbili ya kukagua miradi ya miundombinu iliyopo mkoani Tabora.

Imetolewa  na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments:

Post a Comment