TANGAZO


Monday, February 27, 2017

WAKAZI 214 DAR ES SALAAM KUPEWA HATI ZA ARDHI

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akionyesha baadhi ya nyaraka za ardhi wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Angelina Mabula na kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Yamungu Kayandabila.    

Na Jacquiline Mrisho – Maelezo
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetayarisha hati 214 kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam waliosalimisha ofa zao za umiliki wa ardhi kwenye wizara hiyo ili waweze kumiliki  ardhi hizo kihalali.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini humo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya mambo mbalimbali yanayohusu wizara hiyo.

Waziri Lukuvi amesema kuwa ni rahisi kwa wananchi wenye umiliki wa ofa kutapeliwa kuliko wakiwa na umiliki wenye hati ambazo ni halali hivyo ili kuondoa changamoto hiyo wizara ilitoa muda kwa wananchi kupeleka ofa hizo ili watayarishiwe hati halali.

“Kuwa na umiliki halali wa ardhi ni jambo kubwa kwa usalama wa wananchi wenyewe, nataka ifike siku Tanzania iwe haina mtu anayemiliki ardhi kwa kutumia ofa kwa sababu sasa hivi wizara haitoi ofa, ofa hizo zilishakoma siku nyingi,”alisema Lukuvi. 

Ameongeza kuwa ingawa muda wa kusalimisha ofa hizo za umiliki umekwisha lakini wizara hiyo inatoa muda zaidi kwa watu ambao bado hawajapeleka ofa zao katika Halmashauri zao za wilaya kupeleka ofa hizo ili waweze kumiliki ardhi hizo kwa hati.  

Aidha, akiongelea kuhusu utayarishaji wa teknolojia itakayohusika na masuala yote ya ardhi inayojulikana kama ‘Mfumo Unganishi wa Ardhi’, Waziri Lukuvi amesema kuwa tayari Kampuni ya Kifaransa iliyoshinda tenda inaendelea na kazi na mnamo Julai mosi mwaka huu hati ya kwanza ya kielektroniki ya mfano itatolewa.

Tayari jengo litakalotumika kwa ajili ya shughuli hizo limeshakamilika na mfumo huo bado unaendelea kutengenezwa ili kuwezesha wananchi wote wanaomiliki ardhi Tanzania wanamilikishwa hati za kielektroniki.

No comments:

Post a Comment