Pages

Friday, January 6, 2017

MIAKA 53 YA MAPINDUZI: DK. MOHAMMED SEIF KHATIBU, “MAPINDUZI YAMEONDOA MATESO KWA WAAFRIKA WA BARA NA VISIWANI”

Mwanasiasa mkongwe, Waziri mstaafu katika Serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Seif Khatib

Na Judith Mhina - Maelezo
KATIKA kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar Idara ya Habari - MAELEZO ilipata fursa ya kufanya mahojiano na Mwanasiasa Mkongwe, Waziri Mstaafu katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Pili, Tatu na ya Nne  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na Mtaalamu wa Lugha ya Kiswahili Dkt. Mohammed Seif Khatib kuhusiana na maadhimisho hayo. Yafuatayo ni maswali na majibu katika mahojiano hayo:

SWALI: Zanzibar imetimiza miaka 53 ya Mapinduzi ni jambo gani muhimu la kuwaeleza Wazanzibar?

JIBU:
Kwa lugha fupi nasema “Mapinduzi Daima” Mapinduzi yaliyofanywa mwaka 1964 yanahitaji kuendelezwa kwa sababu yamesaidia ukombozi wa Waafrika, yameondoa utawala wa Uingereza na Waarabu. Madhila ya Zanzibar hayawagusi Waafrika wa Zanzibar peke yake, bali pia  Waafrika wa Tanzania Bara.  Mapinduzi hayo yalikusudia kuondoa madhila hayo, yaani utumwa, masuria kufanyishwa kazi, kuteswa  kudhalilishwa kunyanyaswa kudharauliwa na kuuzwa kama samaki. “Mapinduzi Daima” maana yake ni endelea kutekeleza yale yaliyokusudiwa na “Mapinduzi” yaani kupata huduma bora za afya, elimu, maji, Umeme na  makazi bora

SWALI:
Mheshimiwa Mohammed Seif Khatib wewe ni kati ya watu wachache waliobobea katika siasa na umeitumikia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Unadhani muelekeo uliopo mpaka sasa unaleta hali halisi ya matarajio ya Mapinduzi yaliyofanyika mwaka 1964?

JIBU
Muelekeo upo kwa maana ya “Ndio au Hapana” kwa sababu miisingi ya Mapinduzi Zanzibar ni kubadilisha hali ya  Wazanzibar wanyonge waliowemgi katika maeneo ya elimu, afya, maji umeme na makazi bora ambapo Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Hayati Shekh Abeid Amani Karume aliltimiza lengo.

Sababu za kiuchumi Zanzibar ni kisiwa na kina eneo dogo sana la kuwekeza kwenye sekta mbalimbali za uzalishaji na sekta ambayo ni kubwa ya uvuvi haijaendelezwa kwa sababu wananchi wana  zana duni za uvuvi.

Mara baada ya Mapinduzi uchumi wa Karafuu ulikuwa mzuri na bei katika soko la dunia ilikuwa kubwa. Idadi ya watu wakati wa Mapinduzi ilikuwa laki tatu na nusu, karafuu ilikuwa na bei nzuri sana kwenye soko la dunia sasa imeshuka sana bei duniani na Idadi ya watu imeoongezeka mpaka milioni moja na nusu, hii ina maana tunatakiwa kuzalisha mara sita zaidi ya tulivyokuwa tunazalisha 1964.

Sekta ya ujenzi inaongeza majengo makubwa makubwa na eneo la Zanzibar haliongezeki. Hivyo kwa sasa inatubidi kunoa bongo zaidi kuwa na viwanda ambavyo havihitaji maeneo  makubwa ili kujenga uchumi wetu.  

Utamaduni wa waswahili wa kutegemea babu, bibi, shangazi, mjomba, baba mdogo na mambo kama hayo,  pia tabia ya Wazanzibar kuchagua kazi za kufanya na kutotambua  kazi ndio msingi wa maendeleo  inadhoofisha uchumi wa Zanzabar.

