Mkate, chipsi na viazi pamoja na vyakula vingine havifai kuchomwa au kupikwa hadi kupata rangi ya hudhurungi, wataalamu wameonya.
Badala yake, wanasema zinafaa kupikwa hadi viwe na rangi ya manjano iliyokolea dhahabu.
Wanasema hilo litapunguza ulaji wa kemikali ambayo huenda inachangia saratani.
Acrylamide huzalishwa wakati vyakula vyenye wanga vinapochomwa au kukaangwa kwa muda mrefu katika kiwango cha juu sana cha joto.
Wakala wa Viwango vya Ubora vya Chakula Uingereza (FSA) anapendekeza wapishi wafuate vyema maagizo wakati wa kupika na wasiache chakula kipate rangi ya kahawia.
Shirika la kukabiliana na kansa la, Cancer Research UK, linasema hata hivyo kwamba uhusiano wa moja kwa moja kati ya Acrylamide na saratani miongoni mwa binadamu haujathibitishwa.
FSA wanasema pia kwamba viazi na mboga aina ya karoti ziitwazo parsnips hazifai kuhifadhiwa kwenye friji.
Hii ni kwa sababu viwango vya sukari kwenye mboga huongezeka zinapohifadhiwa kwenye viwango vya chini sana vya joto (mazingira baridi) na hivyo kuongeza kiasi cha Acrylamide inayozalishwa chakula kinapopikwa.
Acrylamide hupatikana katika vyakula vingi na huzalishwa chakula kinapopikwa.
Viwango vya juu vya kemikali hiyo hupatikana wakati wa mapishi, vyakula vyenye viwango vya juu vya wanga kama vile viazi, vibanzi (chipsi), mkate na parsnips, vinapookwa, kuchomwa au kukaangwa katika viwango vya juu sana vya joto.
Viwango vya juu vya acrylamide hupatikana kwenye vyakula vyenye kiwango cha juu cha wanga vinapopikwa viwandani kwa joto ya zaidi ya nyuzi joto 120C, kama vile kaukau, mkate, biskuti, keki na kahawa.
Aidha, huzalishwa nyumbani wakati wa kupika vyakula vyenye viwango vya juu vya wanga kama vile viazi, chipsi, mkate na pasnips kwa kuoka, kuchoma au kukaanga katika kiwango cha juu sana cha joto.
Mkate unapochomwa na kutengeneza tosti, kwa mfano, hilo huzalisha acrylamide zaidi.
Kadiri rangi ya tosti inavyokolea hudhurungi (kahawia), ndivyo kiwango cha acrylamide kinavyokuwa juu.
Wakati wa chakula kubadilika rangi na kuwa cha hudhurungi, sukari, amino asidi na maji kwenye mkate hushikana na kutengeneza rangi na acrylamide - pamoja na ladha tamu na harufu nzuri.
FSA wanasema hawana uhakika binadamu anafaa kula kiasi gani cha acrylamide bila kupata madhara.
Hata hivyo, wanasema wanaamini kwamba binadamu kwa sasa wanakula chakula chenye kiwango cha juu cha acrylamide kupita kiasi.
Watu wanashauriwa:
- Kupika chakula hadi kiwe rangi ya manjano ya dhahabu
- Kutohifadhi viazi vibichi kwenye friji, badala yake hifadhi kwenye ghala au phala penye giza, eneo lenye kiwango cha joto zaidi ya nyuzi 6C
- Fuata maagizo yaliyotolewa wakati wa kupasha moto chipsi, pizza, viazi na parsnips
- Kula chakula bora chenye afya, chenge vipimo vitano vya mboga na matunda kila siku pamoja na kabohaidreti ya kutoka kwa chakula chenye wanga.
No comments:
Post a Comment