Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akisikiliza maoni kutoka kwa
Bw. Mohammed Ally mkazi wa Nakapanya, Wilayani Tunduru, Mkoani Ruvuma kuhusu furaha
yao juu ya kukamilika kwa ujenzi wa Barabara ya Nakapanya-Tunduru KM 66.5.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akionesha kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), picha ya barabara ya Nakapanya-Tunduru KM 66.5 iliyokamilika kwa kiwango cha lami wakati alipokuwa akikagua barabara hiyo, mkoani Ruvuma. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Bw. Juma Homera.
Muonekano wa barabara ya Nakapanya-Tunduru KM 66.5 iliyokamilika kwa kiwango cha lami, mkoani Ruvuma. Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Ruvuma Eng. Lazeck Alinanuswe (mwenye koti la kaki), akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto kwa Meneja), ujenzi wa kingo za Daraja la Lumesule lililopo mpakani mwa mkoa wa Ruvuma na Mtwara wakati alipokagua daraja hilo.
Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Mhe. Dua Nkurua (kushoto), akisisitiza jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kulia), mara baada ya kuzungumza na uongozi wa wilaya hiyo, mkoani Mtwara.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Bw. Juma Homera (mwenye koti la kaki), akimuonyesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto kwa Mkuu wa Wilaya), moja ya ofisi katika jengo jipya la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya huyo, alipoikagua Wilayani humo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiongea na uongozi wa Wilaya ya Tunduru, mara baada ya kukagua miradi iliyo chini ya Wizara hiyo.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akifurahi jambo na wafanyakazi
wa kampuni ya Korosho, Wilayani Tunduru mara baada ya kutembelea na kuangalia
uzalishaji wa korosho katika kiwanda hicho.
WANANCHI wa Nakapanya, wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma wameridhishwa na kasi ya
utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Nakapanya-Tunduru yenye urefu wa
KM 66.5 ambayo imekamilika kwa asilimia Tisini na tisa na sasa
mkandarasi yuko kwenye hatua za kumaliza uwekaji wa alama za barabarani.
Wakieleza
furaha yao kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa mara baada ya kukagua barabara hiyo, wananchi hao wamesema kuwa
uwepo wa barabara hiyo umechochea maendeleo makubwa katika mkoa huo na mikoa ya
jirani.
"Tunaishukuru
sana Serikali kwani imesikia kilio chetu cha miaka mingi cha kuomba
kujengewa barabara ya lami katika wilaya yetu, sasa tunafurahia matunda ya
ujenzi huu", amesema Bw. Mohammed Ally.
Kwa
upande wake, Waziri Prof. Mbarawa amewataka viongozi wa Wilaya hiyo na kamati
za ulinzi na usalama kuhakikisha wanawasimamia wananchi katika kuitunza na
kuilinda miundombinu ya barabara hiyo ili iweze kudumu na kuweza kutumika kwa
vizazi vijavyo.
Ameongeza
kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kumeufungua mkoa wa Ruvuma na wilaya zake
pamoja na mikoa jirani ya Mtwara na nchi ya Msumbiji, hivyo kuchochea fursa za
kibiashara kwa kiasi kikubwa.
Kuhusu
huduma za mawasiliano mkoani humo,
Waziri Mbarawa amesema kuwa Wizara yake itahakikisha inapeleka mawasiliano
haraka iwezekanavyo katika maeneo yenye changamoto hususan vijijini.
Naye,
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Bw. Juma Homera amemhakikishia Waziri huyo kuwa
atashirikiana kwa ukaribu na viongozi wenzake katika kutekeleza maagizo yote
aliyowapa ikiwemo la ulinzi wa miundombinu ya barabara hiyo.
Meneja
wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Ruvuma amemuhakikishia Waziri
Prof. MBARAWA kuwa Wakala utatatua changamoto zote zilizojitokeza wakati
wa ujenzi wa barabara ikiwemo fidia kwa wananchi waliovunjiwa nyumba zao
kupisha barabara hiyo.
(Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano)
No comments:
Post a Comment