TANGAZO


Saturday, February 25, 2017

BALOZI SEIF IDDI AZINDUA MAADHIMISHO YA MIAKA 40 YA JESHI LA KUJENGA UCHUMI ZANZIBAR (JKU) ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikaguwa Gwaride rasmi lilioandaliwa katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Kutimia miaka 40 tokea kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU) hapo Skuli ya Sekondaroi a Ufundi ya JKU Mtoani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar akimuwakilisha Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Balozi Seif akizindua rasmi Bendera ya Kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar hapo Mtoni ikiwa mwanzo wa maadhimisho ya Jeshi hilo kutimia miaka 40 tokea kuanzishwa kwake.

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
25/2/017.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mainduzi Dr. Ali Mohamed Shein alisema mafunzo yanayotumia mbinu za kisasa katika kuimarisha kilimo na ufugaji yanayozingatia taalum ambayo hupatiwa Vijana wanaojiunga na Jeshi la Kujenga  kujiajiri wenyewe.

Alisema Serikali tayari imeshaandaa mpango  kwa kuwawezesha Wananchi Kiuchumi wakiwemo Vijana pale wanapoamua kujikusanya kuanzisha miradi ya kiuchumi  na hupata msukumo wa mkopo kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi unaoratibiwa na Wizara inayosimamia Ustawi wa Jamii Uwezeshaji wa Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto.

Dr. Ali Mohamed Shein  alieleza hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizindua maadhimisho ya kutimia kwa miaka 40 ya kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar {JKU} hao katika viwanja vya Skuli ya Sekondari na ufundi ya JKU Mtoni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema ni jambo la kutia moyo kuona kwamba majukumu ya msingi ya Jeshi la Kujenga Uchumi yanatekelezwa na kutafsiriwa kwa vitendo hasa pale wasimamizi na wataalamu wa Jeshi hilo wanapoelekeza nguvu zao katika kuwahimiza Vijana wao kuimarisha sekta ya Kilimo na Ufugaji.

Rais wa Zanzibar alisema Jeshi la Kujenga Uchumi ambalo ni kioo cha Vijana limekuwa likizingatia mchango muhimu unaopatikana katika sekta ya Kilimo na Ufugaji ambazo hutoa fursa za ajira kwa Wananchi waliowengi katika Jamii, kuongeza kipato pamoja na kupatikana kwa liche bora.

Dr. Shein alitoa rai kwa Viongozi wa Majimbo Nchini pamoja na vikundi vya ushirika kuitumia fursa ya kwenda kujifunza elimu ya Amali na Ufundi katika Kambi za JKU zenye utaalamu mkubwa unaoweza kuwasaidia katika kuongeza ufanisi katika miradi yao.

Rais wa Zanzibar alisema kutokana na faida wanazozipata Vijana wanaojiunga na Jeshi la Kujenga Uchumi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaliangalia upya suala la utaratibu wa sasa wa kujiunga na JKU kwa hiyari.

Hata hivyo Dr. Shein alihimiza kwamba Serikali inaendelea kusisitiza umuhimu wa kutoa ajira hasa kwa Vijana wanaojiunga na Vikosi vya Ulinzi ambao wamepitia na kupata mafunzo JKU na JKT.

Alisema hatua hiyo ina manufaa makubwa kwa kuwapata Vijana  ambao tayari wamekwisha andaliwa vyema katika masuala ya ulinzi, uzalendo na ujenzi wa Taifa hatua itakayowatia pia ari Vijana wenye moyo wa kujitolea.

Akigusia Taaluma  ya juu kwa wapiganaji wa Idara Maalum za SMZ Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alivitaka Vikosi vya SMZ  kuandaa utaratibu maalum wa mafunzo kwa watumishi wao katika fani mbali mbali.

Alisema fani za ualimu, udaktari, Baharia, wataalamu wa kilimo, mifugo na za amali bado zinahitajika katika Vikosi hivyo ili kuvihakikishia vinakuwa na wataalamu wa kutosha.

Dr. Shein alieleza kwamba kutokana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia, lazima vikosi vya SMZ vijiandae kwa ajili ya kwenda sambamba na mabadiliko kwa kuwasomesha watumishi wake.

Rais wa Zanzibar alilipongeza Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwapatia elimu ya msingi, Sekondari na Ufundi Watoto mbali mbali  katika skuli yao waliyoianzisha hapo Mtoni.

