Maelfu ya watu walijitokeza katika barabara za kuelekea nyumbani kwa Bradley Lowery, shabiki wa klabu ya Sunderland FC ya Uingereza, kutoa heshima zao za mwisho.
Lowery, mwenye umri wa miaka sita, alitoka Blackhall Colliery, County Durham.
Mvulana huyo alifariki Ijumaa wiki iliyopita baada ya kuugua saratani kwa muda.
Mchezaji Jermain Defoe, ambaye aliunda urafiki wa karibu sana na Bradley, aliungana na familia ya mvulana huyo kumuaga kwa mara ya mwisho.
Ibada ya wafu ilifanyika katika kanisa la Mtakatifu Yusufu kijijini mwao, wengi wakimsifu sana mvulana huyo kwa ukakamavu wake na sifa alizojilimbikizia.
Barabara za kuelekea kanisa la Mtakatifu Yusufu zilipambwa kwa puto na mabango yenye ujumbe wa kutoa heshima kwa Lowery.
Wengine waliacha ujumbe nje ya uwanja wa Sunderland wa Stadium of Light.
Waombolezaji walifika kwa wingi kanisani, hivi kwamba wengine walikaa nje.
Jamaa za Bradley walivalia jezi za soka, kukumbuka upendo aliokuwa nao kwa mchezo huo.
Mamake Gemma aliambia waliohudhuria mazishi hayo: "Alikuwa na tabasamu kubwa na la kupendeza hivi kwamba lilikuwa lingeangaza chumba chochote kile. Ni shujaa mwenye ujasiri, ametuacha.
"Aligusa nyoyo za wengi - aliwatia moyo watu wengi. Mwana wetu mpendwa, ndugu - nyota ya kupendeza.
"Ingawa wakati uliokuwa nasi ulikuwa mfupi, ni lazima una kazi ya kufanya huko mbinguni na malaika kwani Mungu amekuchagua wewe.
"Kwa sasa, mtoto wangu kwaheri, Hatu tutakapoonana tena shujaa wetu huko juu mbinguni."
Bradley alikuwa anaugua ugonjwa ambao kwa Kiingereza hufahamika kama neuroblastoma - aina nadra ya saratani - tangu alipokuwa na umri wa miezi 18.
Bradley alifanywa kuwa kibonzo-nembo wa klabu hiyo na akaunda urafiki wa karibu na mshambuliaji wa klabu hiyo Jermain Defoe.
Aidha, aliongoza wachezaji wa England kuingia uwanjani Wembley wakati wa mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Lithuania.
Bradley alipewa matibabu lakini saratani yake ikaibuka tena mwaka jana.
Wahisani walichangisha zaidi ya £700,000 kulipia matibabu yake New York mwaka 2016, lakini madaktari waligundua kwamba saratani yake ilikuwa imeenea sana na hangeweza kutibiwa.
Wazazi wake Gemma na Carl, kutoka Blackhall Colliery, Durham, waliambia Desemba kwamba alikuwa amesalia na "miezi kadha tu ya kuishi".
Miezi minne baadaye, walifahamishwa kwamba jaribio la mwisho kabisa la kumtibu lilikuwa limefeli.
Bradley alipendwa na maelfu ya watu na alipokea kadi 250,000 za kumtakia heri wakati wa Krismasi mwaka jana, kutoka kwa watu mataifa ya mbali kama vile Australia na New Zealand.
No comments:
Post a Comment