Na Jovina Bujulu- Maelezo.
WANANCHI wametakiwa
kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapoona mabango ya matangazo
barabarani ambayo wanayatilia shaka.
Haya yanasemwa jijini
Dar-es-salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na
watu wenye Ulemavu Mh. Janista Mhagama alipokuwa akizungumzia uwepo kwa utitiri
wa mabango ya ajira yanayoambatana na ahadi za uongo kwenye mishahara.
Alisema kuwa sheria
za uwekaji mabango barabarani zinazoongozwa na mamlaka husika zikiwemo Serikali
za Mitaa, Halmashauri ya Jiji na Miji ambazo huweka kanuni na taratibu za
mabango hayo.
“Mamlaka husika zina
wajibu wa kujiridhisha na kuhakikisha mabango yanayopewa ruhusa kubandika
barabarani ni sahihi, yanatangaza ukweli na yanafuata maadili” alisema Mhe.
Mhagama.
Waziri Mhagama
aliongeza kuwa ikibainika kuwa mabango hayo yanakwenda kinyume na utaratibu
waliokubaliana, mamlaka husika wana wajibu wa kuyafuatilia na kuyaondoa mabango
hayo ili kuondoa usumbufu usiowa lazima kwa wananchi.
Akizungumzia suala la
mabango yanayotangaza ajira yanayoambatana na ahadi za uongo, Mhe. Mhagama
amesema kuwa kuwa wizara yake ndiyo yenye dhamana ya ajira, inabidi wawasiliane
na mamlaka husika ambazo zimeruhusu mabango hayo ili wafuatilie na kuchukua
hatua stahiki.
Aidha, alizungumzia
ukaguzi unaofanywa na wizara yake mahali pa kazi alisema kuwa wao hawafuatilii
mabango bali huenda kufuatilia kama mwajiri anafuata sheria za kazi ikiwemo
mikataba, mishahara, afya na kupeleka michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi
za jamii.
“Tunapokuta
malalamiko ya wafanyakazi, au kukuta mwajiri hapeleki michango ya wafanyakazi
kwenye mifuko ya jamii, kuna adhabu za hapo kwa hapo kama vile kumtoza mwajiri
pesa” alisema Mhe. Mhagama.
Katika kuhakikisha
utendaji kazi unaridhisha na maridhiano sehemu za kazi Mhe. Mhagama alisema
kuwa wao kama wasimamizi wakuu wa ajira nchini wanafanya kazi kwa karibu na
shirikisho la vyama vya wafanyakazi na waajiri, ili kutatua kero za wafanyakazi
katika sehemu zao za kazi.
Kwa upande wake Mstahiki
Meya wa jiji la Dar-es-Salaam Mhe. Isaya Mwita alisema kuwa utaratibu wa kuweka
mabango upo kisheria katika halmashauri ila usumbufu mkubwa ni kuwa matangazo
madogo madogo ambayo mengi yanawekwa kwenye karatasi za A4 ambayo yanabandikwa
kwenye kuta za nyumba, nguzo za umeme na miti bila kufuata utaratibu.
No comments:
Post a Comment