Waziri Ummy Mwalimu, akizungumza na waandishi wa habari
Na Immaculate Makilika na Jovina Bujulu-Maelezo
18.03.2017, Dar es Salaam.
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekubali ombi la Serikali ya Kenya la kuwapatia madaktari 500 kufuatia upugufu wa madaktari uliotokana na mgomo nchini humo.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema kutoka na maombi yaliyotolewa, serikali imeandaa utaratibu kwa madaktari wa kitanzania kuwasilisha maombi yao katika tovuti ya wizara ya afya pamoja kufuata taratibu zingine kama watakavyoelekezwa.
Alizitaja sifa za anayetakiwa kuomba nafasi hiyo kuwa ni shahada ya kwanza ya udaktari, mafunzo ya vitendo pamoja na kusajiliwa na Baraza madaktari la Tanganyika na kutuma maombi hayo katika barua pepe; maombiyakazi@moh.go.tz kabla ya Machi 27saa 10 jioni.
Aidha, waombaji wanatakiwa kuambatanisha wasifu wao, nakala za vyeti vya taaluma na matokeo, cheti cha kuzaliwa, cheti cha kuhitimu mafunzo kwa vitendo pamoja na cheti cha usajili kutoka Baraza madaktari la Tanganyika.
“Tanzania hatuna upungufu wa madaktari isipokuwa Serikali haina uwezo wa kuajiri madaktari wote wanaohitimu, kwa kuwa kwa mwaka kuna wahimu 1200 wa shahada ya kwanza ya udaktari na uwezo wa kuajiri ni 450 tu” alisema Ummy.
Hata hivyo, Waziri Ummy alisema kuwa ajira hizo hazitawahusu watumishi wa umma, hospitali teule za halmashauri na mashirika ya hiari ambao wanalipwa mshahara na serikali. Madaktari watakaokidhi vigezo na sifa watapewa mkataba wa ajira wa miaka miwili.
Nchi ya Kenya inakabiliwa na upungufu wa madaktari kutokana na mgomo ulioanza mwezi Desemba mwaka jana, ambapo madaktari hao wamekuwa wakaidai nyongeza ya mshahara na marupurupu mengine.

No comments:
Post a Comment