Dhamira ya Serikali ya kusaidia elimu bure maji bure, wafadhili wanasema hapana hatutatoa msaada kama hamtozi fedha kwenye huduma tunazowachangia. Mfano Wajapani walisimamia mradi wa maji Serikali iliposema itatoa maji bure mfadhili alikataa kwa hiyo serikali ikabidi ifate masharti lakini wananchi hawana uwezo.

SWALI: NIni maoni yako kuhusu Serikali ya Mapinduzi ya Zanziibar kuelekea kwenye uchumi wa viwanda vidogo, vyakati na vikubwa?

JIBU:
Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Serikali ilianzisha viwanda vya Sigara, Manukato, Kiwanda cha viatu, Ngozi, sabuni, chuma na Nguo. Viwanda hivi vilikufa kwa sababu havikustahili kuwepo Zanzibar. Mfano ni lazima uwe na uhakika wa upatikanaji wa malighafi, mali ghafi nyingi zilitoka Bara gharama ya kusafirisha mpaka Zanzibar iliongeza gharama ya uzalishaji. Uanzishwaji wa soko huria uliviua viwanda vya ndani  kwa kuwa bidhaa zitokazo nje ziliuzwa kwa bei  rahisi ukilinganisha na za Zanzibar.

Ushauri wangu Zanzaibar iwe na kiwanda cha kuchakata na kusindika samaki, kiwanda cha matunda pia kitakuwa cha muda maana miaka 20 ijayo hakutakuwa na eneo la kulima matunda wala  karafuu hapa Zanzibar. Maana maendeleo yanafanya majengo makubwa kujengwa zaidi na ardhi ni ileile haiongezeki hali hii itafanya ukulima upungue.

Mimi nadhani mambo ambayo Zanzibar wanaweza kufanya ni mambo matatu: “Mosi  viwanda vya samaki Pili, utalii wa utamaduni na wa kutembelea maeneo ya  kihistoria na Tatu Utalii wa matibabu, yaani kujenga hospitali inayojitosheleza kwa vifaa na madaktari, wakati watalii wakija  Zanzibar kwa matembezi ya maeneo ya kihistoria na utamaduni, anapata nafasi ya kupewa matibabu. Utalii huu ni maarufu sana nchi za Urusi na China.

Pia kwa vijana wa Zanzibar wapewe maeneo ya ardhi Tanzania Bara waweze kulima na kuzalisha chakula ambacho kitapelekwa Zanzibar. Zoezi hili litatoa nafasi ya vijana kujifunza na kuwa na tabia ya kujituma na kupenda kazi.

SWALI Rais kwa kwanza wa Zanzibar Hayati Shekh Abeid Amani Karume ni kati  ya Marais wachache wa Afrika ambao walijitolea kuhakikisha kila mwananchi anaishi kwenye makazi bora nini maoni yako kuhusu suala hili?

JIBU;
Shekhe Karume, aliweka msingi huo kwa sababu kulikuwa na kambi tatu.
Kwanza Mji Mkongwe kwa Wazungu, Waarabu, Wahindi  ambao ni Watawala, Matajiri na Wafanyabiashara.

Pili, Ng’ambu waliishi Waswahili Matopasi, Makuli, Wapishi - kazi yao kuhudumia wakazi wa Mji Mkongwe

Tatu, Shamba kazi yao ilikuwa kulima  eneo hili waliishi  Waafrika masikini sana, kazi yao ni kuzalisha mazao mbalimbali kwa ajili ya  kulisha wakazi  wa  Mji Mkongwe. Nyumba za Waafrika hawa zilikuwa za matope,  nyasi ni vibanda vibanda vibovu tu.

 Hivyo, mara baada ya Mapinduzi Rais Karume aliona lazima abadilishe hali ya maisha ya watu waliokuwa wanaishi katika umaskini uliokidhiri ndio akajenga nyuma za makazi bora Unguja na Pemba.

SWALI: Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalipi la kujivunia kutokana na miaka 53 ya Mapinduzi Tukufu ya Zanzibar?

Lipo la kujivunia ambalo ni mpaka leo Mapinduzi yanakumbukwa naona fahari sana kwa hilo. Kama sio Mapinduzi mpaka kesho Sultani angeendelea kutawala kama sio yeye mwanae au mjukuu wake.
Pili, wakati wa sherehe hizi za Mapinduzi miradi na mipango mbalimbali ya maendeleo inazinduliwa.  Hii inaendeleza   dhamira ileile ya Mapinduzi yaliyokusudiwa mwaka 1964.

