Na Husna Saidi- Maelezo
SERIKALI kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imeanza kazi ya uboreshaji wa Reli ya Tanga ambayo ni moja ya chanzo cha kukuza uchumi ili kuleta maendeleo ya nchi.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Amandus Ngonyani alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Muheza Balozi Adadi Mohamed Rajabu wakati wa kipindi cha maswali na majibu katika bunge la kumi na moja aliyetaka kujua kuhusu suala hilo leo mjini Dodoma.
Mhandisi Ngonyani alisema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa Reli ya Tanga katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo nchini, tayari imeanza kufanya usanifu na tafiti mbalimbali zitakazosaidia zoezi hilo kufanyika kwa ufasaha.
“Mpango wa Serikali uliopo ni kuunganisha Bandari ya Tanga na Bandari mpya ya Mwambani kwenye Reli ya Standard Gauge ya Ukanda wa Kati kupitia Reli ya njia panda ya Ruvu hadi njia panda ya Mruazi ambayo imeunganisha Reli ya Kati na Reli ya Tanga hadi Arusha,” alisema Mhandisi Ngonyani.
Aidha alisema kuwa usanifu wa kina wa Reli ya kutoka Tanga hadi Arusha yenye kilomita 438 umekamilika hivyo kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuanza ujenzi wa Reli hiyo ya Tanga hadi Arusha kwa kiwango cha kimataifa.
Mhandisi Ngonyani aliongeza kuwa Mhandisi Msaidizi, Kampuni ya HP Geult ya Ujerumani inaendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kati ya Mikoa ya Arusha na Musoma pamoja na matawi ya kwenda Engaruka na Minjingu ili kuwezesha ujenzi huo kwa umakini.
Kufatia ujenzi wa Reli hiyo Serikali itafanikisha mpango mzima wa kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa kupokea mapato yatokanayo na matunda ya Reli hiyo.

No comments:
Post a Comment