Utata umegubika mdahalo wa moja kwa moja ambao unafaa kuwashirikisha wagombea wenza wa urais nchini Kenya.
Mdahalo huo, ambao utapeperushwa kupitia runinga, umepangiwa kufanyika leo jioni.
Hata hivyo, baadhi ya wagombea wenza wa urais wametangaza kwamba hawatashiriki katika mdahalo huo utakaofanyika katika Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki cha Afrika Mashariki (CUEA).
Miongoni mwa waliojitoa kutoka kwenye mdahalo huo ni mgombea mwenza wa chama cha Jubilee chake Rais Kenyatta, Naibu Rais William Ruto.
Mgombea mwenza wa muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa), wake Raila Odinga, Makamu Rais wa zamani Kalonzo Muysoka pia ametangaza kwamba hapangi kuhudhuria mdahalo huo.
Chama cha Jubilee kilikuwa kimedokeza kwamba kitamtuma mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung'wa, ambaye hana mtu anayempinga uchaguzini eneo bunge lake, angemuwakilisha Bw Ruto.
Kwa mujibu wa gazeti la Standard la Kenya, wagombea wenza Eliud Kariara, Emmanuel Nzai, Joseph Momanyi, Miriam Mutua, Titus N'getuny na Moses Maranga walikuwa wamemwandikia mwenyektii waandalizi wa mdahalo huo Debates Media Limited Wachira Waruru kusema hawakuwa wamepokea mawasiliano yoyote kuhusu mpangilio wa mdahalo huo.
Waandalizi hata hivyo walikuwa wamesema kwamba watawakubali wagombea wenzake pekee na kwamba mdahalo huo utaendelea kama ilivyopangwa.
Mdahalo wa wagombea urais umepangiwa kufanyika Jumatatu wiki ijayo.
Bw Kenyatta pia ametishia kutohudhuria mdahalo huo sawa na Bw Odinga.
Wawili hao walisema kuwa hawakushirikishwa wakati wa maandalizi ya mdahalo huo, na hawafurahishwi na mpangilio wake.
No comments:
Post a Comment