Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Joyce Fissoo
Na Abuu Kimario
KATIBU Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Joyce Fissoo amesema
Serikali iko mbioni kukamilisha sera ya maendeleo ya filamu ambayo inategemewa
kuwa mwarobaini wa changamoto zinazoikabili sekta hiyo yenye kutoa ajira kwa
vijana wengi nchini.
Kauli ya kiongozi huyo wa taasisi ya Serikali yenye dhamana ya
kusimamia maendeleo ya sekta ya filamu nchini aliitoa wakati akijibu swali la
mtangazaji wa kipindi cha Tunatekeleza, Esha Muhiddin, kinachorushwa na runinga
ya TBC1.
Kwenye mahojiano hayo mtangazaji alitaka kujua kama sheria Na. 4
ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ya mwaka 1976 inakidhi mahitaji ya sasa ambapo
Bi. Fissoo alikiri kuwa sheria hiyo ina upungufu kwenye baadhi ya maeneo ambayo
ni ya muhimu kwa ustawi wa tasnia ya filamu na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Bi. Fissoo alieleza moja ya upungufu wa sheria hiyo ni kushindwa
kuwalazimisha watayarishaji wa filamu kutoka nje ya nchi kutoa mgao wa faida
wanazozipata baada ya kutumia mandhari za Tanzania kwenye filamu zao. Upungufu
huo umesababisha nchi kukosa mapato ambayo yangeweza kutumika kwenye miradi
mbalimbali ya maendeleo.
Upungufu mwingine wa sheria hiyo ya mwaka 1976 ni kuiona sekta
ya filamu kama chanzo cha burudani ambacho hakina thamani kwenye soko la bidhaa
na huduma. Mtazamo huu umepelekea wasanii wa filamu kushindwa kupata kipato
wanachostahili.
“Baada ya kutambua mapungufu hayo Serikali ya awamu ya tano
imedhamiria kukamilisha sera ya maendeleo ya filamu nchini ambayo itazaa sheria
na kanuni zitakazokuwa tiba ya changamoto zinazoikabili sekta ya filamu” Bi
Fissoo aliongeza.
Mbali na ujio wa sera ya maendeleo ya filamu nchini Bi. Fissoo
aligusia maeneo mengine ambayo serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Bodi ya Filamu Tanzania yamefanikiwa
kuyapatia ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wadau zaidi ya elfu
moja kwenye mikoa mbalimbali nchini.
Maeneo mengine ni kuiboresha Bodi ya Filamu Tanzania tokea mwezi
Julai 2016. Kwa sasa Bodi ina mamlaka kamili na muundo mpya unaowezesha
kusimamia majukumu mapya yaliyoongezwa ili kuhakikisha sekta ya filamu inakuwa
na mchango wa kutosha kwenye ukuaji wa uchumi.
Katibu Mtendaji huyo wa Bodi ya Filamu pia alitoa msimamo wa
serikali kuhusu tabia ya watayarishaji wa filamu za kizawa kuzigawa filamu zao
kwenye sehemu mbili (part 1&2) kuwa ni kitendo kischokuwa na nia njema na
kina lengo la kuhadaa walaji wa filamu za kitanzania.
Alibainisha tabia hiyo
kuwa moja ya sababu za kushusha soko la filamu za kitanzania ndani na nje ya
nchi.
Bi Fissoo amewaasa wadau wa sekta ya filamu nchini kujitokeza
kwa wingi kutoa mawazo yao ili kuboresha sera ya maendeleo ya filamu nchini
pale watakapo hitajika.
No comments:
Post a Comment