Wanachama wa chama cha Democrats nchini Marekani wanasema bado hawajashawishiwa na matamshi ya karibuni ya mwanasheria mkuu Jeff Sessions kuhusiana na mawasiliano yake na balozi wa Urusi 2016.
Kiongozi wa wabunge wa chama cha Democrats Nancy Pelosi anaongoza wito wa kiongozi huyo mkuu wa mashtaka nchini humo kujiuzulu.
Rais Donald Trump amesema kwamba Sessions ni mtu mwaminifu na kusema kuwa shinikizo ya wanachama wa Democrats ni ya kibinafsi.
Bwana Sessions awali alijiondoa katika uchunguzi wa shirika la FBI kuhusiana na hatua ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani.
Lakini amesema hakudanganya wakati aliposema kuwa hakuwasiliana na raia wa Urusi.
Alisisitiza kuwa matamshi yake ni ya uaminifu na sawa kama alivyoelewa wakati huo.
Bwana Sessions alikuwa akizungumza baada ya kubainika kwamba alikutana na balozi wa Urusi Sergei Kislyaka mara mbili mwaka uliopita.
Bwana Sessions wakati huo alikuwa mwanachama wa kamati ya usalama katika baraza la seneti nchini humo.
Lakini tayari alikuwa mwanachama maarufu wa kundi la kampeni ya bwana Trump.
No comments:
Post a Comment