Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akimsikiliza Afisa Madini Mkazi Wilaya ya Tunduru, Mhandisi Fredrick Mwanjisi akielezea kuhusiana na shughuli za uchimbaji wa madini ya vito zilizokuwa zikifanyika kwenye Mto Muhuwesi, wilayani Tunduru.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza na baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ya vito wilayani Tunduru wakati alipotembelea eneo la Mto Muhuwesi.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akitoa maelekezo kwa Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Nyasa, Mhandisi Fredy Mahobe wakati wa ziara yake kwenye maeneo ya Mto Muhuwesi.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kushoto) akiondoka kwenye eneo la Mto Muhuwesi mara baada ya kusimamisha shughuli za uchimbaji wa madini ya vito ndani ya mto huo. Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, Daimu Mpakate (katikati) akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) ya kutembelea Mto Muhuwesi.
SERIKALI imezuia shughuli za uchimbaji wa madini ya vito kwenye Mto Muhuwesi wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma hadi hapo taarifa za kitaalamu zitakapotolewa mara baada ya kukamilika kwa zoezi la tathmini na ukaguzi.
Agizo hilo limetolewa hivi karibuni wilayani humo na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipofanya ziara kwenye mto huo ili kujionea hali ya eneo husika kufuatia ajali iliyosababisha kifo cha mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Kanje Ally na majeruhi mmoja ambao waliingia na kuanza kuchimba ndani ya mto.
Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Madini Mkazi wa Wilaya ya Tunduru, Mhandisi Fredrick Mwanjisi, zaidi ya watu sita walivamia eneo hilo la mto kufanya shughuli za uchimbaji wa madini kinyume cha taratibu kutokana na kutokuwa na vibali vilivyowaruhusu kufanya shughuli ya uchimbaji katika eneo hilo.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba shughuli za uchimbaji wa madini ndani ya Mto Muhuwesi zilisimamishwa tangu mwaka 2014 kufuatia pingamizi kutoka kwa Mamlaka ya Bonde la mto Ruvuma na Bonde la Kusini kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa rasilimali za Maji Namba 11 ya mwaka 2009 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira namba 20 ya mwaka 2004.
Kufuatia taarifa hiyo na baada ya kujionea hali halisi na kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo pamoja na viongozi wao, Waziri Muhongo aliagiza kusitisha haraka shughuli zote za uchimbaji madini kwenye mto huo hadi hapo taarifa ya tathmini ya athari ya shughuli ya uchimbaji kwa mazingira ya Mto Muhuwesi itakapokamilishwa na kuwasilishwa na wataalam kutoka Mamlaka ya Bonde la Mto Ruvuma, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Wizara ya Nishati na Madini (MEM).
Ili kuhakikisha suala hilo linapata ufumbuzi wa haraka, Waziri Muhongo alitoa miezi mitatu kwa wataalam kutoka Mamlaka hizo wawe wamewasilisha taarifa hiyo kwake na kwa uongozi wa Wilaya ya Tunduru.
No comments:
Post a Comment