Na Judith Mhina -
Maelezo
SERIKAL ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania imetenga maeneo ya uwekezaji mjini Dodoma kwa ajili ya
kujenga viwanda, mahoteli makubwa, nyumba za makazi na huduma muhimu za
kijamii.
Kwa mujibu wa
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) Mhandisi
Paskas Muragili amesema kuwa maeneo hayo ni Njedengwa, hekta 580 ambapo
miundombinu muhimu imewekwa ikiwemo maji,
umeme na barabara ya lami ili kurahisisha uwekezaji, eneo la Iyumbu hekta 78 na Western Industrial Area
hekta 334.6 (WIA).
Mhandisi Muragili
ameongeza CDA imetenga hekta
14,700 eneo la Kikombo, Chigongwe hekta
6, 278, Nyankali hekta 2,495 na Mtumba hekta 8,000, kwa ajili ya kujenga mji
wa Serikali ambapo kutajengwa
Wizara mbalimbali, Idara za Serikali,
Taasisi, na mashirika yatakayowekeza Dodoma.
Vilevile, eneo hilo
litajengwa makazi ya watumishi wa Umma na huduma mbalimbali za kijamii kama
masoko, zahanati, hoteli, maduka na nyumba za kuabudia kulingana na imani zao.
Akikaribisha
wawekezaji kuwekeza Dodoma, Muragili
amewahasisha Watanzania na wasio watanzania kuchangamkia fursa hiyo kwa
kujenga hoteli za kitalii za nyota tano
na zile za kawaida, kwa kuwa mji unategemea kupata wageni wengi siku za usoni.
“Nawakaribisha
wawekezaji wa ujenzi wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo, bila wasiwasi
niwahakikishie ardhi iliyopo Dodoma inatosha
kwa uzalishaji mkubwa wa malighafi mbalimbali zitakazohitajika
viwandani”.
“Aidha, Mkoa huu upo
katikati ya Tanzania hivyo malighafi
yoyote itakayohitajika ni rahisi kufika Dodoma ambayo imeunganishwa kila
kona na barabara za lami,” alisema Muragili.
Pia mikoa
inayoizunguka Dodoma ikiwemo Manyara, Singida, Iringa na Morogoro inaweza
kunufaika kwa wepesi zaidi na fursa hizo.
Akiwatoa hofu
wakazi wa Dodoma Muragili
amesema; “Ardhi itauzwa kwa bei
ya kawaida ili wananchi waweze
kumiliki viwanja”.
Ameyasema hayo akijibu
hoja za waandishi wa habari kuhusu kauli za wananchi kudai bei ya viwanja
itapanda, kutokana na ujio wa Makao Makuu ya Serikali, ambapo wananchi wa
kipato cha chini hawataweza kumiliki viwanja hivyo.
Muragili alisisitiza
kuwa viwanja havitapandishwa bei
kwani kwa sasa CDA inauza mita
moja ya mraba ya kiwanja cha makazi Shilingi
5,500 hadi 10,000 za fedha ya Tanzania, katika maeneo ambayo kitaalamu
tunayaita “medium density”.
Aidha, alisema kuwa
viwanja kwa ajili ya uwekezaji mkubwa mita moja ya mraba ni Shilingi
13,300 fedha ya Tanzania, maeneo hayo
kitaalamu yanaitwa “low density”.
Mhandisi Paskasi
Muragili ametoa angalizo kwa wanaohitaji kununua viwanja mjini Dodoma ya kwamba
anayetaka kiwanja lazima afike na kufuata taratibu za ofisi za CDA kwa kuwa ndiko viwanja
vinakopatikana.
“Tusinunue viwanja
kienyeji, mwisho wa yote utakuwa umedanganywa na madalali ambao kisheria ardhi
ya mji wa Dodoma iko chini ya CDA na haihitaji dalali ila ufuate taratibu
zilizowekwa”, alisema Muragiri.
Alimalizia kwa kusema
“Kwa wale wanaohitaji ardhi nje ya Dodoma kama Mpwapwa, Kongwa, Bahi, Kondoa,
Chemba na Chamwino wahakikishe
wanawasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ili wapate taratibu rasmi za ununuzi wa
ardhi.
Mapaka sasa eneo la
WIA lina viwanda kama Machinjio ya kisasa Dodoma na viwanda vya magodoro QFL na
Dodoma Halisi.
Mamlaka ya
Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ni miongoni mwa Mamlaka zilizopata ufadhili wa
kutekeleza mradi wa Uboreshaji Miji Kimkakati unaofadhiliwa na Mkopo wa Benki
ya Dunia na msaada kutoka Serikali ya Denmark.
Aidha, tamko la
serikali la mwaka 1973 lenye tangazo namba 230 la tarehe 12 Oktoba 1973 ndio
liilianzisha Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma kama mji mkuu wa Serikali ulipewa majukumu makuu 8.
Kutokana na wimbi la
mataifa ya Afrika kubadili miji mikuu, liliingia pia hapa nchini, na Hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa kwanza wa Tanzania, ambaye ni miongoni
mwa wana watiifu wa Afrika alionyesha dhamira hiyo “kuhamia’ Dodoma kama njia
ya kuunga mkono.
Historia ya kuhamisha
miji mikuu ilitokea miaka ya 1970 nchi nyingi za kiafrika zilibadili miji mikuu
ya serikali. Mathalani Malawi ambayo ilibadilisha mji mkuu kutoka Blantyre kwenda jiji la Lilongwe,na Nigeria ilihama
kutoka Lagos kwenda Abuja.
Hoja kubwa
iliyopelekea Mwalimu Nyerere kuchagua
mkoa huo ni kwamba Dodoma ni katikati mwa Tanzania, hivyo itarahisisha
kuleta maendeleo katika mikoa yote kwa urahisi hususan utoaji wa huduma za
msingi kwa wananchi.
Hiyo ndio hoja ya msingi
iliyomsukuma Mwalimu Nyerere kutoa maamuzi hayo ambapo alikuwa na uhakika iko
siku dhana yake itatimia, Hongera Rais Dkt. John Pombe Mangufuli kwa jitihada
zako za kutimiza ndoto za Muasisi wa taifa hili, sote tunaziona juhudi zako na
Watanzania wanakuunga mkono, Hapa Kazi Tu”.
No comments:
Post a Comment