TANGAZO


Monday, July 17, 2017

TAMKO KWA UMMA - CUF YALAANI KAMATA KAMATA YA VIONGOZI

Salim Bimani
CUF - Chama cha Wananchi tunalaani, kitendo kilichoanzishwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ya kuwakamata Viongozi wa Vyama vya upinzani na kuwaweka rumande pasipo makosa yoyote.
Kadhia iliyotokea majuzi mkoani Ruvuma ya kumkamata na kumuweka ndani Katibu Mkuu wa CHADEMA Mhe, Dkt. Vincent Mashinji pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ndanda ambae pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kusini Mhe. Cecil Mwambe vilevile akiwemo na Mbunge Viti Maalum Kanda ya Kusini Mhe. Zubeda Sakuru, vitendo hivi ni ukiukwaji wa Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Vitendo hivi vya kamatakamata ni muendelezo wa utekelezaji wa maagizo kutoka juu katika kudhibiti harakati za vyama vya upinzani, ambapo ni kinyume na sheria za vyama vya siasa na Katiba ya nchi ibara 20. (1) Kila mtu anao Uhuru wa kukutana na watu kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.
Vilevile ibara 21. (2) Kila mtu anayo haki na Uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kifikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu yeye, maisha yake au yanayolihusu Taifa.
CUF - Chama cha Wananchi tumesikitishwa kumkamata Katibu Mkuu huyo wa CHADEMA akiwa ktk kikao cha ndani akikagua shughuli za chama katika majimbo ya kanda hiyo na kumtaka atoe maelezo kwa nini yumo katika mkoa huo na amekwenda kufanya nini? Hivi angekuwa ni Katibu Mkuu wa CCM angethubutu kumkamata na kumuuliza maswali kama hayo?
CUF - Chama cha Wananchi tunamuasa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mhe, John Pombe Magufuli, asiyatumie vibaya madaraka yake ya Urais aliyopewa na wananchi katika kufhibiti upinzani kama sehemu ya maandalizi ya kukinusuru chama chake na chaguzi zijazo za 2019 na 2020, wananchi wanapochoka huwa hawalazimishwi acha wafanye maamuzi wenyewe, na wala kuwadhibiti wapinzani hakutokusaidia bali ni kuhatarisha amani ya nchi kwa kuwajenga mazingira ya chuki na hasira.

CUF NI TAASISI IMARA, YENYE VIONGOZI MAKINI.
HAKI SAWA KWA WOTE
Imetolewa na Kurugenzi ya Habari CUF-Taifa
SALIM BIMANI
MKURUGENZI -MHUMU
0777414112/ 0752325227
MBARALA MAHARAGANDE
NAIBU MKURUGENZI-NMHUMU
maharagande@gmail.com
0715062577/0784001408

No comments:

Post a Comment