Alisema hilo nii jambo jema lililoonyesha mfano mzuri wa kutumia vyanzo vya ndani vya mapato yao kwa kuanzisha miradi mikubwa ya ujenzi wa jengo la skuli ya sekondari ya JKU Mwaka 2007.

Dr. Shein alitoa wito wa Wazazi na Walezi hasa wale wanaoishi maeneo ya karibu na skuli hiyo kutumia vyema fursa ya kuwepo kwa skuli hiyo ili kuendeleza ndoto za Watoto katika kupata elimu huku akiwataka walimu kuongeza juhudi katika kuona kiwango cha ufaulu kinazidi kuimarika kila mwaka.

Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi na wapiganaji wa Jeshi la Kujenga Uchumi {JKU} pamoja na vikosi vyote vya Idara Maalum kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na vikosi hivyo ili viwe na nguvu na uwezo wa kutekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa.

Alisema Serikali itazifanyia kazi changamoto zinazovikabili vikosi hivyo kwa kuandaa mpango madhubuti utakaotoa nafasi ya kuchukulia hatua kulingana na hali ya uchumi itakavyoruhusu.

Aidha alisisitiza kwamba suala la marekebisho ya maslahi kwa wapiganaji wa Idara Maalum za SMZ litazingatiwa ipasavyo ili angalau lilingane na wenzao wa vikosi vya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyoahidiwa na Serikali.

Dr. Shein alisema hatua hiyo ambayo itatekelezwa sambamba na marekebisho ya mishahara ya watumishi wengine wa Serikali ina lengo la kuwapunguzia makali ya maisha wapiganaji hao na kuwapa moyo, ari na imani kwa kufanya kazi zaidi.

Mapema akitoa Taarifa za maadhimisho ya kutimia kwa miaka  40 ya kuanzishwa kwa JKU Kaimu Kamanda wa Kikosi hicho Kanali Ali Mtumweni Ali alisema Watumishi wengi wenye nidhamu zilizowapelekea kupanda daraja ndani ya Taasisi zao wamepitia na kupata mafunzo ya lazima ya mwaka mmoja ndani ya JKU.

Kanal Ali Mtumweni alisema zaidi ya Vijana 55,000  waliomaliza masomo yao tokea kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar Tarehe 3 Machi mwaka 1977 ndani ya Mikupuo 62  wamepitia JKU kwa mujibu wa Sheria.

Alisema JKU katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuwajenga Vijana kimaadili, Kiulinzi, Uzalendo na kujitegemea hivi sasa iki katika matayarisho ya  kuanzisha kiwanda cha chakula cha Kuku ili kupunguza gharama za uagizaji unaofanywa kutoka nje ya Zanzibar kwa hivi sasa.

Kaimu Kamanda huyo wa JKU alielezea faraja yake kutokana na uhusiano mzuri unaoendelea kuwepo kati ya wapiganaji wa Jeshi hilo na Wananchi wanaozizunguuka kambi za Vikosi hivyo katika sehemu mbali mbali Unguja na Pemba.

Alisema uhusiano huo umewapa nguvu na ari ya kushiriki katika kazi za Kijamii wanapopangiwa kuzitekeleza hasa katika matukio ya maafa, ujenzi wa majengo ya Umma amoja na huduma za Afya.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mkikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mh. Haji Omar Kheir alisema lengo la kuanzishwa kwa Kambi za Vijana na baadaye JKU ni kuwaunganisha Vijana kuwa wamoja bila ya kujali asili au nitikadi zao.

Mh. Haji alisema Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inatambua uwepo wa Idara Maalum za SMZ ambazo zinaunganisha Vikosi vyake kikiwemo cha JKU kilichopewa jukului la kuwalea Vijana kuelekea katika maadili mazuri ya kimaisha.

Alisema katika kuona Kikosi hicho kinafikia malengo yake Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala wa Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ iko katika mpango wa kufanya mapitio ya kuangalia majukumu ya JKU  inavyoyatekeleza tokea kuanzishwa kwake Mwezi Machi mwaka 1977.

Mapema  alizindua Bendera ya Jeshi la kujenga Uchumi {JKU} na baadae kutembelea maonyesho ya kazi mbali mbali zinazotekelezwa na wapiganaji hao wa Jeshi hilo.

Maonyesho hayo ni pamoja na miradi ya kilimo, ufugaji, ushoni, huduma za picha, ufundi saramala pamoja na ushoni. 

No comments:

Post a Comment