TANGAZO


Tuesday, July 18, 2017

TAARIFA: DAKTARI BINGWA WA TAASISI JKCI, PEDRO PALLANGYO APATA TUZO YA WATAFITI VIJANA WA KIAFRIKA 2017

Daktari Bingwa, Pedro Kisali Pallangyo
TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inafuraha kuutaarifu Umma  kuwa Daktari wake Bingwa wa Magonjwa ya Moyo ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo Pedro Kisali Pallangyo ameshinda tuzo  ya watafiti vijana wa Kiafrika kwa mwaka 2017 (Young African Researchers Awards 2017). 
Tuzo hiyo imetolewa na Taasisi ya Sayansi na Utafiti ya nchini Misri.
Dkt. Pallangyo alishinda tuzo hiyo baada ya kufanya utafiti wa kisayansi   katika masuala ya  Afya na dawa za binadamu kwa kuandika machapisho 16 katika majarida (Journal) saba ya Kimataifa ya Afya ya nchini Marekani.
Licha ya kukabidhiwa tuzo hiyo mshindi huyo atapewa  zawadi ya   dola za kimarekani 15,000 (zaidi ya milioni 30 za kitanzania), ngao na cheti.
Tuzo hiyo itakabidhiwa mwezi wa nane mwaka huu mjini Cairo na Rais wa Misri Mhe. Abdi El- Fattah Al-Sis.
Tangu kuanza kutolewa kwa tuzo ya watafiti vijana wa Kiafrika  mwaka 2014 Dkt. Pallangyo ni mtanzania wa kwanza kushinda. Mshindi wa mwaka jana alitoka nchini Ghana.
 Imetolewa na: 
Anna Nkinda
Msemaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete

No comments:

Post a Comment