Waziri
wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akizungumza kwa niaba ya Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa
hafla ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa mfumo wa kusafirisha na
kusambaza maji safi pamoja na matenki ya kuhifadhi maji katika Jimbo la Chalinze.
Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Chalinze,
Mhandisi Christer Mdomba, kulia ni Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi
Evarest Ndikilo.(Picha zote na Frank Mvungi-Maelezo)
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo akizungumza wakati wa hafla ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa mfumo wa kusafirisha na kusambaza maji safi kutoka mto Wami pamoja na matenki ya kuhifadhi maji katika Jimbo la Chalinze. Kushoto ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge,kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga.
Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa DAWASA, Mhandisi Romanus Mwangingo (Kulia) akitoa maelezo ya utekelezaji wa mradi kusafirisha na kusambaza maji safi pamoja na matenki ya kuhifadhi maji katika Jimbo la Chalinze.
Mbunge wa Chalinze, Mhe. Ridhiwan Kikwete (Kulia) akiteta Jambo na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Bw.Majid Mwanga Wakati wa hafla hiyo.
Moja ya tenki la maji linalojengwa katika chanzo cha maji cha mto Ruvu ikiwa ni sehemu ya mradi huo.
Mbunge
wa Jimbo la Chalinze, Mhe. Ridhiwan Kikwete akimshukuru Waziri wa Maji
na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge
kwa hatua nzuri iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo.
Mafundi wakiendelea na maandalizi ya ujenzi wa matenki yakuhifadhi maji katika chanzo cha maji Ruvu.
Na Frank Mvungi-Maelezo
TAKRIBAN wakazi 234,398 wa Chalinze watanufaika na mradi wa upanuzi wa mtambo na ujenzi wa mfumo
wa kusafirisha na kusambaza maji safi pamoja na matenki ya kuhifadhi unaolenga
kuondoa changamoto ya upatikanaji wake katika Jimbo hilo.
Akizungumza kwa niaba
ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa hafla ya kukagua maendeleo ya
mradi huo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge amesema kuwa Serikali
inaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo na kumtaka mkandarasi kuongeza
kasi katika kutekeleza mradi huo.
“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata
maji safi na salama ndio maana tumeweka wataalamu wetu hapa kumsimamia
mkandarasi ili afanye kazi kwa ubora na
kwa kasi kama ambavyo Waziri Mkuu aliagiza alipotembelea mradi huu mwezi Machi
mwaka huu”, alisisitiza Lwenge.
Akifafanua, Mhandisi Lwenge amesema kuwa hatua iliyofikiwa
katika utekelezaji wa mradi huo awamu ya
tatu ni ulazaji wa mabomba ya kusafirisha na ya kusambaza maji, ujenzi wa
matanki 19, na ujenzi wa mtambo wa
kusafishia maji ambao unaendelea.
Kazi nyingine zinazoendelea katika kutekeleza mradi huo ni
ujenzi wa vituo 351 vya kuchotea maji ambapo vituo 27 vimekamilika,vituo 226
vipo katika hatua mbalimbali na vituo 98 havijaanza kujengwa.
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa na mkandarasi wa mradi
huo, Mhandisi Lwenge amesema kuwa ni kuongezeka kwa upatikanaji wa vifaa kwa
wakati katika eneo la mradi, kuongeza wafanyakazi na maeneo ya kazi na kuteua
mwakilishi wa kampuni anayeweza kutoa maamuzi kwa niaba ya kampuni
inayotekeleza mradi.
Aidha, Waziri Lwenge amesema kuwa Serikali itatoa ufumbuzi
wa changamoto ya wananchi wa Jimbo hilo kulipia malipo ya huduma (service charge) hata pale wanapokuwa
hawajapata huduma hiyo ili kuwe na utaratibu mzuri unaowezesha wananchi kulipia
huduma pale wanapotumia tu na si vinginevyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Ridhiwani
Kikwete amesema yeye binafsi anaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna
inavyoshughulikia changamoto
zinazowakabili wananchi wa Jimbo hilo ikiwemo ya maji.
“Naridhika na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Awamu
ya Tatu ya mradi huo ambao ukikamilika utasidia kwa kiwango kikubwa kuondoa
changamoto ya upatikanaji wa maji katika jimbo hili hivyo wananchi wataweza
kuongeza kasi katika shughuli za maendeleo”, alisisitiza Ridhiwani.
Akifafanua amesema anaunga mkono juhudi za Serikali katika
kuwaletea wananchi maendeleo.
Mnamo mwezi Machi mwaka huu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Kassim Majaliwa alifanya ziara ya kutembelea mradi huo na kukagua shughuli za ujenzi
wa miundombinu ya mradi huo Awamu ya Tatu na baada ya ziara aliagiza
mkandarasi anayetekeleza mradi huo ambaye ni Overseas Infrastracture Alliance (OIA)Pv Ltd kutoka India mwenye
ubia na Kampuni ya Pratibha Industries nayo ya India kukamilisha kazi hiyo ,mkandarasi
wa mradi huo ameshalipwa shilingi 38,716,375,627 ikiwa ni asilimia 42 ya
gharama ya mradi.
Uhaba wa maji safi na salama umelikumba jimbo la Chalinze
kwa kipindi kirefu. Kwa sasa wanaopata huduma ya maji safi na salama ni
220,241, mradi ukikamilika, watakaopata huduma hiyo watafikia jumla ya 234,394.
No comments:
Post a Comment