TANGAZO


Wednesday, March 1, 2017

TRA NA WASHAURI WA KODI 100 WAJADILIANA SHERIA ZA KODI

Mkurugenzi wa Divisheni ya Mashauri ya Madai na Usuluhishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Obadia Kameya akifungua semina ya  elimu ya sheria za kodi iliyofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ambapo washauri wa masuala ya kodi walijadili namna ya utekelezaji wa mabadiliko mbalimbali katika sheria za kodi nchini. 
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo akizungumza wakati wa semina ya  kujadili namna bora ya utekelezaji wa mabadiliko katika sheria za kodi iliyofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania. 
Washauri wa masuala ya Kodi (Tax Consultants) walioshiriki katika semina ya kujadili namna bora ya utekelezaji wa mabadiliko ya sheria za kodi nchini iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na kampuni ya ushauri wa masuala ya kodi ya Hanif Habib & Co.Semina hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Benki Kuu jijini dar es Salaam. 
Mkurugenzi wa Divisheni ya Mashauri ya Madai na Usuluhishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Obadia Kameya akiwa katika picha ya pamoja na Washauri wa masuala ya kodi (Tax Consultants) baada ya semina ya majadiliano ya namna bora ya utekelezaji wa mabadiliko na maboresho katika sheria za kodi nchini kuisha.Semina hiyo ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa benki kuu ya Tanzania.

Na Jacquiline Mrisho – Maelezo.
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeendesha semina ya siku moja kwa washauri wa masuala ya kodi zaidi ya 100 kutoka taasisi mbalimbali nchini ili waweze kutoa tafsiri fasaha za sheria za kodi kwa wafanyabiashara wanaowahudumia.

Akifungua semina hiyo Jijini Dar es Salaam jana kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Divisheni ya Mashauri ya Madai na Usuluhishi, Bw. Obadia Kameya alisema semina hiyo imekuja wakati muafaka ambapo Serikali imejipanga kuzuia mianya ya ukwepaji kodi. 

Bw.Kameya alisema ukusanyaji wa kodi ndio chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali hivyo ni wazi kuwa TRA inategemea ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau wengine wakiwemo washauri wa masuala ya kodi ambao watasaidia kupeleka elimu fasaha ya tafsiri za sheria za kodi na kuchochea ulipaji wa kodi kwa hiyari kutoka kwa wafanyabiashara hivyo kupelekea nchi kuwa na maendeleo.

“Serikali inaamini kuwa semina kama hizi ni muhimu sana kwa wadau wa kodi kwa kuwa inatoa fursa ya kujadiliana ili kuongeza utashi na uelewa wa haki na wajibu wa kulipa kodi hivyo kusaidia kuchochea utamaduni wa kulipa kodi kwa hiyari ambao kwa kiasi kikubwa kutaongeza makusanyo na hatimaye kukuza uchumi,” alisema Bw.Kameya.

Aidha Mkurugenzi huyo alisema Serikali itaendelea kuwathamini na kuwajengea uwezo wadau wa masuala ya kodi ili waweze kuelimisha wengine na kusimamia vizuri walipa kodi na wananchi kwa ujumla wajue umuhimu wa kulipa kodi kwa kuwa ni jukumu la kila mtanzania anayetakiwa kulipa kodi, kulipa kwa hiyari.

Naye Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Bw. Richard Kayombo alisema vikao vya aina hiyo ni muhimu kwani vinatoa nafasi kwa wadau kujadiliana kuhusu fursa na changamoto zinazotokana na ukusanyaji wa kodi kwa nia ya kuimarisha mahusiano mazuri pamoja na kujenga uchumi wa nchi kwa kuwa kodi ndiyo msingi wa maendeleo.

“Kwa kupitia semina na mafunzo mbalimbali tunayoendesha mara kwa mara kwa wadau na wananchi kwa ujumla tumegundua kuna changamoto ya urasimu katika mchakato wa ulipaji kodi hivyo Ili kupunguza urasimu, tumejitahidi kuimarisha miundombinu ya kielektroniki itakayotuwezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali za ulipaji kodi”,alisema Kayombo. 

Lengo la Serikali na TRA kwa ujumla ni kuhakikisha mlipa kodi anatumia mitandao popote alipo kupata huduma anazozihitaji badala ya kutumia muda mwingi kufika kwenye ofisi zetu hivyo tumeanzisha baadhi ya programu kwenye mitandao zitakazorahisisha upatikanaji wa huduma zetu zikiwemo za ulipaji wa Ankara za Maji, umeme pamoja ving’amuzi, alisisitiza Bw.Kayombo.

“Kwa sasa TRA tunaboresha mifumo ya mitandao inayorahisisha ulipaji kodi bila mfanyabiashara kutembelea ofisi za TRA ambapo mlipakodi anaweza kupakua fomu na nyaraka mbalimbali kutoka katika tovuti na kulipia benki kwa kutumia simu ya kiganjani na hivyo kupunguza muda na kuepuka urasimu wakati wa kulipia,” alisema Bw. Kayombo. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni Binafsi ya Hanif Habib,Bi. Hanif Habib alisema mafunzo hayo yamewakutanisha pamoja Maafisa wa Kodi,wataalamu pamoja na jamii ya wafanyabiashara kutoka mashirika na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi hivyo ni kielelezo cha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika masuala ya maendeleo.

“Kukutana kwa wadau mbalimbali wa kodi katika mafunzo haya hausaidii tu kuchochea ongezeko la mapato bali kunahakikisha nchi inakuwa na maendeleo endelevu, kuchochea demokrasia na uwajibikaji nchini, pamoja na kupunguza utegemezi”,alisema Bi.Hanif. 
​​​​​

No comments:

Post a Comment