TANGAZO


Tuesday, July 18, 2017

BALOZI SEIF IDDI ATEMBELEWA NA MABALOZI W TANZANIA, ASHA-ROSE MAGIRO ALIYEKO UINGEREZA, MBELWA KAIRUKI ALIYEKO CHINA

Balozi wa Tanzania Nchini Uingereza na Ireland Dr. Asha Rose Migiro (kushoto), akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika kumtaarifa uwepo wa Kongamano la Uwekezaji katika Sekta ya Biashara na Uchumi kati ya Nchi hizo mbili.(Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (kulia) akimkaribisha Balozi wa Tanzania Nchini Jamhuri ya Watu wa China Balozi Mbelwa Kairuki kuzungumzia fursa za uwekezaji zinaweza kupatikana China kwa ajili ya Zanzibar.  
Balozi wa Tanzania Nchini Jamuhuri ya Watu wa China Balozi Mbelwa Kairuki akimuelezea Balozi Seif  fursa za uwekezaji zinazoweza kupatikana  Nchini China kwa ajili ya Zanzibar.

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
18/7/2017.
BALOZI wa Tanzania Nchini Uingereza na Ireland Dr. Asha Rose Migiro amesema Serikali ya Uingereza kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania Nchini humo na Ireland unatarajiwa kuandaa Kongamano la Uwekezaji katika masuala ya Biashara na Uchumi litakalotoa nafasi kwa Wawekezaji wa Nchi hiyo kuangalia fursa za kuwekeza Nchini Tanzania.

Hata hivyo alisema Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika mwaka huu ingawa hadi sasa bado hayajafikiwa maamuzi ya sehemu  gani litakapofanyika Kongamano hilo kati ya Tanzania au Uingereza.

Balozi Asha Rose Migiro alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar kumpa taarifa ya uwepo wa Kongamano hilo.

 Alisema maandalizi ya awali yameanza kuchukuliwa kwa kukutana na washirika wa suala hilo wakianzia upande wa Zanzibar ili maeneo ambayo Zanzibar itahitaji kutumia fursa ya kujitangaza kwenye Kongamano hilo.

Balozi Migiro alifahamisha kwamba mipango iliyowekwa na Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchimi Zanzibar {ZIPA}, Sekta za Kilimo, Utalii pamoja na Jumuiya ya ZATO iliyomo kwenye Mpango  Mkuu wa Taifa wa kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA) awamu ya Tatu imeonyesha mwanga wa kufanikisha azma hiyo njema.

Zanzibar ni Visiwa vinavyojitangaza vyenyewe Duniani kutokana na historia yake ya Kibiashara  Kimataifa kwa karne nyingi zilizopita kiasi kwamba sifa hizo zinastahiki ziendelezwe kwa manufaa ya Wananchi wake.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza mpango huo utakaosaidia kufungua ukurasa mpya wa Kiuchumi na Kibiashara kati ya Tanzania na Uingereza na Ireland kwa ujumla.

Balozi Seif alisema Wawekezaji kutoka Uingereza na Ireland wanaweza kuangalia maeneo ya kuwekeza Visiwani Zanzibar hasa katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia pamoja na uvuvi wa Habari kuu kwa vile wameshapiga hatua kubwa ya maendeleo katika maeneo hayo.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alikutana kwa mazungumzo na Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Jamuhuri ya Watu wa China Balozi Mbelwa Kairuki  aliyefika kumuelezea fursa mbali mbali zilizopo Nchini China ambazo Zanzibar inaweza kuzichangamkia.

Katika Mazungumzo hayo Balozi Mbela Kairuki alisema Zanzibar  inastahiki kwenda mbali zaidi katika ushirikiano wake na Majimbo mbali mbali ya  Jamuhuri ya Watu wa China katika  juhudi za kuimarisha Uchumi wake.

Balozi Kairuki alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba mawazo ya kufikiria Beijing itamaliza kila kitu kwa sasa yamepitwa na wakati kwa vile Serikali Kuu yenyewe ya Nchi hiyo imekabiliwa na mambo mengi inayostahiki kuyatekeleza kwanza kabla ya kufikiria kutoa misaada kwa marafiki zake. 

Alisema Majimbo la Jamuhuri ya Watu wa China yamefanikiwa kuwa na uwezo mkubwa Kiuchumi pamoja na njanja nyingi za Uwekezaji kiasi kwamba endapo Zanzibar itafanikiwa kutumia nafasi hizo inaweza kupiga hatua za haraka za maendeleo.

Alisema Sekta ya Utalii ni eneo pana linaloweza kufanikisha Uchumi wa Zanzibar katika kuwakaribisha Wawekezaji pamoja na Watalii kutoka China  ambao bado hawajatumia vilivyo soko la Afrika.

Balozi Kairuki alieleza kwamba  China hivi sasa iko katika kiwango kikubwa cha uwekezaji Duniani katika Sekta ya Utalii sambamba na Wananchi wake kupenda kutembea Nchi mbali mbali Duniani nafasi ambayo inaweza kulitononosha Taifa   iwapo kasi hiyo itaelekezwa Zanzibar.

Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif   Ali Iddi alizipongeza juhudi kubwa zinazochukuliwa na Balozi Kairuki katika kutafuta fursa za Uwekezaji Nchini China kwa ajili ya Zanzibar.

Balozi Seif alimuhakikishia Balozi Kairuki kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kuchangamkia  fursa hizo katika azma yake ya kuimarisha Uchumi na ustawi wa Wananchi wake.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema bado wapo baadhi ya Watendaji wenye dhamana ya kutoa maamuzi wamekuwa na  urasimu  wa kuchelewesha miradi na hatimae Wawekezaji walioamua kuweka vitega uchumi vyao  Nchini kukata tamaa na kuondoka Nchini.

Balozi Seif alitahadharisha wazi kwamba urasimu ni kitendo kibaya kinachoviza Maendeleo na kudumaza Uchumi wa Taifa.

No comments:

Post a Comment