TANGAZO


Wednesday, March 1, 2017

BALOZI SEIF IDDI AKUTANA, AFANYA MAZUNGUMZO NA UONGOZI WA CHAMA CHA WASANII WA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA TANZANIA, WAMUELEZA AZMA YAO YA KUIBUA VIPAJI VYA WASANII WACHANGA ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Chama cha Wasanii wa Muziki wa Kiazai Kipya ofisini kwake, Vuga Mjini Zanzibar. Uongozi huo ulifika kumtaarifu rasmi azma yao ya kuandaa Tamasha la kuibua vipaji vya wasanii wanchanga Zanzibar linalotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ) 
Balozi Seif  akiwa katika picya ya pamoja na Uongozi wa Chama cha Wasanii wa Muziki wa Kiazai Kipya  aliofanya nao mazungumzo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Kulia ya Balozi Seif ni Msanii Jamila Abdulrahman (Babyjay) na Mohamed Abdulla Laki. Kushoto  ya Balozi Seif  ni Msanii Abdulkheir Chum na Msanii Rashid Mustapha ambae ni msemaji wa Chama hicho.

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
1/3/2017.
UONGOZI wa Chama cha Wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya Zanzibar { ZFU } unafikiria kuandaa mpango maalum wa kuwawekea Bima ya Afya wanachama wake kwa lengo la kuwakomboa wakati wanapokumbwa na matatizo ya Kiafya.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Chama hicho Mohamed Abdulla Laki  akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Wanne wa ZFU wakati wa mazungumzo yao na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.

Mohamed Abdulla Laki alisema inakuwa aibu na masikitiko makubwa  pale  Msanii ambaye ni kioo cha jamii anapoonekana akidhalilika wakati akitafuta huduma za matibabu kipindi anaposumbuiliwa na matatizo ya kiafya bila ya kupata msaada wa uhakika.

Alisema wapo baadhi ya wasanii katika zama tofauti zilizopita waliowahi kukumbwa na kadhia hiyo na kuishia katika mazingira ya kusikitisha huku jamii ikijisahau kwamba  wasanii hao walitumia nguvu, ujuzi na uzalendo wao katika kuielimisha jamii hiyo kupitia fani ya sanaa.

Mohamed Laki alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  kwamba Uongozi wa Chama cha Wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya umeanza hatua za awali za kusaidia wanachama na baadhi ya Wasanii pale wanapopatwa na matatizo ya kiafya.

Akizungumzia Tamasha la kuibua Vipaji vya wasanii wapya  linalotarajiwa kuandaliwa na Chama hicho Mwezi Septemba Mwaka huu Katibu wa Chama hicho Laki alisema wasanii watakaoonyesha uwezo mkubwa  watatunukiwa zawadi maalum ili kuwapa motisha wa kuendeleza vipaji vyao.

Hata hivyo Laki alisema kutokana na uanagenzi wa masuala kama hayo Uongozi wa chama chake uko tayari kupokea msaada, ushauri na hata mawazo kutoka kwa wataalamu waliobobea ili kuona lengo la kuandaa Tamasha hilo linafanikiwa vizuri.

Laki kwa niaba ya Uongozi na wanachama wa Chama hicho amemshukuru na kumpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa jitihada alizochukuwa za kuwaunga mkono kwa kuwapatia Ofisi na vifaa katika kuendesha shughuli zao zilizopata ufanisi mkubwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu sasa.

Alimuhakikishia Balozi Seif  kwamba  Wasanii  Vijana  wa Kizazi Kipya hivi sasa wamebadilika kimaadili kiasi kwamba hata sanaa zao wameamuwa kuzielekea zaidi katika maadili yanayohitajika na kukubalika na Jamii.

Alisema Uongozi wa Chama hicho tayari umeshaamua kwamba msanii ye yote wa Kizazi Kipya asiyezingatia maadili kwa mujibu wa Katiba ya Chama hicho wana uwezo wa kumzuia kuendelea na kazi zake.

Aliliomba Baraza la Sanaa Zanzibar kuendelea kukipa mashirikiano ya karibu zaidi Chama hicho ili kuona sheria, kanuni na Maadili ya kazi za Wasanii yanafuatwa na kuzingatiwa ipasavyo.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwaahidi Wasanii hao kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwasaidia  Vijana waliojiweka kimalengo katika kuendesha maisha yao.

Balozi Seif  alisema Sanaa ni miongoni mwa Sekta ambazo hutoa ajira hasa kwa vijana kutokana na umuhimu wake wa kuelimisha, kufurahisha sambamba na kufikisha ujumbe  kwa Jamii.

Alisema ili kuimarisha Sanaa Nchini ni vyema nyimbo zinazotungwa zikaendelea kutoa mafunzo na burdani akiwasisitiza Wasanii umuhimu wa kupenda kufanyakazi kwa kushirikiana na Umoja mambo yanayoshinda majungu na fitina.

Katika mazungumzo hayo Uongozi huo wa Chama cha Wasanii wa Muziki wa Kikazi Kipya {ZFU} umemkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Albamu Mpya iliyozindauliwa na chama hicho.

Albamu hiyo isemayo Amani kwanza yenye nyimbo zote za Kitaifa inakusudiwa kuuzwa kwa lengo la kusaidia kuendesha shughuli zao za kila siku zinazohitaji gharama kubwa katika utengenezaji wake.

No comments:

Post a Comment