SWALI: Suala la Nidhamu kwa Watumishi wa Umma, Taasisi, Mashirika na Idara za Serikali linatiliwa mkazo sana na Rais wa Zazibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein hili unalizungumziaje?

Suala gumu kidogo maana sina takwimu. Hili ni tatizo kubwa sana Zanzibar, Wazanzibar wengi hawajali kazi hawaoni kama maisha yao wanategemea kazi mpaka imekuwa sehemu ya utamaduni wa Wazanzibar. Hivyo lazima mfumo mzima ubadilike na kuona watu wana wajibu wa kazi. Nadhani Rais anahitaji kuungwa mkono kwa hili maana akiachiwa mwenyewe hataliweza ni lazima tulichukulie kwa mtazamo wa pamoja ili kuijenga Zanzibar.

Zanzibar ni ndogo sana na desturi ya Wazanzibar kila siku watu wapo mazikoni harusini kwa shangazi, kwa dada nyakati za kazi huwezi kuamini lakini hayo ndio maisha ya kawaida ya Wazanzibar. 

SWALI: Miaka 53 ya Mapinduzi hali ya kisiasa ikoje Zanzibar?

JIBU:
Hali ya siasa sio nzuri sana inaviza maendeleo ya Wazanzibar, hali hii hujitokeza katika kipindi maalum wakati wa uandikishaji wapiga kura, uchaguzi na mara baada ya uchaguzi.

Zanzibar kuna upinzani wa hujuma na vitisho kwa kambi zote mbili za vyama viwili vikubwa vya siasa katika kipindi hicho maalum wakati wa kujiandikisha kupiga kura wakati wa kupiga kura na baada ya kura, ikipita kipindi hicho nchi inatulia na kuwa salama.

SWALI:
Nini maoni yako kuhusu Mgogoro huo wa kisiasa?

JIBU:
Ni gumu sana chimbuko lake ni viongozi wa Chama cha Mapinduzi - CCM na Chama cha Wananchi - CUF lakini siku viongozi wa Zanzibar wakubwa katika Kambi mbili wataamua kukaa pamoja na kulitatua, litatatuliwa viongozi hao wakubwa wa CUF na CCM  wakikaa na kuamua itakuwa.

SWALI: Unadhani kwa nini vyama vya siasa vya Upinzani vinalalamika kuwa Demokrasia inakandamizwa Zanzibar?

JIBU:
Nadhani tabia au hulka ya nchi za Afrika za kupinga kila kitu wakati wa uchaguzi ili mradi upande wake umeshindwa.

SWALI: Una wito gani kwa Wanzanzibar na Watanzania kwa ujumla?

JIBU:
Kuna haja ya kujenga makumbusho ya kisasa ili kizazi cha sasa na cha baadaye  waone na kujua nini kilitokea kwa nini tunasheherekea Mapinduzi na kwa nini tuko huru sasa. Ni vema kuonyesha katika picha, maandishi na sura halisi historia ya Zanzibar kabla ya Waajemi, Wareno, Waarabu, Waingereza na sasa Serikali ya Mapinduzi.

Vijana wengi ukiwaambia nchi hii kulikuwa na unyanyasaji wa Waafrika hawakubali maana hawajiu historia waelezwe kwa nini tuko huru, kuna wasioitakia mema Zanzibar wanapotosha historia hiyo.
Lazima watu wajue watu walitoka Kongo, Malawi, Kigoma na Tabora wakibebeshwa pembe za Ndovu au Tembo na kusafiri mpaka Bagamoyo, kusafirishwa na boti mpaka visiwani na kuwekwa sokoni kuuzwa kama samaki katika soko la watumwa. Lazima wajue hiyo sio hadith ya kufikirika ni kweli.


Aidha, wengine wakifanyishwa kazi za suluba, masuria, matopasi na kuitwa watumwa maana wametoka Bara.  Hivyo sherehe hizi zinatuhusu wote Watanzania wa Bara na Visiwani.

No comments:

Post a Comment